Jopo la Madaktari bingwa wa Upasuaji wa Ubongo,Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI kwa kushirikiana na Madaktari bingwa wa Pua, Koo na Masikio wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakifanya upasuaji Mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye Ubongo kwa kupitia kwenye tundu la pua. (PICHA NA KHAMISI MUSSA)



NA KHAMISI MUSSA

Madaktari bingwa wa Upasuaji wa Ubongo ,Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI kwa kushirikiana na Madaktari bingwa wa Pua, Koo na Masikio wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye Ubongo kwa kupitia kwenye tundu la Pua (Endoscopic Trans nasal transsphenoidal pituitary surgery) ambao ulikua haufanyiki hapa nchini.


Upasuaji huo wa kihistoria umefanywa kwa mafanikio makubwa na jopo la madaktari bingwa wazalendo wanne kwa kutumia muda wa masaa matatu ambapo wamefanikiwa kuondoa uvimbe wote.



Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu MOI, Dkt Lemery Mchome amebainisha kwamba upasuaji huu umefanyika kwa mafanikio makubwa na mgonjwa hatatumia muda mwingi hospitalini na ataruhusiwa kwenda nyumbani ndani ya siku chache.



“Upasuaji huu ni wa kisasa na wenye matokeo chanya kwa mgonjwa kwani tunaondoa uvimbe kwa kupitia puani badala ya kufungua fuvu kama ambavyo imezoeleka ambapo mgonjwa anatumia muda mwingi kurudi kwenye hali ya kawaida, pia kwa njia hii mgonjwa hatahitaji kupumua kwa kutumia mashine baada ya upasuaji na tutamruhusu ndani ya siku chache zijazo” Alisema Dkt Lemery



Dkt Lemery amesema upasuaji huu umewezekana kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali katika miundombinu pamoja na wataalamu hivyo madaktari bingwa Wazalendo wanaweza kufanya upasuaji huo bila ya utegemezi wa wataalamu kutoka mataifa mengine.



Kwaupande wake daktari bingwa wa magonjwa ya Masikio, Pua na Koo Dkt Edwin Liyombo Kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema upasuaji huu wa kuondoa uvimbe kwa kupitia kwenye tundu la pua ni wa kisasa na wenye matokeo bora zaidi ya njia iliyozoeleka ya kufungua fuvu.



“Tumefanya upasuaji huu kwa mafanikio makubwa sana, tunaamini mgonjwa atakuwa salama na atakwenda nyumbani mapema, awali wagonjwa hawa walilazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa, kwakuwa vifaa vipo hapa MOI tumeamua tushirikiane kuwahudumia Watanzania wenzetu hapa nchini na kuipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa gharama kubwa” alisema Dkt Liyombo.



 Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli umepelekea huduma nyingi za kibingwa ambazo zilikua hazipatikani hapa nchini kuanzishwa na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...