Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
JALADA la kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake wanane sasa kuanza kuunguruma, kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Awali kesi hiyo ilikuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina  baada ya hakimu aliyekuwa akiisikiliza kuanzia ilipofikishwa mahakamani hapo, Wibard Mashauri kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. 

Hakimu Simba amepanga kuanza kuisikiliza kesi hiyo kwa siku mbili mfululizo, Machi 28 na 29, 2019

Mapema wakili wa serikali Simon Wankyo alidai,  kesi hiyo hiyo leo Machi 14, 2019 imekuja kwa kutajwa baada ya kuamuriwa kurudishwa mahakamani hapo baada ya Matiko na Mbowe kupata dhamana ambayo wameisotea zaidi ya miezi mitatu kifuatia kufutwa kwa dhamana zao kwa kukiuka masharti ya dhamana. 

Hakimu Simba ameieleza mahakama kuwa, ni jana tu ndio amepewa maelekezo kuwa shauri hilo limepengwa mbele yake kwa kuwa Hakimu  aliyekuwa akisikiliza awali amebadilishiwa kituo cha kazi.

Hakimu Simba amesema kesi hiyo itaendelea pale ilipoishia na ameutaka upande wa mashtaka kuwasomea upya washitakiwa mashitaka yanayowakabili ambayo wote wamekana.

Hata hivyo, baada ya kusomewa mashitaka yao, wakili Wankyo aliiomba mahakama irejee uamuzi wa mahakama kuu kwamba shauri hilo lisikilizwe haraka iwezekanavyo. Hivyo  alimuomba na hakimu apange tarehe ya kuanza kusikiliza kesi hiyo ili walete mashahidi.

Wakili wa utetezi Profesa Abdalah Safari aliiomba mahakama ipange tarehe za usikilizwaji kulingana na dayari yao kwakuwa wanakesi zingine katika mahakama kuu na wameshalipwa.

Hata hivyo, Hakimu Simba alikataa ombi hilo na kusema kuwa kesi hiyo inawakili wengine wa utetezi hivyo wanaweza kumwakilishwa.
kwani mahakama haiwezi kupanga tarehe kulingana na dayari za mawakili mawakili, kama  mmoja hàtakuwepo mawakili wenzie watakuwakilisha, "sheria inaelekeza kesi zisikikizwe mapema ziishe"ameeleza Hakimu Simba.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...