Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam. Machi, 2019

Bileku Mpasi ni mwanamuziki  aliyethubutu kuunda kundi la wanamuziki wa dansi katika jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara baada ya kifo cha ‘bosi’ wake Pepe Kalle. Huko nyuma tulishudia wanamuziki wengi wakipotea katika anga za muziki pasipo kufahamika sababu za mzingi mara baada ya viongozi wa bendi zao kufariki dunia.

Bendi ya T.P.OK. Jazz ilitoweka baada ya kufariki kwa kiongozi mkuu wa bendi hiyo marehemu Franco Luambo Makiadi. Wanamuziki waliosalia walijaribu kuiendesha, lakini ilishindikana licha ya kuwepo kwa wanamuziki wakubwa akina Lutumba Simaro Masiya, Kiambukuta Joscky, Madillu System na wengine wengi.

Katika makala hii itamzungumzia Djouna Mombafu ‘Bileku Mpasi’.

Bileku alipokuwa katika bendi ya Empire Bakuba ya Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’, alikuwa kama mnenguaji na ‘mfokaji’. Watanzania tulimshudia miaka ya 1990, ambapo Pepe Kalle na kundi zima la Empire Bakuba walipoachia burudani humu nchini.

Bileku alikuwa akiongoza safu ya wanenguaji wafupi ‘Mbilikimo) akina Emoro na Jolly Bebbe. Bendi hiyo ilisambaratika baada ya kifo cha Pepe Kalle, Bileku akafanya jitihada binafsi ya kuanzisha kundi lake la Orchestra Big One.

Bendi hiyo hivi sasa ni gumzo katika jiji la Kinshasa, na viunga vyake, wakitamba na albamu ya Tonnerre de Brest yenye kibao kikali cha ‘6600 Volts’.

Bileku Mpasi akiongoza kundi hilo, wamefanikiwa kufyatua albam nyingi kwa kipindi kifupi, zilizopelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya nchi yao hususan za Ulaya.

Amekuwa kivutio akionekana kwenye video zake nyingi kwa kuimba na kunengua akishirikiana na wanenguaji mbirikimo, Djuma Fatembo na Jolly Bebe.

Baadhi ya album alizoachia mwanamuziki huyo ni pamoja na Moun Baka Bouger, Karachiga, Tatou, Djouna Big One 6600Volts, Cupidon Brise, Tonnere de Best Onze Onze na Bilibili Bino Moko.

Zingine ni Medaile, Ndule Dekin, Keba na Mopepe, Sur Moradoe, Fin du Match na nyingine nyingi.

Wasifu wake

Bileku Mpasi yasemekana kuwa alizaliwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwishoni mwa miaka ya 1940, akapewa majina ya Bileku Jean-Pierre Matonet

Alichukuliwa na Pepe Kalle kama mnenguaji na rapa wa bendi hiyo. Juhudi zake zilimuwezesha kupanda chati haraka na kuwa maarufu, pengine hata zaidi ya waasisi wenyewe.

Kupanda kwa mafanikio yake kulitokana na umahiri wake mkubwa wa kucheza, kurapu na baadae akawa akiimba.

Hali hiyo ilimfanya Pepe Kalle kufikiria kumpa nafasi ya hisa zake katika bendi hiyo ya Empire Bakuba.

Pepe Kalle alitokea kumpenda sana Bileku na kumuamini, kama alivyofanya marehemu Franco Makiadi  kwa marehemu Madilu System, enzi za uhai wao walipokuwa pamoja katika bendi ya T.P. OK Jazz.

Kasi yake ya kucheza na kurapu kwa wakati mmoja, ndiyo kwa sasa imeigwa na marapa mbalimbali wa makundi ya muziki wa rumba, kuanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kongo Brazzaville hadi humu nchini.

Bileku Mpasi alikuwa akichuana na nyota wa kurap kama Robert Ekokota Wenda wa Wenge Musica BCBG, kabla ya kuibuka wengine kadhaa waliofuata nyayo zao.

Historia yake katika muziki.

Bileku Mpasi alianza  shughuli zake za muziki katika mji wa Kalemi kabla ya kwenda katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Kinshasa mwishoni mwa miaka ya 1970.

Aliwahi kufanya shughuli za unenguaji katika bendi ndogondogo mnamo miaka ya 1980, kabla ya ‘kunyakuliwa’ na Pepe Kalle.

Bileku akiwa katika bendi hiyo ya Empire Bakuba, aliweza kuonesha kuwa anacho kipaji cha kuimba.

Wanamuziki waimbaji wa bendi hiyo Pepe Kalle, Dilu Dilumona na Papy Tex, walimpika hadi akawa mwimbaji hodari.

Ukali wake katika kunengua wakati huohuo akiimba, ulipekelekea kuwafunika baadhi ya magwiji wa uimbaji wa kundi hilo, akiwemo Papy Tex, wakaweka ‘Bifu’ dhidi yake.

Baada ya kifo cha Pepe Kalle Novemba mwaka 1998, kulitokea mtafaruku kama uliotokea katika bendi ya T.P. OK Jazz baada ya kifo cha Luambo Makiadi ‘Franco’ juu ya mustakabali wa bendi hiyo.

Familia ya Franco Makiadi ilimpa uongozi wa bendi ya T.P.OK. Jazz Madilu Sysytem. Kitendo ambacho wakongwe wa bendi hiyo akina Lutumba Simaro Massiya na Kiambukuta Joscky, wakaamua kujiengua na kwenda kuunda bendi yao ya Bana OK.

Ilidaiwa kwamba wanamuziki waliosalia katika bendi ya Empire Bakuba walikuwa na nia ya kuiendeleza bendi hiyo. Waliokuwa na waasisi wa wamiliki wake, Dilu Dilumona na Papy Tex, walianzisha ‘zengwe’ baada ya kufahamika kuwa Bileku Mpasi, alikuwa amepewa usimamizi wa hisa za Pepe Kalle.

Katika njia ya kuepusha shari, Bileku Mpasi na muungurumishaji wa gitaa la zito, Gode Lufombo, waliamua kujiondoa na kuiacha Empire Bakuba.

Wakaenda kujiunga katika kundi la Delta Force, ambalo lilikuwepo hata kabla ya kifo cha Pepe Kalle.

Walipiga muziki katika bendi hiyo ya Delta Force, tangu mwaka 1999 hadi 2002.

Baadae Bileku Mpasi aliamua kujiondoa na kuwa msanii wa kujitegemea na kufanikiwa kufyatua albamu yake ya kwanza ya ‘Tonnerre de Brest’.

Albamu hiyo ina kibao matata cha ‘6600 Volts’, kilichotolewa mwaka 2004 na kumfikisha Bileku kwenye fainali za tuzo za muziki Afrika za Kora (Kora Music Awards), ingawa hakufanikiwa kubeba tuzo yoyote.

Miongoni mwa vibao vilivyomo kwenye albamu hiyo iliyompa mafanikio makubwa kabla ya kuunda Orchestra Djouna Big One.

Bendi hiyo ilitamba kwa albamu zake nyingine mpya za ‘100% TVA’, ‘6600 Volts’ na ‘Cupidon Bris√©’.

Bileku Mpasi  na kundi lake waliachia albam zingine za ‘Fin Du Match’, ‘Karachiga’, ‘Nez a Nez’, ‘Mihona’, ‘ ‘Onze Onze’, ‘Respect Pepe Kalle’ na ‘Tatou’.

Bileku anakumbukwa na Watanzania kwa kuchangia kuibua vipaji vya madansa wa Kitanzania wakati huo alipotinga nchini. Madansa hao ni pamoja na Kokoriko aliyeshabihiana naye kwa unenguaji hata mavazi, Maxi Prest na Mrisho Mpasi.

Baadhi ya wanamuziki wetu hapa nchini wameanzisha bendi zao ambazo zinafanya vizuri katika ‘game’ la muziki.

Hapa nawazungumzia Hussein Jumbe na kundi lake la Talents Band, Banana Zorro, Mafumu Bilal, Lady Jdee, Deo Mwanambilimbi na kundi lake la Kalunde Band, Kanku Kelly na kundi la The Kilimanjaro Connection, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ kundi lake la La Capitale na wengine wengi.

Wito wa makala hii kwa wanamuziki wetu humu nchini, wawe wabunifu kwa kutengeneza vyao badala ya kukopi vya wenzao.

Mwisho.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...