Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dr. Augustine Mahiga amewataka Viongozi wa Tanzania hasa Viongozi Vijana kuiga mfano wa UZALENDO na UTUMISHI ULIOTUKUKA wa Hayati Edward Moringe Sokoine ambaye aliitumikia nchi hii kwa nafasi mbalimbali za Uongozi mpaka katika Ngazi ya Uwaziri Mkuu.

Hayo yamesemwa Wilayani Monduli,Arusha Tarehe 12.04.2019 wakati wa Ibada ya maadhimisho ya miaka 35 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine,Ibada iliyoongozwa na Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.

“Sokoine aliipenda nchi yake,aliweka uzalendo mbele.Alikuwa ni mchapakazi asiyechoka,kuna siku aliniita nyumbani kwake saa 8 usiku kujadili masuala nyeti ya Taifa akanionea huruma akasema nikapumzike ila nirudi saa 11 Alfajiri, na nilivyorudi nilimkuta yeye bado yupo macho mezani pale pale ananisubiri.Viongozi tuna la kujifunza kwa aina hii ya maisha ya utumishi na kujitoa”Alisema Balozi Mahiga

Akishukuru kwa niaba ya Familia,Mtoto wa Kiume wa Hayati Sokoine Balozi Joseph Sokoine amewashukuru watu wote waliojumuika nao katika siku hiyo muhimu na kuwataka Watanzania wayaenzi mambo mema yaliyofanywa na Baba yake na kwa kuwa Hayati Sokoine aliwapenda sana watanzania katika kumuenzi katika hilo Sokoine Memorial Foundation ilikabidhi madawa yenye Thamani ya Tsh 2.5m kwa kituo cha Afya Monduli na kadi 100 za Bima ya Afya kwa kaya maskini.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne Mh Mizengo Kayanza Peter Pinda,Naibu Waziri wa Kilimo Mh William Ole Nasha,Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Mh Anthony Mavunde,Mwenyekiti wa CCM Mkoa Arusha na Viongozi mbalimbali wa Siasa na Dini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...