Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 

ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) Ludovick Utouh amewashauri wanachama wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania(TAWCA) kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu hasa kwa kutambua wanawake wakiamua naweza. 

Pia amewahamasisha wanawake wenye taaluma mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi kwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwakani ili kupata nafasi ya kuingia kwenye vyombo vya maamuzi pamoja na kutunga sera kwa maslahi ya wananchi wote. 

Utouh amesema hayo leo Aprili 12, 2019 wakati anafungua mkutano wa pili wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu nchini ambao utafanyika kwa siku mbili ambapo wakati anazungumza kwenye mkutano huo amesema anaamini wanawake wanaweza na hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuungana kuleta maendeleo. 

Amesema anatambua nguvu ya wanawake huku akitoa mfano kuwa hata kupinduliwa kwa Rais wa Sudan kumetokana na nguvu ya wanawake baada ya kuamua kupaza sauti zao kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula katika masoko ya nchi hiyo. 

"Nina uhakika wanawake mnaweza, na kwa kuwa leo mnajadili kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi kuna sifa za msingi ambao kiongozi mzuri anatakiwa kuwa nazo.Baadhi ya sifa hizo ni kwamba kiongozi mzuri ni yule anayekuwa na maono kwa ajili ya wale anaowangoza, uthubutu katika kufanya maamuzi na kuweka ajenda zenye tija kwa jamii unayoiongoza. 

"Hivyo mwaka huu na mwakani ni mwaka uchaguzi, nitoe rai kwenu hakikisheni mnajitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi .Utakapokuwa kwenye vyombo vya maamuzi kwa kutumia taaluma zenu mtakuwa na nafasi nzuri ya kushauri na kutoa muelekeo katika kuleta maendeleo kwa ajili ya nchi yetu,"amesema Utouh. 

Amefafanua tena kwa wanawake hao wanakila sababu ya kupambana kwa nguvu zao badala ya kusubiri nafasi za kupewa kwani kusubiri kupewa kunakwenda sambamba na kujipendekeza na kwake hayuko tayari kuona wanawake wanajipenda kwani wanaweza kufanya mambo makubwa bila kusukumwa na mtu mwingine. 

Kuhusu nafasi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi, amesem utafiti uliofanyika duniani unaonesha wanawake ndio wanaoongoza kwa kuwa waamini katika kulinda raslimali za nchi ukilingana na wanaume, hivyo ameshauri kwa Serikali kutosita kuwapa nafasi wanawake katika nafasi za uongozi. 

Amesema kufika kwake kwenye mkutano huo imetokana na heshima ambayo amepewa na TAWCA hasa kwa kutambua wazo la kuanzishwa kwake limetokana na yeye akiwa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu(NBAA) ambapo alishauri kuanza kwa taasisi hiyo. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania(TAWCA) Neema Kiure-Mssusa amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwainua wanawake nchini na hasa wanachama wa TAWCA.Pia kuangalia changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wake. 

"Katika mkutano huu tupo zaidi ya wahasibu wanawake 300, hivyo tutajadili kwa kina kuhusu changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua maana tunaamini kwa umoja wetu tunaweza. Tutajadili kwa kina namna gani tunaweza kupiga hatua kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.Ujumbe wangu kwa wanawake nchini tuthubutu kwani tunaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo,"amesema Kihure. 

Akizungumzia nafasi ya Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo Renata Ndege ambaye ni Meneja Mkuu Fedha TANESCO amesema wanatambua umuhimu wa mkutano huo na hivyo wakaona ni vema wakawa sahemu ya kuufanikisha. 

"Tumeona ipo sababu ya TANESCO kushiriki kikamilifu kwa kudhamini mkutano huu wa Wahasibu Wanawake.Kupitia mkutano huu wa siku mbili wahasibu hao watapata nafasi ya kubadilishana mawazo na kutatua changamoto zilizopo na kwetu TANESCO kuna wahasibu wengi wanawake, hivyo kwetu mkutano huu ni muhimu kwani unakwenda kuwajenga wahasibu wanawake na kutoka na ari mpya ya kulitumikia Taifa,"amesema Ndege. 

Kuhusu nafasi ya mwanamke, amesema kikubwa ni kujiamini na kuthubutu kwani kwake anamini hakuna unyanyasaji wowote iwapo mwanamke atasimama imara na kujiamini kwa kile ambacho anakifanya. 

"Katika mkutano wanawake wahasibu waliohudhiria leo hii ni 300 na wote huko ambako wanatoka ni viongozi.Hivyo ni kujiamini tu badala ya kusema huwezi.Nipo TANESCO nafanya kazi vizuri, sioni kunyanyaswa na mtu , kikubwa ni kuhakikisha unakuwa na sifa zinazohitajika kufanya kazi katika eneo ambalo umepewa kulitumikia.Wanawake tujiendeleze katika elimu na bahati nzuri kwa sasa wanawake wanajitahidi kusoma,"amesema Ndege. 

 Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) Ludovick Utouh (kulia) akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania(TAWCA) Neema Kiure-Mssusa baada ya kufungua mkutano wa pili wa TAWCA ulioanza leo jijini Dar es Salaam.Utouh alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo
 Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) Ludovick Utouh (kulia) akioesha tunzo aliyopewa na w Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania(TAWCA) Neema Kiure-Mssusa kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuanzishwa kwa taasisi hiyo na kufungua mkutano wao wa pili uliofanyika leo Aprili 12,2019 jijini Dar es Salaam
 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) mstaafu Ludovick Utouh akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu nchini uliofanyika leo jijini Dar es Salaam
Meneja Mkuu Fedha -TANESCO ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo Renata Ndege akizungumzia sababu za Shirika la Umeme Tanzania kuamua kudhamini mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahasibu Wanawake Tanzania wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili ulioanza leo
Sehemu ya wanawachama wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu Ludovick Utouh wakati anafungua mkutan o wa taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...