Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF).

Hatua hiyo imekuja baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yaliyofunguliwa na Katibu wa CUF, Maalim Seif Hamad  aliyekuwa akiiomba mahakama kutoa amri ya kubatilisha barua ya Msajili wa vyama ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
 Katika uamuzi wake, Jaji Benhaji Juma Masoud amesema,  mjibu maombi namba moja, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alikuwa na mamlaka ya kutoa ushauri na maamuzi kwa chama husika ili wahusika wachukue hatua stahiki.

Katika shauri hilo, Maalim Seif alikuwa akiwakilishwa na Wakili Juma Nassoro na Loveness Denis huku wajibu maombi ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Lipumba na wanachama wengine wa CUF waliwakilishwa na Mashaka Ngole.
Akiendele kusom uamuzi huo, Jaji Msaoud amesema, baada ya migogoro iliyotokea ndani ya chama hicho, Msajili aliandika barua kutoa msimamo na ushauri kwa Uongozi wa juu wa CUF ambapo katika barua hiyo ilimtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Amesema, majukumu ya Msajili hayaishii katika kusajili vyama pekee bali pia anayo mamlaka ya kufuta vyama na kutoa msimamo kitu ambacho ndio alichokifanya. Hivyo kanuni ambazo waleta maombi wanataka zirejewe na kuelekeza kile wanachokiona zinatupiliwa mbali na kuongeza kuwa hatatoa amri yoyote kuhusu gharama.

Jaji Masoud amesema,  kwenye kiapo chake Maalim Seif alisaini mwenyewe kikionyesha kuwa alipata mamlaka hayo kutoka kwenye bodi ya wadhamini wa chama hicho na kuonesha  kuwa pamoja na kuwa Katibu Mkuu, pia alikuwa Mhasibu Mkuu.

Ameongeza,  kwenye kiapo hicho hakukuwa na maelezo ya bodi ya wadhamini yaliyomruhusu Maalim Seif kusaini kiapo hicho wala hakukuwa na nyaraka yoyote inayoonesha maelezo ni wakati gani idhini ya kufungua kesi hiyo ilitolewa na wakina nani.

Aidha amesema, katika kiapo kinzani kilichotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga idhini hiyo, alitoa kielelezo ambacho kina orodha ya majina ya bodi ya wadhamini lakini wakati wa Maalim Seif kujibu hoja hiyo, hakuonesha kama ameipinga au kukubali bodi hiyo ya wadhamini iliyoainishwa na msajili.

‘’Katika hoja ya waleta maombi kwamba mjibu maombi wa tatu (Profesa Lipumba) aliitisha kikao isivyohalali na kuunda watu watano kuwa wadhamini katika kufanikisha adhma ya kufungua akaunti nyingine, watu hao waliotajwa kwenye kiapo hicho wapo kwenye kiapo cha Msajili na Mwanasheria wa Serikali (AG),’’ alisisitiza Jaji Masoud.

Alieleza kuwa mleta maombi alipaswa kubainisha nani ni nani ambaye alitoa idihi ya kufungua shauri hilo mahakamani na kwamba kifungu cha 8 (1) inayoelezea kiapo haikutekelezwa kwa sababu Maalim Seif hakusema idhini ilitolewa katika kikao kilichoketi siku gani.

‘’Kwa msingi huo, muombaji ni mtu mmoja na sio bodi ya wadhamini kwa sababu haikuoneshwa kama nafasi ya Katibu ni sehemu ya wadhamini. Katika taarifa yoyote haikuoneshwa kama Maalim Seif ni sehemu ya bodi hiyo,’’alifafanua.

Maalim Seif na wenzake walikuwa wanaiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF, wakidai kuwa hana mamlaka na imzuie kuingilia masuala ya ndani ya kiutawala ya chama hicho.

Wanadai kuwa Profesa Lipumba alishajiuzulu nafasi hiyo na Katiba yao ya chama haina utaratibu wa kiongozi kujiuzulu na kutengua tena uamuzi wake huo na kurejea katika nafasi hiyo na kwamba si mwanachama kwani alishavuliwa uanachama.

Hata hivyo, Profesa Lipumba na wafuasi wake wanadai kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF, hususan ibara ya 117 (2) mchakato wa kujiuzulu kwake ulikuwa bado haujakamilika.

Wanadai kuwa ili uamuzi wa kujiuzulu ukamilike, ni lazima mamlaka ya uteuzi wake (mkutano mkuu wa Taifa wa chama) ukae na kuridhia au kukataa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...