Mafumu Bilali ni kati ya wanamuziki wachache waliopo katika tasnia ya muziki aliyeanza kupiga muziki mwaka 1973 hadi leo. Vipaji vya mwanamuziki huyo ni vya pekee ambapo anamudu kupuliza Saxophone ‘mdomo wa bata’ anao umahiri mkubwa katika kulicharaza gitaa la solo na rhythm.

Halikadhalika Mafumu ni mtunzi na mwimbaji mzuri wa nyimbo licha ya yeye kuchelewa kugundua kipaji hicho. Amepata mafanaikio makubwa kupitia vipaji vyake hivyo ambavyo amekuwa akivitumia ipasavyo na kupelekea kuweza kuzuru nchi nyingi za bara la Ulaya na Asia kwa nyakati tofauti.

Mafumu hivi sasa ni mzee wa miaka 60, aliyezaliwa mjini Kigoma eneo la Mwanga, barabara ya Legeza Mwendo mwaka 1958. Alipata kupata elimu ya msingi katika shule ya H.H. Aga Khan. 

Alipofika darasa la sita ndipo alipong’amua kuwa anapenda muziki. Hii ilitokana na yeye kumshuhudia mjomba wake Shem Karenga, aliyekuwa akipiga gitaa la besi katika bendi ya Lake Jazz wakati huo.

Umahiri wake wa kupuliza saxophone ulipelekea kupewa jina la ‘Super Sax’. Mafumu alidhamiria moyoni kuwa aje mwanamuziki kama mjomba wake huyo, licha ya kuwa na vikwazo kutoka kwa baba yake aliyekuwa hapendi kabisa mambo hayo.

“Nikafaulu kuingia kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kazima iliyopo mjini Tabora ambako nilikosoma hadi kidato cha nne…” anasema Mafumu Bilali. Akiwa shuleni hapo alisema walikuwa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba na mbunge wa Tabora mjini, Alhaj Ismail Aden Rage. 

Mafumu alisema baada ya kumaliza shule alikwenda Makutupora Dodoma jeshini kwa mujibu wa Sheria na mwaka 1973, huko ndiko alikojifunza kuimba na kupuliza Saxophone. Yakatangazwa majina ya vijana walipata ajira, jina  lake halikuwepo lakini aliambiwa asubiri orodha nyingine.

Super Sax akaamua kutoroka kwenda Morogoro  kujiunga katika bendi ya Morogoro Jazz. “Nilikwenda kujiunga na Morogoro Jazz bila kuwa na ndugu katika mji huo, yaani nilikwenda moja kwa moja kwenye bendi na nikapokewa wakati huo ndio hayati Mbaraka Mwinshehe wakati huo alikuwa katika harakati za kuondoka kwenda kuunda bendi yake ya Super Volcano…” alitamka Mafumu.

Alisema kwamba hakukaa sana na bendi hiyo akaamua kwenda katika jiji la Dar es Salaam kwa kaka yake. Mwaka uliofuata wa 1973, aliingia katika bendi ya Western Jazz alikoshiriki vyema kupiga Saxophone. Akiwa na bendi hiyo waliokuwa wakitumia mtindo wa ’Saboso’, ikiwa chini ya uongozi wa Shamba Ramadhani.

Aliutaja mshahara wake wa kwanza kupokea akiwa na bendi ya Western ni Sh. 275, ambazo alizitumia zote kununua nguo.  “Nilikuwa naishi kwa kaka yangu kila kitu bure ‘kula kulala’, nilikuwa napenda sana kuvaa, hivyo nikautumia mshara wote kununulia nguo. Wakati huo sikuwa mnene kama leo nilinunua suruali za mtindo wa bugaluu, viatu virefu vilivyokuwa vikiitwa  raizoni na mashati ya kubana ‘slim fit’ ya kutosha.

Hapo ndipo nilianza kuona umuhimu wa kuwa mwanamuziki na jinsi gani natakiwa kung’ara…” Mafumu alisema huku akicheka. Anaeleza kuwa wakati huo hakuwa akiimba bali alikuwa anapuliza mdomo wa bata na kupiga rhythm gitaa. Mwanamuziki huyo ameeleza kuwa wakati akiwa katika bendi ya Western Jazz, wapinzani wao wakubwa ilikuwa ni bendi ya Dar Jazz, waliokuwa wakijiita  ‘majini wa bahari’, wakitumia mtindo wao wa ‘Mundo’.

Bendi hizo wakati huo pamoja na kupiga muziki, pia zilikuwa ni wapinzani wa jadi katika soka. Western Jazz ilikuwa ni mashabiki wa Klabu ya Yanga ingawa yeye hashabikii timu hiyo na Dar Jazz ni  ilikuwa na wakishabikia klabu ya Simba. Hivyo bendi hizo zilijigawa katika mtindo huo.

Ilikuwa marufuku na haikutokea bendi ya Western kupiga kwenye tafrija za Simba halikadhalika kwa Dar Jazz vile vile kwenye shughuli za Yanga.
“Mamluki kama mimi wasiokuwa wanachama au mashabiki wa timu inayoshabikiwa na bendi husika, tulikuwepo lakini mashabiki na wapenzi wa bendi hizi walijigawa katika mtindo huo Western Yanga na Dar Jazz Simba, ilikuwa wenyewe huwaambii kitu hasa matajiri wa Western na ushabiki wa soka wa zamani ulikuwa wa kweli…” alifafanua Mafumu.

Akiwa katika bendi hiyo ya Western Jazz, nyimbo ambazo zilitamba wakati huo zilikuwa za Jela ya mapenzi, Rosa, Vigelegele, ‘Kazi ni Kazi’ na Hakika. Mafumu hakusita kutaja baadhi ya vibao kadhaa alivyoshiriki katika bendi hiyo kuwa ni pamoja na ‘Hakika’, na ‘Sadaka’.

Ameutaja ukumbi mkuu wa bendi hiyo kuwa ulikuwa Community Centre, ambao kwa sasa Makao Makuu ya Wilaya ya Kinondoni, maeneo ya Magomeni Mapipa. Mafumu aliaeleza safari yake ya muziki ilivyoanza kwa kusema kuwa kama siyo moyo wa dhati wa kupenda muziki, wala asingefika hapo alipo. Baba yake mzazi aliyekuwa mganga maarufu mkoani Kigoma, alikuwa hataki ajiingize kwenye muziki.

 “Baba mzee Bilali hakutaka kabisa kusikia muziki alipenda nisome sana dini, lakini nilikuwa kila nikipata nafasi nilikuwa natoroka kwenda kwenye muziki…” alieleza Mafumu. Hivi sasa ni baba wa familia na watoto wake saba katika makazi yao maeneo ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

Historia yake katika muziki Mafumu alieleza kuwa inaanzia mwaka 1972 nilipojiunga na bendi ya Morogoro Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Mbaraka Mwishehe Mwaruka, akitokea JKT Makutupora. Alianza rasmi kujiingiza kwenye tasnia ya muziki mwaka 1973, lakini hadi leo ni moto wa kuotea mbali kutokana na kuwa maahiri wa kufanya kazi hiyo ambayo kwa mujibu wake atakufa akiifanya.

Mwaka 1978 aliamua kwenda katika jiji la Dar es Salaam. Alipotinga jijini humo, mwaka uliofuatia wa 1979 ‘alitua’ katika bendi ya Vijana Jazz. Hapo akatunga kibao ‘Taabu’ na pia kushiriki kukiimba. Halikadhalika akipuliza Saxophone kwenye vibao kama ‘Chiku’ na ‘Matata Ndani ya Nyumba’.

Ilipotimu mwaka 1980, Mafumu alihamia katika bendi ya Maquis du Zaire. Huko alikutana na miamba mingine wa kupuliza Saxophone akiwemo Chinyama Chiyaza, Suleiman Akulyake ’King Maluu’, Alex Kanyimbo, Mukuna Roy na  Khatib Itei Itei kwa nyakati tofauti.

Akiwa na bendi hiyo alipuliza ‘mdomo wa bata’ kwenye vibao vingi, baadhi yake ni ‘Zoa’, ‘Sina Ndugu’, ‘Noel Christmas’ pamoja na ‘Mage’. “Nilikaa Maquis hadi mwaka 1984, nilipochomoka tena na kuhamia katika bendi Bima Lee Orchestra iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Bima la Taifa. Huko nilikokutana na wakali wengine katika muziki kama Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shaaban Dede Kamchape ‘Super Motisha’, ‘Joseph Mulenga ‘King Spoiller’…” alisema Mafumu.

Mwaka 1985 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya MK Group ‘Ngoma za Maghorofani’, iliyokuwa ikiporosha muziki wake katika ukumbi wa Bandari Grill, ulipo katika hotel ya New Africa. Bendi hiyo ilikwa ikiongozwa na Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’. Hapo alikutana na wanamuziki wengine akina Andy Swebe, Asia Darwesh, Kayembe Ndalabu ‘Trumblo’ Omari Makuka na wengine wengi.

Mwaka 1986 alikwenda Iringa akawa tena mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Tancut Alimasi ya mjini humo. Mwaka 1987 alirejea tena MK Group ambapo wimbo wake wa kwanza kupuliza Saxophone awamu hiyo ya pili ilikuwa ni ‘Utakuja kuanguka kwenye matope’.Mwaka 1989, kaka yake Adam Kinguti alirudi nchini akitokea Sudan, alipokuwa akifanyakazi kwenye ofisi za Ubalozi.

Wakaanzisha bendi ya Bicco Stars, yeye akashiriki kupuliza Saxophone kwenye vibao kadhaa kama vya ‘Magret Mage’, ‘Wapangaji’ na Kisamvu’. Mwaka 1991 Mafumu alitoka katika bendi hiyo ya Bicco akiwa na mpapasaji kinanda mahiri wa kike Asia Daruweshi, baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na Kinguti. Wakaamua kuanzisha bendi yao ya Zanzibar Sound.

“Tukiwa na Zanzibar Sound, tulipata mkataba katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha na mwaka mmoja baadaye mwanamuziki mwenzetu kwenye bendi hiyo, Kanku Kerry Nkashama, alipata mkataba nchini Japan. Tukaondoka naye kwa sharti la sasa kujiita Kilimanjaro Connection…” anasema Mafumu Bilali.

Walizunguka nchi nyingi za bara la Asia wakiwa na bendi hiyo ya Kilimanjaro Connection. Waliporudi mwaka 1994, alijitoa katika bendi hiyo na baadae kidogo Asia Darwesh nae alijitoa, akairudisha upya bendi yake ya Zanzibar Sound na kurejea mkataba wake Bahari Beach Hotel.

Mafumu yeye alibaki bila bendi, ambapo muda si muda, Asia Darweshi alipata kazi nchini Bahrain na kumuachia Super Sax mkataba wake wa kupiga muziki katoka hoteli ya Bahari Beach. Baada ya kuona ameachiwa mkataba wakati hana bendi, Mafumu ndipo alipomfuata Baraka Msirwa na kumuomba vyombo vya muziki ambapo alimpa kwakuwa havikuwa na kazi kutokana na kufa kwa bendi za MK Group, MK Beat na MK Sound walivyokuwa wakivitumia.

Bendi ya African Beat ilianzishwa mwaka 1998, baada ya Mafumu Bilali kujiengua kutoka katika bendi ya African Stars ambayo nayo ilianzishwa mnamo mwaka 1994 kwenye Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, huku yeye akiwa ndiye mwanzilishi. Mafumu anakumbuka kuwa, wakati akiwa na African Stars ambayo hata jina lake alilibuni yeye, walitamba na vibao kama ‘Sakatu Sakatu’, ‘Mayanga’, ‘Maya’, ‘Afrika’ na ‘Dance Dance’.

Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi hilo la African Stars linalojulikana zaidi hivi sasa kama ‘Twanga Pepeta’, ni Bob Gady, Andy Swebe, Alfa Nyuki, Palmena Mahalu, Pamela pamoja na Hamisi Kayumbu ‘Amigolas’. “Hicho ndio kilikuwa chanzo cha bendi ya African Stars niliyoibuni mwenyewe hadi jina, lililoniletea uhasama mkubwa na dada yangu Asha Baraka baada ya kujitoa,” anasema Mafumu Bilali.

Akiwazungumzia wanawe amesema ana wawili  ambao wanaoonekana kufuata vyema nyayo zake, ambao ni Feruzi, anayepapasa kinanda na Aziza ambaye ni mwimbaji. Aidha Mafumu Bilali amekuwa mmoja kati ya wanamuziki wachache humu nchini walioamua kuunda bendi zao binafsi. Wengine wanaomiliki bendi zao ni akina Hussein Jumbe anayemiliki bendi yake ya Talent, Banana Zorro na Matei Joseph anayemiliki bendi yake ya African Minofu.8m

Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...