*Asema ushindi wa Taifa Stars ni wa Watanzania wote

*Asisitiza sasa timu yoyote itakayokuja nchini itapigwa tu



Na Said Mwishehe,Globu ya jamii



KAMATI ya Saidia Taifa Stars ishinde yenye wajumbe 14 wakiongozwa na Mwenyekiti wao Paul Makonda imetoa shukrani kwa Watanzania wote kwa kufanikisha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kushinda mechi yake dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda.




Taifa Stars waliifunga Uganda mabao 3-0 na hivyo kufanikiwa kuipeleka Tanzania nchini Misri kwenye michuano ya AFCON mwaka 2019.Ushidni wa Taifa Stars umeifanya nchi yetu kuandika historia ya aina yake baada ya miaka 39.



Akizungumza leo Machi 26,2019 jijini Dar es Salaam Makonda amesema  Kamati ya Saidia Taifa Stars ishinde inatoa shukrani kwa makundi mbalimbali kwa kufanikisha ushindi huo ambao ni Watanzania wote.



"Nitoe shukrani kwa  wapenzi ,wakereketwa na wadau wote wa michezo. Walihakikisha Taifa Stars inashinda kwa kushiriki kwenye dua na sala.Kamati yetu ilikuwa na kazi kubwa mbili , kwanza ni kuhakikisha Taifa Stars inashinda na mbili kufuatilia mchezo mwingine wa Lethoto na Cape Verde.



"Baada ya Rais wa TFF kuteua kamati hii tulihakikisha  hatukuangushi na tunafahamu tulipoteza mechi yetu dhidi ya Lethoto ambako kwa sehemu fulani kulikatisha tamaa.Tuliwepa kazi ngumu,"amesema Makonda.



Amefafanua ili kuhakikisha kamati inatimiza majukumu yake ilichukua jukumu la kuunda makundi mbalimbali yakiwamo ya watu mashuhuri, mastaa katika tasnia ya sanaa nchini, wanamichezo wa zamani, wenye mahoteli, wenye baa,vyombo vya habari na wenye vyombo vya usafiri.



Amefafanua katika nchi yetu klabu za Simba na Yanga ndivyo vyenye mashabiki wengi wa soka, hivyo aliona haja ya kuwachukua Haji Manara na Jerry Muro ambao nao aliwaita kwenye kamati hiyo na hakika wametoa mchango mkubwa katika kusaidia kuunganisha mashabiki wa vilabu hivyo.



Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema pamoja na kazi hiyo Kamati yao ilihakikisha inairudisha timu ya Taifa Stars kwa Watanzania na kazi hiyo imefanikiwa kwani hapo awali ilionekana kama vile haina mwenyewe na baada ya hapo ndipo likaja wazo la kutafuta watu mashuhuri.



"Kazi ya pili ilikuwa kuzungumza na vyombo vya habari kusaidia kuhamasisha. Jambo la tatu ni kuhamasisha kwenye maeneo yenye watu wengi kama baa, hoteli na vyombo vya usafiri ili nao wato ruhusa ya kujadili kwa mchezo wa Uganda na Tanzania kama sehemu ya kuhamasisha.Kazi ambayo imefanikiwa na wote tumeona,"amesema Makonda.



Amefafanua ushiriki wa makundi hayo ya kufanya kazi ya kuhamasisha, Uwanja wa Taifa ulizidiwa kwa idadi ya watu ambapo ametumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa wote waliokuwa na tiketi zao lakini hawakuingia uwanjani na kwamba wamejifunza , hivyo watajipanga isitokee tena.



"Kwa namna ambavyo walijitokeza kwa wingi uwanjani maana yake Watanzania wanapenda mpira na michezo mingine yote. Tutaendelea kushauri ikiwemo ya tiketi kukatwa mapema na pale ambapo uwanja utakuwa umejaa basi watu wambiwe mapema,"amesema Makonda.



Pia amempongeza Kocha wa Taifa Stars kwa kupanga kikosi kizuri cha ushindi na kufafanua zawadi ya viwanja ambayo imetolewa na Rais Dk.John Magufuli wataweka uratatibu utakaosaidia hata wale wachezaji ambao walikuwemo kwenye ile michezo ya awali nao wanapewa.



"Kwa namna ambavyo Watanzania wamehamasisha na timu yetu ya Taifa, nina uhakika timu yoyote itakayokuja Uwanja wa Mkapa lazima itapigwa tu.Mashabiki ni mchezaji wa 12 na sasa tunao , hatuna wasiwasi na timu yetu,"amesema Makonda.


KAMATI ya Saidia Taifa Stars ishinde yenye wajumbe 14 wakiongozwa na Mwenyekiti wao Paul Makonda ikitoa shukrani kwa Watanzania wote kwa kufanikisha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kushinda mechi yake dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...