WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema kwa sasa umechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha miti bora ya asili iliyopo nchini inaendelea kuwepo kwani tayari kuna tishio la miti hiyo ikiwemo ya Mpingo, Mninga,Mkongo na Mvule kutoweka nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Meneja wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti-TFS mkoani Morogoro Dk.Hamnza Katety amesema wanapotafuta miti hiyo hata mahali ambako waliamini ipo wanaikosa.

"Kuna miti tuliyozoea kuiona katika nchi yetu na sasa imeanza kupotea .Miti hiyo maarufu imekuwa adimu kuipata na hata ikipatakana haiko kwenye ubora unaostahili.Mninga,Mkongo, Mvule na Mkakangazi imeanza kupotea kabisa.

"Hatua ambazo TFS tunachukua ni kuhifadhi mbegu bora za miti hiyo, tuna mashamba ya mbegu bora ambayo yameanzishwa.Tayari miti ya mvule, mkongo na mkangazi imepandwa katika vishamba vidogo,"amesema Dk.Katety.

Ametoa rai kwa Watanzania kuhakikisha wanashiriki kuitunza miti hiyo ambayo ni alama katika nchi yetu na huenda ni mpango wa Mungu kwa kuweika katika ardhi ya Tanzania.

Akizungumzia mbegu bora, Dk.Katety amesema kupitia Kituo cha uzalishaji wa mbegu za miti Morogoro ambacho kipo chini ya TFS Wizara ya Maliasili na Utalii kitaendelea kuzalisha mbegu bora na kushauri ni vema wananchi wakapata ushauri kabla ya kununua mbegu.Amesema matarajio ya TFS ni kuhakikisha kunakuwa na mashamba mengi ya mbegu bora za miti ambapo itasaidia kupunguza gharama kubwa inayotumika kununua mbegu kutoka nchi nyingine na hasa Zimbabwe.

Amesema tayari wageni wameanza kutambua mashamba ya mbegu yaliyopo nchini na hivyo katika siku zijazo nchi itaingiza fedha kwa kuuza mbegu.

"TFS tumewapokea wageni kutoka Ethiopia wamekuja kujifunza kuhusu utunzaji wa misitu.Eneo ambalo limewavutia ni mashamba ya madogo ya mbegu tuliyonayo kwani yameandaliwa katika kiwango cha kimataifa. Tunaamini kwa miaka mitatu au minne ijayo mbegu zitatoka kwetu hapa hapa na kuuza kwa wengine.

"Lakini lengo si kuuza tu mbegu bali kuboresha mashamba ya miti kwa kuwa na mbegu bora na kwa kutumia mbegu bora kiasi cha uzalishaji kitaongozeka na hivyo kuongeza pato la taifa.Kwa sasa ni vigumu kupanua ukubwa wa mashamba bali ni kuongeza uzalishaji.Lengo letu ni kuongeza pato la nchi kwa kuongeza uzalishaji wa miti.Hatua ambazo tunazichukua katika kuzalisha mbegu bora umewafanya raia hao wa Ethiopia kutoa pongezi kwa wataalam wetu.Tunaamini tutashirikiana nao,"amesema Dk.Katety.

Kuhusu wapi zinapatikana mbegu bora, amesema ni vema kwa wanaohitaji mbegu wakaenda katika ofisi za TFS ambazo zipo katika ngazi ya wilaya na mikoa ambako watapata maelekezo ya wapi wanaweza kupata mbegu bora.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...