Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

MENEJA Rasilimali watu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mary Samson, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, haelewi ni shtaka gani ambalo vigogo watano wa shirika hilo wanashtakiwa nalo. 

Pia amedai hajui kama bodi ya Wakurugenzi ya TPDC ndio waliopeleka tuhuma zinazowakabili vigogo hao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) au la.

Mary ambae ni shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka ameeleza hayo leo Machi 21, 2019 wakati akijibu swali la Wakili wa utetezi Emmanuel Makene lililomtaka aieleze Mahakama kama anafahamu washtakiwa wanakabiliwa na kesi gani mahakamani hapo na kama shirika hilo ndilo lililowashtaki ama la.

Katika keai hiyo, vigogo wanaoshtakiwa ni, Mkurugenzi Mtendaji James Mataragio, Kaimu Meneja wa Uvumbuzi, George Seni, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala Wellington Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba na Edwin Riwa ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa mipango.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina, shahidi Mary amedai

mshtakiwa James Mataragio aliteuliwa na Rais lakini hajawai kupokea barua kutoka kwa Rais ya kumsimamisha kazi mshtakiwa huyo wala hajawai kupokea barua kutoka kwa Rais ya kumuelekeza Mwenyekiti wa bodi ya TPDC kumsimamisha kazi mshtakiwa huyo. 

Amedai, washtakiwa hao mpaka leo bado ni watumishi wa TPDC isipokuwa walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ambazo yeye hazijui. 

Akiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru Aneth Mavika kutoa ushahidi wake shahidi Mary amedai kuwa nyaraka za watumishi wa shirika hilo zipo katika majalada yanayotunzwa kwenye masijala ya siri na kuongeza anawafahamu washtakiwa kwa kuwa ni watumishi wenzie na ni mabosi zake ila kwa sasa wamesimamishwa kazi.

Amedai majalada ya washtakiwa hao, yalichukuliwa ofisini kwao Januari mwaka huu na kuyapeleka Takukuru baada ya taasisi hiyo kuyahitaji kwa ajili ya uchunguzi.

Amedai, Januari mwaka huu, shirika lilipokea hati kutoka Takukuru iliyoelekeza kuhitaji majalada hayo agizo ambalo walilitekeleza kwa kukabidhi majalada hayo kwao.

Akifafanua kuhusu jalada la mshtakiwa mmoja mmoja, amedai mshtakiwa James jalada linaonesha kuwa mtumishi huyo aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Desemba 15,2014 ambapo alidumu katika nafasi hiyo hadi Agosti 24,2016 aliposimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili. 

Mshtakiwa George Seni yeye inaonesha aliajiriwa TPDC Februari ,2014 na kutakiwa kuendelea na wadhifa aliokuwanao kutoka ofisi za Bunge ambapo alikuwa Mhasibu Mkuu hata hivyo alipofika TPDC hakukuwa na cheo hicho hivyo kupewa cheo cha Mkurugenzi wa Fedha. 

Kwa upande wake, mshtakiwa Wellington Hudson aliajiliwa TPDC Mei 23, 1989 kama Mtaalamu wa Jiolojia na Juni, 2015 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala ambapo alidumu katika cheo hicho mpaka Julia 14, 2017 aliposimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili. 

Pia Mary amedai, mshtakiwa Kelvin Komba aliajiriwa TPDC, Mei 23, 1989 na April 2014 aliteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa mipango aliyodumu nayo hadi Agosti 24, 2016 aliposimamishwa kazi kupisha uchunguzi. 

Kuhusu mshtakiwa Edwin Riwa naye aliajiriwa Desemba 12, 2009 kwa nafasi ya Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi baadae cheo hicho kilibadirishwa jina na kuitwa Meneja Manunuzi, baada ya mchakato Januari, 2015 alikuwa Meneja Manunuzi na alikaa katika nafasi hiyo hadi Agosti 24, 2016 aliposimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka na wanadaiwa kuwa walitenda kosa hilo kati ya April 8, 2015 na June 3,2016.

Inadaiwa wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.

Inadaiwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika.

Inadaiwa kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyohalali ya dola 3,238,986.50 ambazo ni sawa na Sh7.2 bilioni kwa Bell Geospace.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 16, itakapokuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...