Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam
Tshimanga Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za Negro Success, Les Kamalee, Lipua Lipua na Fuka Fuka. Akiwa katika bendi hizo alishirikiana wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na Georges Kiamuangana Mateta Wazela Mbongo ‘ Verckies’.

Asossa hata leo utakapokutana nae mitaani au ukimuona awapo jukwaani, hauwezi kudhani kuwa ni mzee wa miaka 68 hivi sasa. Ni mtanashati, mcheshi asiye na majivuno pia hupenda kuongea na watu wa rika zote. Tshimanga Asossa ana vipaji vya kutunga na kuimba nyimbo za muziki wa dansi pia ni hivi sasa ni kiongozi wa bendi ya Bana Maquis.

Mwandishi wa makala hii alimtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa alizaliwa katika mji wa Kamina uliopo Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo tarege Aprili 04, 1949. Asossa alipata elimu ya Sekondari katika shule iliyojulikana kama Charles Ruangwa hapo Kamina.

Alianza kuimba akiwa bado mdogo na kwamba alijipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina ambako Mapadri walimsaidia kumfunza muziki. Pamoja na juhudi zake hizo, Baba yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye ajitumbukize katika muziki,  alimtaka afuate masomo yake shuleni.

Baada kumaliza kidato cha nne, baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Asossa muziki ulikuwa ndani ya damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo hapo Kamina ya Super Gabby.

Ikumbwe Super Gabby ndiyo ilikuja kubadilishwa majina hatimaye ikaitwa Orchestra Maquis du Zaire, iliyoingia humu nchini mwaka 1972. Mazoezi hayo yalimtia hamasa kubwa ya kupenda muziki.

Siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa kuimba katika bendi hiyo. Asossa alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla baba yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko. Pamoja na makatazo yote hayo, hatimaye baba yake alikubali ombi la mwanaye baada ya kubaini kuwa hashikiki wala habadiliki kitabia.

Mwaka 1969, Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana na mwanamuziki Bavon Marie Marie akampeleka kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo aliyejulikana kama Didi Kalombo.

Asossa aliitumia vyema nafasi hiyo ya kujaribiwa sauti ambapo mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika bendi hiyo. Asossa anazikumbuka changamoto alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti na wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo).

Pamoja na hayo, sauti yake ndiyo iliyomuokoa na kupewa heshima kama wanamuziki wengine. Kiongozi wa bendi ya Negro Success Bavon Marie Marie alipofariki kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye ikafa. Mwaka 1974 Assosa alikutana na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa bendi ya Lipua Lipua, aliyejulikana kwa majina ya Kiamuangana Mateta Wazela Mbongo "Vickie’s".

Alipofika huko alitakiwa kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka. Hata hivyo, hakujua ujasiri aliupata wapi siku hiyo pale alipomtamkia mmiliki huyo kwamba hayuko tayari kuimba sauti ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.

Akajiunga na bendi ya Orchewstra Lipua Lipua ambako aliungana na wanamuziki wengine wakali. Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya Mombasa, Nikibwe na Amba. Mwaka 1975 bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na wanamuziki. Asossa aliamua kuondoka na kwenda kujiunga na Bendi ya Les Kamale.

Akiwa na Les Kamale walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na nyingine nyingi. Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa sifa na kujiamini kupita kiasi. Hiyo ilitokana na kitendo cha kulipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao vya muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo.

Mbwembwe zikazidi na kusababisha kusahau wajibu wao katika kazi, zilizopelekea bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975. Baada ya hapo Asossa alikaribishwa kujiunga katika bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma. Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tanzania.

Fuka Fuka ilipoingia Dar es Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga Funga ambazo alizielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa jiji la Dar es Salaam wakati huo. Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga muziki kwa miezi sita na Chama cha mateksi Dereva cha Tanzania Transport, Tax and Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park.

Baada ya kumaliza mkataba Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi nchini Kenya na Kampala huko Uganda. Wakiwa Kampala kwa bahati mbaya nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani, ikipigana na Tanzania mwaka 1979.

Vita hivyo viliiwaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia, wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ilihali kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha yake. Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita. Akiwa Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa muziki wa Tanzania, akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule.

Baada ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Asossa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986. Akiwa hapo alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani. Mwaka huo huo aliamua kuanzisha bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na maadili mema.

Bendi hiyo ilijengewa mizengwe na kusababisha kasambaratika baada ya muda mfupi. Assosa alichukuliwa na bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987. Alipigia bendi ya Maquis hadi ilipo sambaratika. Baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo akiwemo yeye walijipanga na kuisuka bendi kwa jina jipya la Maquis Original.

Wakaaza kupiga muziki katika ukumbi wa Wapi Wapi’s na baadaye wakaenda Kata ya 14 huko Temeke jijini Dar es Salaam. Maquis Original ikafanya makao yake makuu katika ukumbi mpya wakati huo wa Lang’ata uliopo Kinondoni mano miaka ya 1990. Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia utanashati wake.

Baadaye alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi. Baada ya kumaliza mkataba aliungana na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya Bana Maquis. Anawataja akina Kasongo Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’.

Tshimanga Kalala Asossa licha ya kufaya muziki, pia mtunzi wa vitabu. Ameweza kutunga kitabu cha ‘JIFUNZE LINGALA KWA KISWAHILI’, ambacho kipo sokoni nchi nzima. Aidha husikika akitafsiri na kuuelezea muziki na wanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo cha Cavacha Time kila Jumamosi asubuhi kupitia TBC FM.

Assosa ana familiya ya mke na watoto kadhaa. Mkewe ni binti wa aliyepata kuwa na nyadhiza nyingi zikiwemo za ubunge na  Uwaziri Bwana Paul Kimiti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...