Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam
Tshala  Muana ni mwanamuziki maarufu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwenye vituko visivyolingana na umri wake awapo jukwaani. Mama huyo hivi sasa ni mtu mzima mwenye umri wa miaka 61 sasa, alizaliwa Mei, 13, 1958 katika mji wa Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Majina yake halisi anaitwa Elizabeth Tshala Muana Muidikay. Ni mama mwenye sura na umbile la kuvutia kwa mtu yeyote atakayemuona.Tshala Muana anavyo vipaji vingi kikiwemo cha kutunga na kuimba pamoja na uwezo mkubwa kunengua jukwaani.

Mama huyo alianza muziki mwaka 1977 akiwa katika bendi iliyokuwa na majina ya Tsheke Tsheke Love. Elizabeth Tshala Muana Muidikay maarufu kama ‘ Malkia wa Mutuashi’  au ‘Kasa wa Mutshanda’ ni bingwa  wa miondoko ya mtindo wa Mutuashi ulio na sili ya utamaduni wa kabila la Baluba toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwaka 1982 aliamua kuwa mwanamuziki wa kujitegemea na akaweza kupata mafanikio makubwa kwa kazi zake. Katika kipindi cha miaka 20 ya kuvuja jasho, Tshala alifyatua album 19 mnamo mwaka 2002. Tshala Muana ameunda kikundi chake kiitwacho Dynastie Mutuashi. Baadhi ya nyimbo ambazo bado zinaendelea kutamba ni pamoja na Dezo dezo, Karibu yangu, Kokola, Tshbola, Seli Pere, Mutuashi, Amina, Chena, Nasi Nabali, Benga na Na respect.

Zingine ni pamoja na Baba Nima, Vundula, Sukisa, Mpokolo, Golgotha na Lekela Muadi. Tshala ameachia ngoma nyingine za Malu Parole, Tshaza, Dinanga, Nkashama, Dikeba, Tshikuna Fou, Cicatrice d’amour, Viluka Dilolo, Burkina Faso, Nguma Yanyi na Luadia Bombo

Muana amekwisha shida zawadi katika mashindano ya Kora Award mwaka 2003 kama mwanamuziki bora wa kike toka nchi za Afrika ya Kati. Katika sherehe hizo za Kora Award, Muidikay hakuweza kuhudhuria kufuatia hali ya uchumi ulokuwa ukimkabiri wakati huo. Muana baadaye katika mahojiano na vyombo vya habari alikiri kwamba yeye pamoja na wanamuziki wake  walitakiwa kuwa na Pauni 4,000 kwa ajili ya usafiri wa ndege  wa kwenda Afrika ya Kusini  kuhudhuria na kupokea zawadi yake.

Wakati huohuo mwanamuziki mwanamuziki mwenzake Charls Antonie Kofi Olomide, alikuwa amepata bahati ya ya kupata tiketi kumi toka kwa waandaji wa Tamasha hilo. Wasanii wengine toka nchi mbalimbali walihudumiwa na serikali zao, bingwa huyu wa Mutuashi aliwahi kukiri katika mahojiano kushindwa kwake kuhudhuria sherehe hizo akisema zilihitajika Dola za Kimarekani 4,000 kwa ajili tiketi za ndege kwa yeye na wanamuziki wake kwenda Afrika ya Kusini.

Akiwa kama mwimbaji bora wa Mutauashi, Afro- Cuban aliyoitambulisha huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tshala Muana anajulikana mno kwa umahiri wa kulimiliki jukwaa akicheza kwa kujiachia na wakati mwingine huwaduwaza wapenzi na mashabiki wa muziki pale anapoamua kucheza wa asili ya Baluba na kuachia ‘Nyeti’ zake zikiwa wazi.

Wanamuziki wake nyota anaowahusudu anawajumuisha kina Emedo Wabafike, Jojo Kashama na wengine wote wanaotoa mchango kuendeleza muziki wa KiKongo.
Fikra zake kubwa ni kuwa Produza mkubwa, kuwa na Studio kamambe katika jiji la Kinshasa ya kurekodia muziki kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya vijana wanaochipukia katika muziki.

Tshala Muana alijipatia umaarufu mkubwa hapaTanzania pale alipokopi na kuimba wimbo wa Dezo dezo kwa umahiri wa aina yake. Awali wimbo huo ulipigwa na Orchestra Safari Sound chini ya Supreme Fred Ndala Kasheba. Pia alitoka na wimbo mwingine aliouimba kwa lugha ya Kiswahili unaoitwa Karibu yangu. Nyimbo nyingine ni pamoja na Malu, Mbombo na Menteur.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...