NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Ndugu Gaudensia Kabaka amewataka Wanawake kuitumia vyema fursa ya Ujasiriamali ili wajiongezee kipato na kujiajiri wenyewe.

Rai hiyo ameitoa katika ziara yake katika Mkoa wa Mjini Kichama wakati akizungumza na Wana CCM huko katika ukumbi wa Kwa Waazee Sebleni Unguja.

Alisema ujasiriamali ni nyenzo pekee ya kuwakomboa wanawake kiuchumi na wakaweza kuwa na uwezo na nguvu za kujiajiri wenyewe.

Ameeleza kwamba CCM kwa sasa ipo katika Sera na Mkakakati wa Siasa na Uchumi hatua inayotakiwa kuchangamkiwa na Akina Mama Nchini, kwa kuanzisha vikundi vya ushirika.

Kupitia ziara hiyo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwalea wazee katika mazingira bora yanayowawezesha kupata huduma zote za msingi za kijamii.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapibduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa busara zake za kuendeleza mambo mbali mbali yaliyoasisiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume hasa kuendeleza Vituo vya ustawi wa jamii vya kuwatunza wazee.

Aliongeza kuwa wazee ndio chimbuko la maendeleo ya Zanzibar kwani wao ndio waliotoa nguvu zao kujenga nchi katika nyanja za kiuchumi, kimaendeleo na kijamii.

Akizungumzia ziara yake katika Wilaya ya Amani aliwapongeza viongozi wa UWT kwa juhudi zao za kubuni masuala mbali mbali ya kuimarisha jumuiya hiyo na CCM kwa ujumla.

Wakati huo huo akizungumza na Akina Mama wa Wilaya ya Mjini aliwapongeza kwa ubunifu wao wa kuanzisha Kituo cha mafunzo ya Amali ya kuwajengea uwezo wa fani mbali mbali Vijana wa CCM ili wapate ujuzi na kujiajiri wenyewe.

Alielezea kufurajishwa kwake na hatua hiyo ya kuwapatia vijana wafunzo ya Ushoni, Uuguzi, Uandishi wa Habari na mafunzo ya Komputer kwani fani hizo alizitaja kuwa zinaendana na wakati wa sasa kiajira.

Sambamba na hayo alitembelea Shule ya Maandalizi iliyopo katika Jengo la UWT Mkele na kuwataka Wazazi na Walezi kuwarithisha Watoto Elimu ili iwasaidie katika maisha yao ya sasa na baadae.

Aidha alitembelea Kanisa la Angilicana la Mkunazini Zanzibar na kujionea kumbukumbu za historia ya Watu ambazo ni miongoni mwa vielelezo vya historia ya Nchi.

Aliwasihi Wanawake Zanzibar bila kujali tofauti za Kisiasa wajitokeze kwa Wingi kushiriki Kongamano la Kitaifa la UWT la kupongeza Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, litakalofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Verde Machi 16,mwaka 2019 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 Mchana ambapo Mawaziri na Manaibu Waziri watazungumzia kwa upana namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walivyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa ufanisi mkubwa.

Katika ziara hiyo alipokea Taarifa za Utekelezaji wa shughuli za UWT Wilaya ya Mjini, Wilaya ya Amani pamoja na Taarifa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mjini.

Bi. Gaudensia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliambatana na Viongozi mbali mbali wa Umoja huo akiwemo Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwaiba Kisasi, Katibu Mkuu wa UWT Taifa Mwl. Queen Mlozi,Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo, Naibu Katibu Mkuu wa UWT Tanzania Bara Ndugu Jesca Mbogo ‘Jasmini’ pamoja na Wajumbe wa Kamati Tekekelezaji wa UWT Taifa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...