Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.

Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.

Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.

“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.

Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.

Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema “ Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.

Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.

Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa. 
 Eneo la Nyumba ya mtuhumiwa ambaye ni Mganga wa Kienyeji wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite mjini Sumbawanga baada ya nyumba hiyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kubaini kuwa mganga huyo amesababisha vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa mahututi. 
  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Vuta Sangu Sokoni juu ya tukio la kupotea kwa watoto watatu na hatimae kupatikana wawili wakiwa wamefariki na mmoja kuwa mahututi akiendelea na matibabu.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akionyesha eneo katika nyumba iliyokuwa haijamalizika ambapo maiti za watoto hao zilipatikana baada ya kutupwa na mtuhumiwa James Kapyela ambae ni mganga wa kienyeji. 
  Diwani wa Kata ya Kizwite ambae pia ni mchungaji Felician Mavazi (alipiga magoti) akiomba muda mfupi kabla ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Mh. Joachim Wangabo kuongea na wananchi wa mtaa huo wa Vuta kata ya Kizwite juu ya tukio la mauaji ya watoto wawili. 
-Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akiongea na wananchi wa mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite Sumbawanga mjini. 

  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa pole kwa wazazi waliofiwa na watoto wao alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mara tu baada ya kupata taarifa ya vifo vya watoto wawili na mmoja kuwa mahututi baada ya kupatikana tangu kupotea kwao tarehe 21.3.2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...