Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

 Mahakama ya Rufani Tanzania,   Machi 12, 2019  imesikiliza mashauri manane ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kwa kupitia mfumo wa video conference.

Rufaa hizo zimesikilizwa kwa mara ya kwanza kwa njia hiyo katika Kituo cha Mafunzo kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na Mahakama ya Mbeya.,   

Rufaa zilizosikilizwa ni za mkoa mbeya na Rukwa ambapo miongoni mwa rufaa hizo ni ya Venance Kazuri dhidi ya Eldard Sospeter  pamoja na Agness Sanga dhidi ya Among Halinga na Peter Haonga ambazo zimesikilizwa mbele ya Jaji Jacobs Mwambegele.

Pia rufaa namba 38/2018 ya aliyekuwa Askari polisi namba F 5842 DC, Maduhu dhidi ya jamhuri na  namba 1/2019 ya Charles Kalunga na wenzake dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) mbele ya Jaji Rehema Mkuye.

Rufaa nyingine ni pamoja na rufaa namba 3/2018 ya Festo Sodi dhidi ya Ihombe Village Council na kesi namba 100/2018 ya Osward Mruma dhidi ya Mbeya City na rufaa namba 2/2018 ya Ismail Shaban dhidi ya Jamhuri zilizosikilizwa mbele ya Jaji Sivangirwa Mwangesi.

Pamoja na rufaa ya Faman Investment (T) Ltd dhidi ya Dk Anthony Nsonjo na wenzake iliyosikilizwa mbele ya Jaji Gerald Ndika.

Akizungumza  baada ya  usikilizwaji wa mashauri hayo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu amesema, usikilizwaji was mashauri kwa njia ya video conference inapunguza gharama na kwamba inalenga utoaji wa haki kwa wakati.

Amesema, garama inayotumika kuendesha video conference ni Sh 140,000 kwa siku ambayo ni tofauti na majaji kusafiri na watumishi wao kwenda Mbeya kwa ajili ya kusikiliza mashauri hayo.

Ameongeza kuwa faida kubwa ya mfumo huu husaidia kupunguza gharama kwani ili majaji waweze kwenda Mbeya kusikiliza mashauri inawapasa kulipia gharama kubwa za malazi yao pamoja na watumishi wao wanaoongozana nao lakini mfumo huo unatumia Sh 70,000 kwa Kisutu na 70,000 kwa Mbeya ili kukamilisha usikilizwaji huo.

Mkwizu amesisitiza kuwa mashauri yote ya Mbeya na Sumbawanga walitakiwa wafuatwe lakini kwa mfumo huo wanatimiza malengo ya mahakama ya utoaji wa haji kwa wote na kwa wakati.

Moja ya rufaa iliyosikilizwa ni ya Sanga ambaye yupo Mbeya na hakuwa na Wakili kupitia video conference aliiomba mahakama (Jaji ambaye alikuwa Kisutu) kumuongezea muda wa kufungua ili kukata rufaa dhidi ya Halinga na Haonga ambao wanadaiwa kuuza nyumba ya urithi.

Sanga amedai sababu ya kuongezewa muda ni baada ya Mahakama Kuu Kanda hiyo kumkatalia kuomba kesi kusikilizwa nje ya muda. Amedai, alicheleweshewa kupewa nakala ya hukumu ambayo ilitoka Julai 14, 2017 na kupata nakala hizo Agosti 4, 2017 hivyo alichelewa kufungua kesi.

"Kila mtu anatakiwa aridhike na kile alichokitafuta kwa juhudi zake na isiliwe na mtu mwingine hivyo, naomba nipatiwe haki hiyo," alidai Sanga.

Hata hivyo, wadaiwa hao waliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu katika hati ya kiapo mdai hakueleza sababu ya kuchelewa kukata rufaa kuwa ni kucheleweshewa hukumu lakini alichoeleza ni kwamba alikuwa mgonjwa.

"Tunaomba mahakama itupilie mbali maombi haya kwa sababu mdai ni muongo kwani alichoeleza kwenye hati ya kiapo ni tofauti na anachoeleza," walidai.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Mwambegele alisema atapitia hoja zote na atatoa uamuzi kuhusu shauri hilo na kwamba watajulishwa  tarehe ya uamuzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...