Na Teresia Mhagama, Pwani

Imeelezwa kuwa, kazi mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ( MW 2115) zinazofanywa na Mkandarasi kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric zimefikia zaidi ya asilimia 4O.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea eneo la mradi lililopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na Serikali ikiwemo Barabara, umeme, nyumba za Wafanyakazi na sehemu maalum ya kushushia mizigo katika Stesheni ya Tazara katika Kituo cha Fuga.

Dkt. Kalemani, alisema kuwa, Mkandarasi huyo ameanza kazi za maandalizi mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo la mradi mwezi wa Pili mwaka huu. 

Alisema kuwa, miongoni mwa kazi ambazo Mkandarasi anaendelea kutekeleza kwa sasa ni ujenzi wa kambi ya muda ya Wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi pamoja na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kukamilisha kazi hizo za maandalizi Mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya ujenzi ndani ya miezi 36.

Alieleza kuwa, pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo ya maandalizi, bado Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kumsimania mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, baada ya kukagua miundombinu iliyotekelezwa na Serikali pamoja na kazi za maandalizi zinazofanywa na Mkandarasi, aliipongeza Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo na kuusimamia kikamilifu.

Alisema kuwa, Kamati hiyo pia inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini ambapo pia alitoa wito kwa Wizara kutorudi nyuma katika usimamizi wa mradi.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwani Serikali itatumia takribani shilingi Trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo hivyo ni muhimu watanzania wafaidike na fedha hizo.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali waliambatana na Kamati hiyo akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka pamoja na wataalam kutoka kampuni inayotekeleza mradi huo.
 Moja ya nyumba inayojengwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambapo katika eneo hilo kunajengwa  kambi ya muda ya Wafanyakazi wa mradi huo.

 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kutoka mbele) wakiwa  katika eneo ambalo litatumika kutekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufanya  ziara katika eneo la mradi huo.

 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula (katikati), Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Gulamali (wa Pili kulia) wakimsikiliza mtaalam kutoka kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric wakati akizungumzia mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115).

 Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt Tito Mwinuka (katikati) wakikagua eneo kutakapotekelezwa mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115), wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati), akizungumza na Wataalam wanaosimamia na wanaotekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufika katika eneo la mradi huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akiwaongoza baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mara walipofika katika eneo kutakapotekelezwa mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115), wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...