Na Moshy Kiyungi

Muziki wa Kongo hivi sasa ‘umekamatwa’ na wanamuziki wa kizazi kipya, akiwemo Fally Ipupa. Sifa za mwanamuziki huyu zimeenea kila pembe Afrika, Ulaya hadi Marekani kuliko na wapenzi wa muziki wa dansi. Ipupa pamoja na mwenzake Ferre Golla, wanatajwa kuelekea kuchukua nafasi za wanamuziki wakubwa waliowatangulia. 

 Vijana hao hivi sasa waatamba katika anga ya muziki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakipishana kwa mwaka mmoja kwa kuzaliwa. Ferre Gola alizaliwa Machi 03, 1976 wakati Fally Ipupa alizaliwa Desemba 14, 1977 wote katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Majina yake kamili anaitwa Fally Ipupa Nsimba, alizaliwa na ndugu zake watatu akikwemo kaka yake ajulikanae kwa majina ya Bony Listton pamoja na dada zake wawili Tyna na Niclette. Baba yake mzazi anaitwa Faustin Ebamba na mama yake anajulikana kwa majina ya Monique Bolutuli Mbo.

Fally alianza kuvutiwa zaidi katika muziki kati miaka ya 1992 na 1993. Akishirikiana na wenzake akina Sankara Dekunta, Atele Kunianga, Pitshou Luzolo kwa pamoja wakaunda kundi lao la muziki walilolipa majina ya Flash success. Kundi hilo lilikuwa limejikita katika mitaa yao iliyopo kwenye Manispaa ya Bandalungwa aka Bandal, jijini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kundi hilo likaungana na la Fraternité Musica. Wazazi wa Fally Ipupa hawakupenda awe mwanamuziki, walikuwa wakimhimiza na kushinikiza kuendelea na shule. Wao walitaka kijana wao asomee fani ya Udaktari badala ya muziki. Kati ya mwaka 1995 na 1996, Fally Ipupa alikwenda kujiunga na kundi la Kibinda Nkoy, kwenye Manispaa ya Kintambo. Alipoingia kundini humo, aliwakuta wanamuziki wengine kama Seguin Mignon.

Wakati anaendelea kupiga muziki katika bendi hiyo, ukatokea mgawanyiko kwenye katika kundi hilo. Yeye Fally Ipupa, Seguin Mignon na wengine wakajiengua na kwenda kuunda kundi jingine walilolipa majina ya Nouvelle Alliance. Katika kundi hilo ndiko Fally Ipupa umaarufu wake wa kuimba na unenguaji uliimarika zaidi.

Mwaka 1997, Fally alijiunga na bendi ya Talents Latent’s, akawa kama Kiongozi wa bendi. Kwenye bendi hiyo pia walikuwepo marafiki zake akina Atele Kunianga, Pitsho Uluzolo bila kuwasahau ma rapa akina Gentamicine Lissimo, na Cellulaire Yankobo.

Mwaka 1999, Fally Ipupa akajiunga katika bendi ya Quartier Latin, inayomilikiwa na Koffi Olomide Le Grand Mopao Mokonzi. Akiwa na bendi hiyo Ipupa akatokea kupendwa sana na kiongozi huyo, kwa kipindi kifupi akatafutiwa hati yake ya kusafiria. (Passport). Baada ya kupata hati hiyo aliungana na wanamuziki wenzake kwenda hadi jijini Paris, nchini Ufaransa kufanya onesho la Bercy.

Kwenye album ya Attentat ingawa Fally Ipupa alikuwa bado mpya kwenye bendi, alichangia kwa kiasi kikubwa sana. Koffi Olomide aliweka matumaini makubwa sana kwa Fally Ipupa, hata pale album ya Force De Frappe ilipotolewa, alipewa fursa ya kuimba na Mopao kwenye wimbo wake wa Éternellement.

Wakati anatunga wimbo huo, Fally alikuwa na umri mdogo wa miaka 15. Albuma ya Effrakata wakati inatolewa mwaka 2001, Koffi Olomide akampendelea zaidi Fally Ipupa ukilinganisha na wenzake. Ipipa licha ya kuweka sauti yake kwenye nyimbo takriban zote, pia aliweka rap kwenye wimbo wa Generation Bercy. Fally Ipupa aliimba kwa Pamoja na Koffi Olomide kwenye wimbo wa Effervescent.

Kama hiyo haitoshi, Koffi Olomide akampa cheo cha kuwa kiongozi wa bendi badala ya Felly Tyson ambaye ndiye ilitakiwa apewe wadhifa huo. Mwaka 2003, ikatolewa album Affaire D’etat, Fally Ipupa akawa mwanamuziki pekee ambae wimbo wake wa Ko Ko Ko Ko, uliwekwa kwenye CD zote mbili za album. Album ya Monde Arabe iliyotolewa mwaka 2004, Fally Ipupa akapewa kipaumbele tena.

Sauti yake yasikika kwenye nyimbo zote zilizopendwa, nyimbo za Esili na Eputsha, ni mfano tosha. Ipupa aliimba kwa weledi mkubwa wimbo wa Pharmacie, ambapo sifa zake ziliendelea kusambaa.

Nguli huyu ana talanta nyingi zikiwemo za kutunga na kuimba nyimbo, unenguaji, pia anao uwezo mkubwa wa kurap. Baada ya kujiona kuwa ameiva katika muziki majina yake si ya kutambulishwa tena, wazo la kutaka kujitegemea likajengeka kichwani mwake. Fikra zake za mwanzoni zilikuwa apewe fursa ya kufanya muziki kivyake vyake ‘Solo artist’, ndipo akaanza kununua nyimbo toka kwa watunzi mbalimbali.

Ipupa akijiweka mwenyewe katika kazi ya kutunga akisaidiwa na marafiki zake. Akawa anasubiria wakati muafaka ambao atatangaza hadharani nia yake ya kufanya ‘Solo Album’, wakati huohuo akiendelea kufanyakazi katika bendi ya Quartier Latin. Mwaka 2005 ikatolewa Maxi-Single ya Boma Nga N’elengi, ambapo Fally Ipupa alichangia pia kwenye matayarisho ya album ya Danger De Mort. Hapo ndipo kaamua kuifichua siri yake, akamwendea bosi wake Koffi OLomide, akamwambia nia ya kutaka kutoa Solo Album yake.

Kwa makusudi mazima jambo hilo lilipingwa vikali na Koffi Olomide. Fally Ipupa hakuridhishwa na maamuzi ya bosi wake huyo, mapungufu ya kutokuelewana kati yao yakaanza. Mvutano huo ulijitokeza huku wapambe wa pande zote mbili wakiingilia kati kujaribu kupata suluhisho. Wapambe wa Fally Ipupa wakamshauri aweke tishio la kujiondoa kwenye bendi yake ya Quartier Latin, ikiwa ni njia mojawapo ya Koffi Olomide kukubali kufanya Solo album yake.

Muafaka ukapatikana, ombi lake likakubaliwa, baada ya kuzungumzwa kwenye jopo la uongozi, japo wengi wa Wanamuziki wakawa hawaridhishwi na jambo hilo hasa pande ya Waimbaji. Baadhi ya wanamuziki waliokubali na kumpa kampani, Fally Ipupa ni Modogo Abarambwa na Montana Kamenga, ambao kwa kiasi kikubwa walichangia kwenye album ya Danger de Mort.

Fally Ipupa akatangaza kwenye luninga kwamba wimbo wa Associe, ndio utakao uweka kwenye album hiyo. Baadae akabadili mawazo hayo, akaamua kuweka wimbo wa Pharmacien, huku wa Associe akiuweka kwenye album yake. Mwaka 2006, Fally kajiunga na Lebo ya Obouo Music, iliyokuwa ikiongozwa na David Monsoh ambae ni raia kutoka nchi ya Cote D’Ivoire. (Ivory Coast)

Pasipo kuchelewa David akamtolea Ipupa album yake ya kwanza ya Droit Chemin. Album hiyo ilikubalika mno na kundi la walio wengi, ikafanikiwa kupewa tuzo la Dhahabu baada ya mwaka mmoja tangu itolewe. Ipupa ilipotimu mwaka 2009, ikatolewa album ya Arsenal Des Belles Melodies. Aidha mwaka 2013 wakatoa album ya Power Kosa Leka.

Fally Ipupa ni kiongozi na mmiliki wa Lebo ya F’Victeam), jina ambalo amelipa bendi yake muziki ya Fally na F’Victeam. Walifanikiwa kutoa Album ya Libre Parcours. Baadhi nyimbo za Fally Ipupa ni pamoja na Eloko Oyo, Kiname, Bad Boy, Jeudi Soir, Nidja, Mannequin na Liputa. Nyingine ni Just une danse, Na Lingui Ye, Travelling Love, Mon Amour, Double Clinc, Esengo Sexy dance, Sopeka na Bakandja. Ipupa na kundi lake waliachia vibao vya Associe, Siamois, Cadenas, Orgas na Ndoki.

Walitoka na Video za Origina na Sweet Life na Love don’t care. Video ya Original aliyoitoa Mei 05, 2014, wimbo huo umefuatiliwa na kutizamwa watu takribani million 10 kwenye You Tube. Mwanamuziki Fally Ipupa alifunga ndoa ya asili na bi Nana Ketchup Bafana, mwaka 2000. Kwa kipindi chote cha ndoa hiyo, wamebahatika kupata watoto watatu ambao ni Marcosins, Vincenzo na Jayden.

Mwanawe mwengine ni Keyna, alimpata toka kwa mama mwengine Nicky Menga. Fally ni msanii mwenye moyo wa kusaidia jamii kupitia shirika lake la Fally Ipupa Foundation (FIF) Shirika hilo hutoa misaada mingi kwa makundi ya watu walio na hali duni kimaisha, Watoto, pia hupenda kuwajulia hali wagonjwa.

Fally Ipupa amekwisha nyakua tuzo nyingi za Kimataifa. Mwaka 2008 alipokea tuzo ya msanii bora wa Kiume Afrika kwenye KORA Awards Mwaka 2013, alipewa tuzo la msanii bora wa Afrika kwenye Trace Urban Music Awards. Aidha mwaka huohuo wa 2013, alipata tuzo mbili kwenye Ndule Awards, album bora ya Power Kosa Leka na video bora Eke. Julai 2014, alichukua Tuzo la Afrimma kama mwanamuziki bora wa kiume Afrika ya Kati, jijini Dallas nchini Marekani.

Fally Ipupa amewahi kushiriki kwenye MTV all stars, akiambatana na wanamuziki wenye majina makubwa, akina Snoop Dogg, 2Face Idibia, Flavour na wengineo wengi Wakati wa uongozi wa rais Barack Obama wa Marekani, Fally Ipupa aliwahi kuwa mmoja wa Wasanii wengine walipokea mwaliko kutoka kwa rais huyo, ili wapate fursa ya kushiriki kwenye kikao cha Ushirikiano na Maendeleo kati ya Marekani na nchi za Afrika.

Fally Ipupa ni mmoja kati ya wanamuziki waliotumbuiza mara mbili na kuujaza ukumbi wa kifahari wa Zenith, uliopo katika jiji la Paris nchini Ufaransa. Hiyo ilikuwa kati ya Januari 02, 2010, kwa mara ya pili Ilikuwa Machi 12, 2011. Ikumbukwe kwamba mwanamuziki huyo kijana Fally Ipupa, aliwahi kufika nchini Tanzania, akafanya maonesho kadhaa katika jiji la Dar es Salaam mwaka 2009.

“Bravo Fally Ipupa”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...