Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam. Machi, 2019.

Johnny Bokelo alizaliwa mwaka 1939 nchini Kongo, nje kidogo ya jiji la Kinshasa. Familia yake ilikuwa ni ya wanamuziki. Johnny alikuwa mdogo wa Paul Ebengo’Dewayon’ Isenge.

Mwanamuziki mwingine aliyekuwa mkubwa sana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, toka mwanzoni mwa miaka ya 50, alikuwa Dewayon.

Alikuwa na bendi inaitwa Watam, ambako  Johnny Bokelo,  alipoanzia akipiga muziki akiwa na mtoto mwingine wakati huo akiwa na miaka 12, aliyekuja kutikisa ulimwengu wa muziki Franco Luambo Luanzo Makiadi


Bokelo aliendelea kupiga katika bendi alizoanzisha kaka yake Paul Ebengo’Dewayon’ Isenge.


Bendi hizo ni kama Konga Jazz na Orchèstre Cobantu, lakini mwaka 1958 John akaanzisha bendi yake, Orchestra Conga Success, akiwa na mdogo wake Mpia Mongongo, maarufu kwa jina la Porthos Bokelo.

Mpia wakati huo alikuwa mpiga gitaa la rhythm kwa umahiri mkubwa sana. 

Kaka yao Dewayon, akaja kujiunga na kundi hilo 1960, lakini miaka miwiwli baadae mwaka 1962,  Johny na kaka yake Dewayon wakatengana. 

Bokelo alifanikiwa kulijenga kundi lake kuwa na nguvu, likawa kwa namna fulani linafanana sana kimirindimo ya T.P.OK Jazz.

Hata tungo nyingine zilikuwa ni za kujibu tungo za T.P.OK Jazz au kuzungumzia mada ambayo imeanzishwa na  wenzao hao. 

Kuna wakati Bokelo alianzisha kuimba nyimbo alizozipa jina la Mwambe no 1 na 2 mpaka 5. Katika nyimbo hizo alikuwa akiongea na kushangaa jamii inaelekea wapi. Upigaji wa gitaa wa Bokelo, Dewayon na Franco ulishabihiana, pengine ni kutokana na wote kuanzia bendi ya Watam.

Mwaka 1968 Johnny Bokelo akabadili jina la kundi lake la Conga Success na kulita Conga 68, akaanzisha label yake, akaanza kutoa santuri. Kitendo hicho kilimuongezea kipato japo wanamuziki wake walitishia kuachana nae.

Walidai kuwa hawakuwa wanapata fedha zozote kutokana na mradi huo.

Santuri nyingi wakati huo alikuwa akiziachia kwanza kutoka nchini Ufaransa, ili kupata mapato zaidi. 

Kati ya 1972 mpaka 1974 Bokelo Isengo alikuwa anatumia muda mwingi zaidi akiwa studio. Kwenye mwaka 1970 viwanda vya kutengeneza santuri vya Kinshasa vikawa vimechoka hivyo bokelo akaanza kupeleka master zake ili kutengeneza santuri. 

Mwaka 1980 Bokelo aliachana kabisa na shughuli za muziki.

Ni miaka 24 imepita tangu kifo cha Johnny Bokelo Isenge, kilichotoke Januari 15, 1995, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwisho.

Mungu alilaze roho yake pahala pema peponi, amina.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...