*Ni baada ya Polisi, DC Kinondoni kufanya msako usiku wa manane
*Ng'ombe waliopewa mafunzo maalumu watumika kubeba magendo 
*Waliohusika wakimbia nyumba...sasa msako wa nyumba kwa nyumba kufanyika

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii 

SUKARI bandia kilo 350 na mafuta ya kupikia madumu 25 ambayo hayana ubora yamekamatwa katika eneo la Mbweni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Sukari na mafuta hayo ya kupikia yamekamatwa usiku wa kuamkia leo, Machi 12.2019 eneo la Mbweni ambako kumebainika kuwepo kwa bandari bubu ambayo watu wasiowaaminifu wanatumia bandari hiyo kuingiza bidhaa za magendo na kibaya zaidi zisizokuwa na ubora.

Msako mkali uliofanyika usiku wa kuamkia leo, kupitia Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi Mbweni kilichopo katika Wilaya ya Konondoni pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo wamefanikiwa kukamata bidhaa hizo za magendo.

Kwa mujibu wa Polisi Mbweni ni kwamba wanaopitisha bidhaa hizo za magendo wamekuwa wakitumia ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo hilo na kisha baada ya kuingiza bidhaa hizo nchi kavu wanatumia ng'ombe ambao wamepata mafunzo maalumu kwa ajili ya kubeba mizigo hiyo na kukimbia nayo kwa ajili ya kufichwa.

Akizungumza akiwa katika Kituo cha Polisi Mbweni ambako ndiko bidhaa hizo za magendo zimehifadhiwa, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo amesema, kutokana na msako mkali ambao umefanywa na Polisi wamekamata bidhaa hizo ambapo kimsingi ni hujuma kubwa kwa Serikali kwani wanaopitisha wanakwepa kodi na kibaya zaidi wanahatarisha maisha ya wananchi.

"Baada ya kufanyika kwa msako huu usiku kucha tumekamata mifuko 70 ya sukari na kila mfuko una kilo 50, hivyo kwa ujumla tumekamata kilo za sukari 350 pamoja na mafuta madumu 25.Haifahamiki hii sukari na haya mafuta yanatoka nchi gani lakini wanaofaya biashara hii haramu wakifika nchi kavu wanachukua hiyo sukari na kisha kuijaza kwenye mifuko ya sukari ambayo inazalishwa nchini na kisha kwenda kuuza.

Hata hivyo amesema kuwa jahazi au boti ambayo imetumika kuleta sukari hiyo baada ya kuona Polisi wamefika eneo la tukio wahusika waliirudisha kwenye maji na hivyo haikufanikiwa kupatikana kwani iliondolewa.

Chongolo amesema Serikali haiko tayari kuona zinaingizwa bidhaa ambazo ziko chini ya ubora na wanaofanya hivyo watambue mwisho wao umefika na wote ambao wamehusika watachukuliwa hatua kwani majina yao yamefahamika.

Amefafanua kuwa kwa sasa sukari kutoka nje hairuhusiwi kuingizwa nchini kwani viwanda vilivyopo vinazalisha sukari ya kutosha huku akifafanua sukari ambayo wameikamata haijathibitishwa ubora wake wala inakotoka.

"Hatuwezi kukubali kuona wananchi wanadhuruka.Huu msako ambao tumeuanzisha ni endelevu na utaendelea kila siku, wale ambao wamezoea kufanya biashara kiujanja ujanja ikiwa pamoja na kukwepa kodi watambue mwisho wao umefika.

Amesema kitendo cha kuingiza sukari ambayo haina ubora inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupata saratani ya tumbo au vidonda vya tumbo."Hii sukari ambayo tumeikamata haijulikani ni ya viwandani ama wapi? Wanaohusika na michezo hii wajue hatutawaacha."

Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Polisi Kawe Dk. Ezekiel Kyogo amesema bidhaa hizo zinapitishwa kupitia bandari bubu na matokeo yake kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi.Amefafanua baada ya kufanya uchunguzi wao wamebaini nyumba zinazotumika kuficha bidhaa za magendo pamoja na majina ya wahusika ambao wengine wamekimbia nyumba zao baada ya kufanyika msako.

Amesema kuwa watu wanne wanashikiliwa na Polisi kutokana na kutuhumiwa kuhusika kwenye kuingiza bidhaa hizo za magendo na sheria itachukua mkondo wake."Tutafanya msako nyumba hadi nyumba kuhakikisha wote ambao wamehusika wanachukuliwa hatua".

Kuhusu jahazi ambalo limetumika kuleta bidhaa hizo za magendo, Dk.Kyogo amesema wameshindwa kulipata kwani walikimbia eneo la tukio.
Mkuu wa Wilaya ya KInondoni Mh Daniel Chongolo akioneshwa bidhaa hizo za Magendo zilizokamatwa leo katika Bandari Bubu,Mbweni jijini Dar
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya  Kipolisi Kawe ,Dkt Ezekiel Kyogo  akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Daniel Chongolo (kulia) mashine iliyokuwa ikitumika  kwenye boti za kubebea mizingo ya magendo kutoka baharini katika Bandari Bubu ya Mbweni jijini Dar es Salaam.

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh.Daniel Chongolo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kukamatwa kwa bidhaa mbalimbali za magendo katika Bandari Bubu ya Mbweni,leo jijini Dar.
 Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya  Kipolisi Kawe ,Dkt Ezekiel Kyogo akitoa ufafanuzi namna bidhaa hizo za magendo zilivyokamatwa katika bandari bubu,Mbweni jijini Dar. 
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya  Kipolisi Kawe ,Dkt Ezekiel Kyogo  akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Daniel Chongolo (kulia) Ng'ombe wanaobeba mizingo ya magendo kutoka baharini katika  Bandari Bubu ya Mbweni jijini Dar es Salaam.
Bidhaa mbalimbali za magendo zilizokamatwa katika bandari Bubu ya Mbweni jijini Dar es Salaam .
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Daniel Chongolo akipewa maelezo na
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Kawe ,Dkt Ezekiel Kyogo mara baada ya kukamatwa bidhaa za magendo katika ufukwe wa Mbweni (bandari Bubu),leo jijini Dar

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh DaniellChongolo akizungumza jambo na vijana wanaodaiwa kutumika kubeba mizigo hiyo ya magendo inapofikishwa nchi kavi,Mbweni jijini Dar

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...