Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akiwahutubia wafugaji wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro wakati wa uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akikata utepe kuashiria uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima katika kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akivalishwa shuka la kimasai na mzee wa mila wa kabila la kimasai Ezekiel Lesenga kama ishara ya kumsimika katika uongozi wa sekta ya ambapo alipewa jina la Ole Mpina wakati wa uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima katika kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro.


Na John Mapepele

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema Wizara imeanza program maalum ya kitaifa ya kuwafundisha wafugaji na wavuvi kote nchini kuhusu sheria za mifugo na uvuvi na sheria nyingine hatua itakayowezesha kujua haki zao na kujiepusha na migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi kwa upande wafugaji ambapo kwa upande wa uvuvi Wizara itawafundisha ufugaji bora wa samaki,utekelezaji wa sheria na kanuni za uvuvi,udhibiti wa ubora wa mazao ya uvuvi na ushirika wa wavuvi ili kuboresha maisha yao.

Akizindua mafunzo hayo kitaifa katika Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina alisema mafunzo kwa wafugaji yatawezesha wafugaji kutambua namna ya kutumia fedha zitokanazo na mifugo na mazao yake kwa kuwekeza maeneo mengine kujenga makazi bora, kusomesha watoto, kukata bima ya mifugo na kujiwekea akiba benki.

“Leo tunaanza kuzindua mafunzo kwa wafugaji lengo likiwa ni kuwawezesha kuzijua sheria za mifugo na kutambua haki zao ili kujiepusha na migogoro baina yao na majirani zao wakiwemo wakulima, wahifadhi pamoja na kuelimishwa mbinu za kisasa za namna ya kuboresha maisha na ufugaji.” Alisisitiza Mpina

Alisema kwa pande ufugaji sheria zitakazofundishwa kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya Nyanda za Malisho na Raslimali za Chakula cha mifugo Namba 13 ya mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Wanyama pori Namba 5 ya Mwaka 2009.

Pia wafugaji hao watafundishwa namna ya kudhibiti magonjwa ya kimkakati 12 ambayo yanadhibitiwa kwa njia ya chanjo ikiwemo Sotoka ya mbuzi(PPR), Homa ya mapafu ya ng’ombe(CBPP), Ugonjwa wa miguu na Midomo(FMD), Homa ya mapafu ya Mbuzi(CCPP),Mdondo(ND)Homa ya Bonde laUfa(RVF).

Magonjwa mengine ni Mapele ya Ngozi (LSD) Homa kali ya Nguruwe(ASF) Ndigana Kali (ECF) Kimeta(Anthrax), Kichaa cha Mbwa (Rabbies) na ugonjwa wa wa kutupa mimba(brucullosis) na kuokoa vifo vingi vya mifugo vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Pia wafugaji watafundishwa matumizi sahihi ya dawa,chanjo na viuatilifu vya mifugo nchini,uzalishaji wa mbegu bora za malisho, utunzaji wa nyanda za malisho na machunga , ufugaji kibiashara na kuweka utaratibu wa kuvuna mifugo na kuanzisha ushirika wa wafugaji.

Hivyo Waziri Mpina aliwahimiza wafugaji kote nchini kuchangamkia mafunzo hayo kwani ndio yatakayokuwa mkombozi baada ya kuishi kwa zaidi ya mika 50 hivyo Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati kuwakomboa kutoka kwenye dhiki na dhuluma waliofanyiwa.

Pia Waziri Mpina alimwagiza Katibu Mkuu wa Mifugo kuhakikisha anakarabati bwawa la Narakauo katika Kijiji cha Loibosoit kwenye Wilaya ya Simanjiro katika kipindi cha miezi miwili toka sasa ili kutatua tatizo sugu la maji kwa ajili ya kunywesha mifugo na binadamu.

Aidha alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefled Myenzi kufanya marekebisho kwa majosho yote yaliyoharibika kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji nchini George Bajuta aliishukuru Wizara ya Mifugo kwa uamuzi wake wa kuanzisha mafunzo hayo kwa mara ya kwanza ambayo hayajawahi kutolewa kwa wafugaji nchini na kwamba yatawasaidia kubadilisha maisha ya wafugaji ambao walikuwa wakidharaulika na kufukuzwa kila mahali walipokuwa wanakwenda kwa ajili ya shughuli za ufugaji.

Pia alimwomba Waziri Mpina kuandaa mwongozo utakaosaidia kuondoa tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kukamata hovyo mifugo kuitesa kwa muda kwa muda mrefu huku mingine ikipotea kwa kutaifishwa.

Mafunzo ya sekta za Mifugo na Uvuvi yataendeshwa katika Wilaya zote 185 nchini na yatawafuata wafugaji na wavuvi kwenye maeneo yao na kwa kuanza kwa upande wa mifugo yatatolewa kwenye wilaya mbili za awali za Simanjiro na Kaliua mkoani Tabora, ambapo kwa upande wa Sekta ya Uvuvi mafunzo ya awali yatatolewa kwenye katika wilaya za Mafia, Bagamoyo,Mkuranga,Kigambni na Kinondoni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...