Na Moshy Kiyungi
Hugh Masekela ni majina ya mwanamuziki mashuhuri wa Afrika Kusini, aliyefariki dunia Januari 24, 2018 jijini Johannesburg, nchini Afrika ya Kusini akiwa na umri wa miaka 78. Chanzo cha kifo chake ni ugonjwa wa tezi dume ulimpata kwa miaka kadhaa ilyopita. Bendi yake ilitoa taarifa ikisema kwamba marehemu Masekela amekuwa akipambana na ugonjwa huo tangia mwaka 2008.

Mwezi Machi 2016 alifanyiwa upasuaji wa jicho baada ya saratani kusambaa, ikabidi akafanyiwa upasuaji mwingine mwezi Septemba mwaka huo huo. Hugh Masekela alisifika kwa nyimbo zake zilizotoa mchango mkubwa katika harakati za kupinga ubaguzi wa rangi. Wasifu wa Masekela, unaonesha kuwa alizaliwa Aprili 04, 1939 katika mji wa KwaGuga huko Witbank, nchini Afrika ya Kusini.

Alikuwa mpulizaji mashuhuri wa tarumbeta wa muziki ya Jazz. Hugh alianza kuimba na kucheza Piano tangia akiwa mtoto, baada ya kuona filamu ya ‘Young Man with a Horn’. Masekela alifahamika ulimwenguni kote kwa aina ya kupiga muziki wa Jazz la mtindo wa Afri Jazz. Alikuwa na talanta ya upulizaji wa tarumbeta, uongozi wa bendi ya muziki, utunzi na mwandishi mahiri wa mashairi ya muziki.

Masekela alijifunza kupuliza tarumbeta akiwa shuleni, kupitia kwa mwalimu wake ni Padri Trevor Huddleston ambaye alikuwa ni mkuu wa shule yao ya Huddleston. Hakuchukua muda Hugh Masekela kuweza kuitawala ala hiyo ya tarumbeta. Mwaka 1956 akajiunga na kundi la Jazz la Herbert’s African Jazz Revue.

Akiwa na umri wa miaka 20, Masekela alikuwa akitumbuiza muziki ya aina tofauti, hasa ya Jazz, Bebop, Funk na Afro beat wakati huo alikuwa na kundi la Jazz Epistles. Kundi hilo lilikuwa na wasanii maarufu kama mpiga kinanda mahiri Abdillah Ibrahim.

Mwaka 1960 Masekela alikwenda London, Uingereza ambako alijiunga na shule ya muziki ya Guildhall School of Music na baadae alikwenda New York, Marekani ambako alisoma katika mji wa Manhattan. Mwaka 1962 alitoa albamu yake ya kwanza iitwayo Trumpet Africa. Miaka miwili baadaye Hugh alitoa nyingine iitwayo The Americanization of Ooga Booga, ambayo ilitamba mpaka kushika chati, hasa baada ya kuchezwa sana na kituo kimoja cha radio cha mjini California.

Mpaka kufikia Agosti 2000, Masekela alikuwa ameuza nakala milioni 50 na kumfanya apate tuzo ya Platinum. Hugh alishirikiana na wasanii kama Miriam Makeba wa Afrika Kusini na Paul Simon wa Marekani kwenye albamu ya Graceland. Tarumbeta lake limesikika zaidi kwenye nyimbo za Gumboots na Diamonds on the soles of her shoes.

Enzi za uhai wake Masekekla aliwahi kusema kwamba alitumia muziki kama silaha ya kusambaza mageuzi ya kisiasa enzi hizo za ubaguzi wa rangi, na alifanikiwa sana. Ilielezwa kwamba Masekela alikuwa ni baba wa muziki wa Jazz nchini Afrika Kusini. Mchango wake mkubwa kimziki ulimebakia ndani kumbukumbu kwenye mamilioni mioyo ya watu.

Aidha kwa upande wake rais wa Afrika Kusini wakati huo, Jacob Zuma alimsifia Masekela kama msanii wa muziki wa  Jazz, mpiga tarumbeta maarufu, mwanaharakati wa utamaduni na mtu aliyekuwa katika harakati za ukombozi.

"Aliuweka hai mwanga wa uhuru duniani kote katika harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi kupitia muziki wake na kushinikiza uungwaji mkono wa Kimataifa, fani ya muziki na nchi kwa Ujumla tumempoteza mtu muhimu sana…" alisema rais Jacob Zuma.

Mwimbaji mmoja wa Afrika Kusini Johnny Clegg alimuelezea Hugh Masekela kama mwanamuziki bora na siku zote akiishi kwa mitazamo ya asili yake ya Afrika Kusini. Nguli huyo aliondoka nchini Afrika Kusini wakati ilipoongozwa na watu weupe mwaka wa 1960, hakurejea hadi pale Nelson Mandela alipoachiwa huru mwaka wa 1990.

Muda wote alikuwa uhamishoni mjini London nchini Uingereza. Baadaye alihamia mjini New York Marekani, ambako alikutana na msanii mwenzake wa Afrika Kusini Miriam Makeba, Dizzy Gillespie na Harry Belafonte. Hugh Masekela na Makeba waliishi maisha ya ndoa ya muda mfupi na Miriam Makeba.

Miongoni mwa nyimbo zake zilizovuma na zilizopendwa ni ule wa "Bring Him Back Home", akishinikiza Nelson Mandela achiwe huru. Hugh Masekela alitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini ikiwa ni mara ya kwanza fainali hizo kufanyika barani Afrika.

Kwa upande wake Waziri wa Sanaa nchini Afrika Kusini Nathi Mthethwa alisema kwamba taifa hilo limempoteza mwanamuziki wa haiba ya kipekee aliburudisha nyoyo za watu wa taifa hilo kupitia miziki yake. Wakati wa enzi wa nguli huyo alikuwa mwanaharakati akipigania haki na kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Moja ya kazi zake ni “Soweto Blues" muziki ambao ulitumiwa  na makundi ya kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Zingine ni pamoja na Tagi, Mandela , Apartheid, Afrika Kusini, Hugh Masekela. Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...