*Ni baada ya Ofisi ya Msajili kutoa barua ya kusudio la kukifuta Chama hicho
*ACT Wazalendo wajitetea kwa kukiri kupeleka hesabu kwa CAG,wagusia udini

Na Said Mwishehe,Globu ya jmii

CHAMA cha ACT Wazalendo kupitia Kiongozi wake Zitto Kabwe kimefafanua na kuweka wazi kuhusu tishio la Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka kukifuta chama hicho ambapo pamoja na mambo mengine wamejibu hoja moja baada ya nyingine.

Kauli ya Zitto inakuja baada ya jana Machi 25,2019,Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwaandikia barua ACT-Wazalendo ambayo kwa sehemu kubwa ilijikita katika mambo matatu na kisha kutoa kusudio la kutaka kukifuta.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa jambo la kwanza ni hoja zinazohusu ukaguzi wa hesabu ,pili ni vitendo vya kuchomwa hadharani kwa bendera na kadi za chama cha CUF na tatu ni matumizi ya neno Takbiri kama yalivyoonekana katika baadhi ya video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza leo Machi 26,2019 akiwa katika Makao Makuu ya ACT-Wazalendo Zitto amesema kuhusu ukaguzi ni kwamba barua ya Msajili wa vyama vya siasa inadai ACT imekiuka sheria ya vyama vya siasa kwa kutopeleka kwake hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 kama sheria inavyotoka.

Amesema tuhama hizo hazina ukweli wowote kwasababu wajibu wa Chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) na kwamba hesabu za mwaka 2013/2014 ziliwasilishwa kwa CAG na kufafanua Chama hicho kilianzishwa kwa kupata usajili wa kudumu Mei 5 ,2014 miezi miwil kabla ya mwaka wa fedha wa Juni 30,2014. 

"Kwa kutumia kanuni za kimataifa za kihesabu na kwa ushauri wa CAG ,Chama chetu kilielekezwa kinaweza kuunganisha hesabu za mwaka 2013/2014 na 2014/2015 katika ripoti moja.Na hili ni jambo la kawaida kabisa katika kanuni za uhasibu kwani inaruhusu kuunganishwa hadi miezi 18 .ACT ilikuwa na miezi 14 tu.

" Kabla ya kuchukua uamuzi huu wa kuunganishwa hesabu,Chama chetu kilimwandikia Msajili wa vyama vya siasa kwa barua mbili zenye kumbukumbu namba AC/HQ/ MSJ/ 2015/006 na AC/ HQ/ MSJ/ 2015/008 za tarehe 22 na 29 Januari 2015.Naye alijibu na kuridhia hesabu za miezi miwili za mwaka 2013/2014 kuunganishwa kwenye mwaka wa fedha 2014/2015,"amesema.

Zitto ameongeza taarifa zote hizo ziko wazi kwa CAG na kama Msajili wa vyama vya siasa angekuwa na nia njema angeweza tu kuuliza na angepewa taarifa sahihi.Kazi ya Chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na sio kwa kukagua hesabu zake chenyewe.

"Tulitimiza wajibu wetu huo, CAG naye alitimiza wajibu wake kwa kutukagua ,hivyo basi Chama chetu kwa sasa hakuna mwaka ambao hakijawasilisha hesabu zake.Kwa mwaka 2015/2016 na 2016/2017 chama kina hati safi na mezani kwake.

" Mambo haya ya ukaguzi yako nje ya wigo wa uelewa wa Msajili na ndio maana sheria za nchi zinampa CAG wajibu wa kufanya mambo haya na ukaguzi wa msajili kuwa mlezi wa vyama vya siasa.Msajili afanye mambo anayoyajua,asiyoyajua aachane nayo,"amesema Zitto.

Kuhusu kuchoma bendera na kadi, Zitto amesema barua yenyewe ya Msajili iliyowafikia inasema kuwa hana uhakika kama kweli wahusika ni wanachama wa ACT Wazalendo wakichoma bendera na kadi za chama cha CUF.

"Katika hili Msajili mwenyewe anaonesha hana uhakika kama kweli wahusika ni wanachama wa ACT.Inashangaza anafika uamuzi wa kuandika barua ya kutishia kutufuta kama chama cha siasa kwa tuhuma ambazo hata yeye mwenywe hana uhakika nazo," amefafanua.

Kuhusu Takbir ,Zitto amesema barua ya Msajili wa vyama vya siasa inaeleza chama chao kimevunja sheria ya vyama vya kwasababu wanaodaiwa kuwa wanachama wao wametumia maneno ya takbiri kwenye shughuli za kichama na kwamba maneno hayo ni udini.

"Jambo hili limetushangaza na kutuudhi kwa wakati mmoja.ACT ni chama cha watu wa dini zote na hata wale wasio a dini.Katiba yetu ya Chama tumeonesha wazi hatufungamani na dini yoyote na ndio sababu tumeruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa.Hata hivyo tunafahamu watanzania wana dini zao na wana maneno yao ambayo ni ya kawaida kutumia na hayana uduni wowote.

"ACT haitaki kuamini kusema Takbir kwa muumini wa dini ya Kiislam au hata kwa Mkristo ni udini .Jambo hili tunaachia wanazuoni na waumini wa dini ya Kiislamu walieleze vizuri na kumfahamisha Msajili kwamba hakuna udini wowote katika neno hilo la kuitiana hamasa kwa wahusika,"amesema Zitto.

Amefafanua barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina nia njema kwa ACT Wazalendo na wapenda demokrasia wote hapa nchini huku akiitumia nafasi hiyo kuomba Msajili kuangalia na kutafakari kwa upana kuhusu hiyo barua yake na ikiwezekana aifute mara moja kwani inaonesha namna ambavyo nia yake sio nzuri kwa Chama hicho. Hata hivyo amesema barua ya Msajili haiwatishi na wala hawatatishika na kusisitiza kuwa ACT inafanya shughuli zake za kisiasa kwa misingi ya kuheshimu na kuifuata Katiba ya nchini na kwamba wanachama wao kokote waliko wahakikishe wanaheshimu Katiba.
 Waandishi wa habari wakifautilia mkutano wa CHAMA cha ACT Wazalendo kupitia Kiongozi wake Zitto Kabwe alipokuwa akifanunua mambo mbalimbali kuhusiana na tishio la Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka kukifuta chama hicho ambapo pamoja na mambo mengine wamejibu hoja moja baada ya nyingine.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...