Na Ramadhani Ali Maelezo Zanzibar
Wakala wa Chukula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeteketeza samaki tani 106
aina ya peduu walioingizwza nchini kutoka China na maziwa tani 23
kutoka Dubai baada ya bidhaa hizo kuharibika na kukosa sifa kwa ajili
ya matumizi ya binadamu.
Samaki hao waliokuwa kwenye makontena manne ya futi 40 waliingizwa na
Kampuni ya Drive Shark na kontena moja la maziwa kutoka Dubai
yaliletwa na mfanyabiashara Yunus Hashim.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuangamiza bidhaa hizo
katika kijijii cha Kibele, Afisa Uhusiano wa ZFDA Abdulmatin Yassin
alisema samaki waliharibika baada ya kukosa umeme wa uhakika kwenye
makontena.
Alisema kukosekana kwa umeme wa kutosha kwenye makontena yalipofika
bandarini Zanzibar kulisababisha kupungua barafu iliyogandisha samaki
na kuanza kuharibika.
Abdulmatin alisema samaki wanapoingizwa nchini huwa wameganda na
hutakiwa waendelee kubakia katika barafu wakati wote lakini wakati
makontena yakisubiri taratibu za uingizaji palitokea kasoro na
kusababisha samaki kuharibika.
Alisema kwa upande wa bidhaa ya maziwa, yaliharibika baada ya baadhi
ya maboksi kupasuka wakati yakisafirishwa kutoka Dubai kuja Zanzibar.
Mkuu wa Kitengo cha uchunguzi wa athari zitokanazo na chakula wa
Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar Aisha Suleiman alisema samaki aina
ya peduu wanaoingia nchini kutoka nje ni salama kwa matumizi ya
binadamu lakini umakini unahitaji wakati wa kuwasafirisha na
wanapofika bandarini .
Aliwataka wananchi wanaponunua samaki wanaoingizwa nchini kuwa
waangalifu na wahakikishe wameganda kwenye barafu na wasiwaweka muda
mrefu kabla ya kuwapika ama waendelee kuwaweka katika barafu.
Aidha aliwashauri wafanyabiashara kufuata taratibu zote za kuingiza
bidhaa nchini na kutafuta bidhaa zenye ubora uliowekwa na Bodi ya
Chakula na Dawa Zanzibar ili kujiepusha na gharama zisizokuwa za
lazima.
Alikumbusha kuwa Sheria ya ZFDA kwa bidhaa zilizoharibika ama kupitwa
na muda wa matumizi, mfanyabiashara hushauriwa kuirudisha ilikotoka
ama kuangamizwa kwa gharama zake.
Mkuu huyo wa Kitengo cha uchunguzi wa athari zitokanazo na chakula wa
ZFDA amewahakikishia wafanyabiashara kwamba Bodi hiyo haina ni ya
kuwadidimiza kutokana kazi nzuri wanayofanya, lakini lengo ni kulinda
afya za wananchi kwa kuhakikisha wanapata bidhaa zilizo salama.
Mmoja wa Afisa kutoka Kampuni ya Drive Shark, alieficha jina lake,
aliishauri Serikali kwa kushirikiana na mfanyabiashara husika
kuangalia matumizi mbadala wa bidhaa za aina hiyo, kwa sababu hazina
sumu, badala ya kupoteza fedha nyingi kuziangamiza.
Gari zilizobeba makontena yenye tani 126 za Samaki na Maziwa yakiwa yameegeshwa katika jaa la Kibele Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya maboksi ya Samaki walioharibika yakiwa kwenye Kontena yakisubiri kushushwa kwa ajili ya kuharibiwa katika eneo la Kibele Wilaya ya Kati Unguja.
Gari aina ya Gurdoza la Manispaa ya Mjini likisaga Samaki na Maziwa yaliyoharibika katika eneo la la Kibele Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja.
Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Athari za Chakula wa
ZFDA Aisha Suleiman akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kuangamizwa tani 126 za Samaki na Maziwa kutokana na kutokufaa kwa
matumizi ya binadamu.
Picha na Makame Mshenga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...