Na Shamimu Nyaki-WHUSM 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalojulikana kama JAMAFEST linatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 21-28 mwaka huu. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Dkt.Mwakyembe ameeleza kuwa Tamasha hilo linaloongozwa na Kauli mbiu “Uanuai wa Kitamaduni;Msingi wa Utengamano wa Kikanda,Maendeleo ya Kiuchumi na Kushamiri kwa Utalii. Lengo lake ni kulinda na kuendeleza Urithi wa Utamaduni na kukuza utambulisho wa Afrika Mashariki. 

Ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo litawezesha uhamasishaji wa Sanaa na Utamaduni kwa kutangaza vivutio vya kitalii na utamaduni vilivyopo nchini,kutangaza fursa za kiuchumi na kijamii pamoja na mandhari mazuri ya upigaji picha na filamu kwa wadau wa kitaifa kikanda na kimataifa. 

“Tamasha litaunganishwa na matamasha mengine ya Utamaduni nchini ikwemo Usiku wa tuzo za Serengeti International Film Festival pamoja na tukio la watu sita watakaopanda Mlima Kilimanjaro na kupeperusha bendera za nchi zao juu ya kilele cha Mlima huo kuashiria uzinduzi wa Tamasha hilo la JAMAFEST”alisema Dkt.Mwakyembe. 

Mhe. Mwakyembe ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo litakuwa na maonesho mbalimbali ya kiutamaduni ikiwemo mavazi asili, sanaa ya uchongaji,wabunifu wa vifaa vya mapambo,michezo ya kuigiza watunga riwaya na mabingwa wa lugha ya Kiswahili,watengenezaji wa vyakula na michezo mbalimbali ya Jadi. 

Aidha Dkt. Mwakyembe ameisitiza Watanzania kushiriki katika tamasha hilo kwa kuuza na kutangaza kazi zao za Sanaa na Utamaduni kwani nchi yetu mwaka huu imebahatika kuwa na matukio makubwa yenye fursa ya kuitangaza nchi ikiwemo Sekta ya Michezo kwani timu ya Taifa Stars na Serengeti Boys zinatarajiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya Afrika ya AFCON. 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bibi.Joyce Fissoo amesema kuwa Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini ambapo nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi Sudan Kusini na Mwenyeji Tanzania zinatarajiwa kushiriki. 

Bibi Fissoo ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Rwanda mwaka 2013 ambalo lilihudhuriwa na washiriki17,500 Kenya ikafuatia mwaka 2015 kwa kuwa na washiriki 21,000 na Uganda mwaka 2017 ambapo washiriki 42,600 walijitokeza. 

“Tamasha hili linafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi hizo wanachama wa Jumiya ya Afrika Mashariki kwa kila baada ya miaka miwili kwa mujibu wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki la mwaka 2012”.aliongeza Bi Fissoo. 

Tamasha hilo linaratibiwa na Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara nyingine,pamoja na Kamati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi wanachama. 
.Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe (Katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 20/2019 Jijini Dar es Salaam kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalojulikana kama JAMAFEST linalotarajiwa kufanyika septemba 21 -28 2019.Wa Kwanza kulia  ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi Joyce Fissoo na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara hiyo Bibi Leh Kihimbi.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi Joyce Fissoo(katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 20/2019 Jijini Dar es Salaam kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalojulikana kama JAMAFEST linalotarajiwa kufanyika septemba 21 -28 Kushoto ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe na Kulia ni Katibu Mtendaji wa BASATA Bw.Godfrey Muingereza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...