WENYEVITI wa Vitongoji na Vijiji wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutokwamisha shughuli za serikali kwa kutoa matamko yasiyo na tija kwenye machimbo ya madini.

Ofisa madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima aliyasema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wa madini ya Green kwenye machimbo ya Lemshuku Kata ya Komolo.

Ntalima alisema wenyeviti hao wanapaswa kutambua kuwa Rais John Magufuli akishatoa maelekezo hawapaswi kuyakwamisha kwa kutoa kauli tofauti. Alisema baadhi ya wenyevi wanatoa maagizo yasiyo na tija ambayo yanakinzana na kauli ya Rais Magufuli ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini. 

"Hili ni eneo la uchimbaji madini, Mwenyekiti wa kijiji au kitongoji hana mamlaka ya kutoa matamko ya kuwachangisha watu sh15,000 au kuwaagiza waendelee kwenye mkutano kilomita 18 kutoka hapa," alisema Ntalima. Alisema viongozi hao wanapaswa kushirikiana na ofisi ya madini endapo kuna jambo wanataka kulifanya kwenye maeneo ya madini yenye leseni kuliko kujiamulia wao wenyewe. 

"Rais Magufuli amewapa unafuu wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwasamehe kodi sasa anapotokea mwenyekiti wa kijiji anawachangisha fedha lazima tuingilie kati," alisema Ntalima. 

Mwenyekiti wa chama cha wachimba madini mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Lemshuku, Bernard Kasanu alisema wenyewe wana haki ya kuchimba na siyo kuwekewa vikwazo vya kisiasa visivyo na tija. Kasanu alisema wamekuwa wakipata vikwazo vingi kutoka kwa uongozi wa kijiji ikiwemo huduma ya maji ambayo hivi sasa imesimama. 

Mchimbaji wa madini ya Green, Charles Shoo alisema viongozi wa wizara ya madini na kijiji wangekutana ili wapeane utaratibu wa suala hilo kwani wananchi wamebakia njia panda. Shoo alisema tatizo hilo ni la muda mrefu hivyo ni wakati muafaka wa kufanyiwa kazi ili lipatiwe ufumbuzi wa kudumu. 

Hata hivyo, mmoja kati ya wachekechaji wa madini hayo Shedrack Ibrahim alisema viongozi wa vijiji na vitongoji wanapaswa kutoa kipaumbele kwenye huduma za kijamii kuliko kuwachangisha fedha bila utaratibu wowote. 

Ibrahim alisema machimbo hayo hayana sehemu za kuwazikia wenzao wanapokufa hivyo wanaomba serikali iwatengee sehemu ya maziko machimboni. Mkoa wa kimadini wa Simanjiro unaongoza kwa kuwa na madini mengi katika mkoa wa Manyara, ikiwemo Tanzanite, Rubby na Green.
Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima akikagua migodi ya madini ya Green kwenye machimbo ya Lemshuku Kata ya Komolo. 
Maofisa wa Tume ya madini, wakikagua migodi ya madini ya Green kwenye machimbo ya Lemshuku Kata ya Komolo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara. 
Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima akizungumza na wachimbaji madini ya Green kwenye machimbo ya Lemshuku Kata ya Komolo. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...