Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam

Tatizo la madawa ya kulevya ni janga kubwa duniani kote, ambapo idadi kubwa ya watu wameathirika.

Janga hili halichagui tajiri, masikini, jinsia, rika, vijana kwa wazee pia wamo.Madawa ya kulevya hutumiwa kwa njia ya kunywa, kunusa, kula au hata kujidunga.

Matokeo yake hubadili akili au fikra za mtumiaji kuwa tofauti na akili zake za kawaida.Yasemekana kuwa wapo watu wengi wanaotumia madawa hayo wakiwemo baadhi ya Wasanii, Wanamuziki na baadhi ya vijana, waliojiingiza katika matumizi hayo ya madawa ya kulevya.

Katika makala haya yanamzungumzia aliyekuwa mnenguaji mahiri humu nchini, aliyejiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, yakapelekea kupoteza maisha yake. Msanii huyo ni Aisha Mohammed Mbegu ‘Aisha Mandinda’, aliyekuwa mnenguaji maarufu humu nchini.

Mara baada ya kujiingiza katika matumzi ya madawa ya hayo, tabia na maisha yake kwa ujumla yalikuja kubadilika kabisa.

Aisha Madinda alifikia hatua ya kucheza picha ya utupu ikarushwa kwenye mitandao ya kijamii, akionesha sehemu zake zote nyeti, akisindikizwa sauti ya kibwagizo cha ‘Alamba Alamba’ kilichochoachiwa na aliyekuwa Mfalme wa taarabu nchini, Mzee Yussuf.

Msemo wa Kiswahili usemao “Majuto mjukuu” ulijionesha dhahiri kwa mwanamama huyo baada ya kujikuta amepoteza mwelekeo wa maisha.

Aliwahi kutamka kuwa anajuta kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, kwamba yamechangia kuharibu maisha yake aliyoyatengeneza akiwa na nguvu zake.Aisha alisema kwa uchungu kwamba alighiribika na kujikuta akiuza nyumba zake tatu kwa bei ya kama katoa bure, ili kupata fedha za kununua madawa hayo.

Majina yake kamili alikuwa alikuwa akiitwa Aisha Mohammed Mbegu, aliyezaliwa katika Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam mwaka 1980.Kutokana na wazazi wake kuhamishiwa Mkoani Mbeya kikazi, Aisha alilazimika kuanza masomo yake katika shule ya Msingi Kiganamo iliyopo wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, hadi alipohitimu darasa la saba mwaka 1992.

Mwaka 1993 alihamishia makazi yake mjini Kigoma akajiunga na shule ya Sekondari ya Katubuka.Kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuhitimu masomo yake ya sekondari, baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia karo hivyo aliishia kidato cha pili tu.

Baada ya kukatisha masomo yake, mwaka 1994, alihamia jijini Dar es Salaam na kuanza kazi ya usafi katika Kampuni iliyojulikana kama Dar Cleaner, ambako alifanya kazi ya usafi katika majengo mbalimbali.

Aisha alijiingiza rasmi kwenye unenguaji mwaka 1996, baada ya Prodyuza wa muziki aliyefahamika kwa jina moja la Maloni, kumtonya kuwa Club Billicanas ilikuwa ikihitaji wanenguaji.

Club ya Billicanas ilianzisha kundi la wanenguaji la Bill Bambums, yeye akawa miongoni mwao.Kundi hilo lilikuwa likiundwa na yeye pamoja na Mussa Hassan ‘Super Nyamwela’, ambao kwa pamoja walikuwa wakitoa burudani maridadi katika ukumbi huo wa Club Bilicanas.

Katika enzi za uhai wake alikiri kwamba alichagua kazi ya unenguaji, akafanikiwa na kudumu ndani ya kazi hiyo kwa takriban miaka kumi na sita.Mwaka 1999, mkali huyo wa nyonga ambaye tayari alishakuwa tishio kokote apandapo jukwaani, alipata ‘mchongo’ wa kwenda kupiga ‘kazi’ Uarabuni katika mji wa Muscat.

Aliambatana na mnenguaji mwenzake aliyekuwa swahiba wake Halima White ambaye naye ni marehemu pia. Walipiga kazi kwa takriban mwaka mmoja na mwaka 2000 walirejea nchini.Aisha mara baada ya kurejea, alichukuliwa na bendi ya Borabora Sound, ambako aliitumikia kwa miezi sita kabla hajaachana nayo.

Aliondoka tena kwenda Bahrain, Uarabuni ambako alipiga kazi katika kumbi mbalimbali nchini humo kwa miezi mitatu.Aisha aliporejea Dar es Salaam kwa mara nyingine, alijiunga na bendi ya The Kilimanjaro Connection ambapo pia hakukaa sana.

Mwaka huohuo wa 2000 mwishoni, akaachana na bendi hiyo, akaamua kufanya biashara zake ndogondogo.Mwaka 2001, Aisha Madinda ndipo aliamua kujiunga rasmi na bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Aisha baada ya kujiunga na bendi hiyo, akawa kivutio kikubwa kwa wapenzi na mashabiki wa bendi hiyo kufuatia urembo wake, shepu nzuri na tabasamu usoni mwake wakati wote.Wapenzi wa bendi hiyo ya Twanga walikuwa wakipaza sauti wakimhitaji pindi Aisha Mdinda ikitokezea siku amekosekana katika onesho la bendi hiyo, kwa kuwa pengo lake lilionekana mapema.

Mnenguaji huyo kwa tabia hakuwa na makuu wala majivuno yeyote, licha ya kujaaliwa kuwa na maisha mazuri.Alifanikiwa kujenga nyumba tatu, alimiliki usafiri wake pia watoto wake aliwapa chakula na malazi bora, pia aliweza kuwapeleka shule nzuri.Aisha Madinda alipiga kazi ya unenguaji hadi mwaka 2011, mwishoni, akaenda kujiunga katika bendi ya Extra Bongo iliyokuwa ikiongozwa na Ally Choki.

Wakati huo tayari alikuwa ameshakuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya.
Ilifikia hatua ya kushindwa kunengua jukwaani, shoga zake walikuwa wakimfariji kwa amaneno matamu kuwa asikate tamaa bado ana nguvu bora alilie uzima wake.

Mkurugenzi wa kampuni African Stars Entertainment Tanzania, Asha Baraka na yeye alionesha dhamira ya kumsaidia Aisha, ili aweze kurudi katika hali yake ya zamani.Hivyo akawa anakwenda kuchukua fedha mara kwa mara kwa ajili ya manunuzi ya mahitaji yake kama mwanamke wa mjini.

Baadae afya yake ilianza kuimarika akaweza kuhudhuria onesho la usiku wa Mwafrika katika ukumbi wa Club Bilicanas.Hakika usiku huo baadhi ya watu walimsahau kwani alikuwa amependeza na amerudi katika hali yake ya zamani.Wakamsisitiza aendelee na tiba ya dawa za Methodine ambazo alikua anatumia.

Wadau wa Twanga Pepeta walipania kumrudisha katika hali yake ya kawaida, wakitamka kuwa kupotea kwa kipaji cha Aisha kuliwauma mno.
Wakajitolea kwa hali na mali ili kuyanusuru maisha yake.Aisha Madinda alikuwa ni mama wa watoto wawili na mjukuu mmoja.

Wakati akihangaika ujinasua na janga hilo ili alikuwa akipita huku na kule ili aweze kupata tiba ya ugonjwa unaomsumbua.Hivyo Aisha aliwahi kuokoka na alithibitisha hilo. Yaelezwa kuwa alifanya hivyo kwa kuamini kwamba matatizo yake yangemalizika kwa kuombewa.

Aisha Mohamed Mbegu maarufu kama ‘Aisha Madinda’ alikutwa na rafiki yake Samira Saleh akiwa amelala usingizi mzito kibarazani nyumbani kwake Mabibo (Nyumbani kwa Samira).Samira alibainisha kwamba Aisha Madinda hakuwa kwake, lakini alimkuta barazani kwake asubuhi ya akiwa hajitambui.

Alisema kuwa alijitahidi kumtingisha lakini Aisha alikuwa kimya na hivyo akaamua kuchukua Bajaji na kumkimbiza hospitali ya Mwananyala, jijini Dar es Salaam.Walipofika katika hospitali ya Mwananyamala majira ya saa 2 asubuhi, Daktari aliyempokea akamwambia tayari mgonjwa wake alishafariki dunia Desemba 17, 2014.

Kamanda wa kanda ya Polisi mkoa wa Kinondoni wakati huo Camillus Wambura, alithibitisha kutokea kwa kifo chake.

Samira alieleza ukweli kwamba yeye kama alivyo Aisha Madinda, ni muathirika wa madawa ya kulevya ambapo anaitaja hospitali ya Mwananyamala ndio Kliniki yao ya kupata tiba saidizi (MAT) ya madawa ya kulevya na ndio sababu hakumpelekea hospitali nyingine yoyote zaidi ya Mwananyamala.

Marafiki wa Aisha Madinda ambao nao ni waathirika wa madawa ya kulevya, walisema Aisha Madinda alikwa amerudia utumiaji wa madawa hayo, wanamashaka kuwa alitumia kiasi kikubwa kuliko inavyohitajika na pengine ndio sababu ya kifo chake.

Maziko ya Aisha Madinda yalicheleweshwa kutokana na zuio la Jeshi la Polisi, kupisha uchunguzi wa sababu za kifo cha ghafla cha mnenguaji huyo.

Hatimae mwili wa Aisha Madinda ukashushwa kwenye nyumba yake ya milele Desemba 19, 2014, kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mikwambe, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Hadi mauti yanamkuta alikuwa katika dozi ya kujinasua na matumizi ya mihadarati na alikuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Baada kifo hicho Asha Baraka alimwelezea Aisha Madinda kuwa alikuwa ndio kwanza amerejea kutoka Dubai alikokuwa amekwenda kwa shughuli za kimuziki na kwamba alikuwa hajajiunga na bendi yoyote hadi mauti yanamkuta.

Kwa upande wake Katibu wa bendi ya Twanga Pepeta, Luiza Mbutu alisema kuwa Aisha alitazamiwa kuanza mazoezi na bendi ya Twanga Pepeta kwa ajili ya maandalizi ya miaka 16 Luiza Mbutu ndani ya Twanga Pepeta.

Hii ni picha kamili ya ubaya wa kutumia madawa ya kulezya.

Makala hii inakuasa wewe achana na fikra potofu za kutaka kutumia madawa ya kulevya.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...