Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akikabidhi Vikundi mfano wa hundi ya shilingi milioni 118 ambao ni mkopo kutoka Halmashauri ya Mji Ifakara. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Mashaka Mbilinyi na kushoto kwake aliyevaa tai ni Mkurugenzi Mtendaji wa hiyo Francis Ndulane.
Dkt. Kebwe akimkabidhi baiskeli Afisa Mwandikishaji wa mfuko wa Afya ulioboreshwa Shakila Limbega ili kumwezesha kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Mashaka Mbilinyi na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Francis Ndulane.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanavikundi ambao wamebahatika kupata mkopo wa jumla ya shilingi milioni 118. Kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Mashaka Mbilinyi na kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Francis Ndulane.

…………………………..

Na . Andrew Chimesela

Halmashauri ya Mji Ifakara Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro imetoa Mkopo wa shilingi milioni 118 kwa vikundi vya akina mama, Vijana na watu wenye Ulemavu ambazo zimetokana na makusanyo ya vyanzo vya ndani kwa 2018/2019 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani na kutoa mikopo kwa makundi hayo.

Mkopo huo umetolewa mwishoni mwa wiki katika Ofisi za Halmashauri ya mji wa Ifakara ambapo jumla ya vikundi 69 vimefaidika na Mkopo huo vikiwemo 52 vya wanawake sawa na 75%, 13 ni vya vijana sawa na 19% na Vikundi 4 ni vya watu wenye ulemavu sawa na 6% ya vikundi vyote vilivyopata mkopo huo.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Ifakara Francis Ndulane amesema katika kipindi cha Julai 2018 hadi Februari 2019 Halmashauri ya Mji Ifakara imekusanya jumla ya shilingi 1.1Bil kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato yake ya ndani.

Aidha amesema, katika kipindi hicho Halmashauri imetenga Tsh 110,000,000 ambayo inakaribia asilimia 10% ya makusanyo hayo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye wenye ulemavu.

Hata hiyvo amesema milioni nane zimetolewa na Wahe. Wabunge kwa ajili ya mikopo hiyo ambapo Milioni tatu zimetolewa kutoka katika mfuko wa Jimbo la Kilombero na shilingi Milioni tano zimetolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Mchungaji Getrude Rwakatare na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kuwa 118 Milioni.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akizungumza mara baada ya kukabidhi mfano wa hundi ya fedha hizo kwa wanavikundi, amewataka waliofaidika na mikopo hiyo kuwa waaminifu na kurejesha fedha wanazokopa kulingana na mikataba wanayoweka ili wengine nao waweze kufaidi mikopo hiyo na wasiorejesha wachukuliwe hatua za kisheria.

Sambamba na maagizo hayo Dkt. Kebwe amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kufanya uhakiki wa kina kabla ya kutoa mikopo hiyo kwa kikundi chochote kinachotaka kukopa, amesema engo ni kutaka fedha hizo za Serikali ziendelee kutoa tija kwa watu wengi kadri inavyowezekana badala ya wachache kuchukua fedha hizo na kutokomea kusikojulikana.

Aidha, Dkt. Kebwe ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kutekeleza sharti hilo la kutenga asilimia kumi ya mapato yake na kukopesha makundi tajwa hapo juu kwa kuwa hilo sasa siyo hiari bali ni lazima kwa maelekezo ya Serikali ambapo kati ya asilimia kumi 4 ni za akina mama, 4 nyingine ni kwa ajili ya Vijana na asilimia mbili ni kwa watu wenye Ulemavu.

“Na ole wake Mkurugenzi ambaye atajivuta atazembea katika Mkoa wa Morogoro katika utoaji wa fedha hizi za vikundi, iatakula kwake” alisisitiza Dkt. Kebwe

Hata hivyo Dkt. Kebwe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri wakishirikiana na Wahe. Madiwani kujaribu kubadili mtindo wa kukopesha fedha hizo. Amesema badala ya kukopesha fedha hizo vikundi vingi kwa fedha kidogo kidogo ni vema vikaunganishwa vikundi vingi pamoja na kupewa mkopo mkubwa ili waweze kuazisha hata kiwanda ambapo kitatoa ajira, kutakuwa na faida na kiwanda kitakuwa endelevu hivyo kuwa na tija zaidi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mhe. Mashaka Mbilinyi ametoa wito kwa vikundi vilivyopata mikopo kujiunga na mfuko wa Afya wa CHF ili kuwa rahisi kwao kupata tiba mara wanapopatwa maradhi huku akisisitiza kuimarisha usafi wa mazingira katika maeneo wanayoishi ili kuondoa mlipuko wa magonjwa na kusababisha watu kuwa na Afya dhaifu inayopelekea uchumi kudorola.

Tukio la utoaji wa Mikopo liliambatana na tukio la utoaji wa vifaa vya kufanyia kazi Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) ambapo simu za viganjani tisa zenye thamani ya Tsh. 2,070,000/= zilitolewa huku baiskeli 11 zenye thamani ya shilingi 1,430,000/=pia zilitolewa kwa Maafisa Waandikishaji kuwawezesha kufika maeneo yaliyombali, kuhamasisha watu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...