Na Mary Gwera, Mahakama-Njombe
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Viongozi wa Mahakama Mkoani Njombe kuwa na desturi ya kutembelea Magereza mara kwa mara ili kubaini changamoto mbalimbali na kuchukua hatua.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Mkoani humo katika Ukumbi wa Mahakama ya Mwanzo Makambako Aprili 08, 2019,  Jaji Kiongozi alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa kufanya ukaguzi kwani huwezesha kuangalia mfanano wa hali halisi katika kuendesha mashauri.
“Kuna umuhimu mkubwa katika kukagua Magereza hii husaidia kubaini dosari pamoja na kutambua maeneo yenye udhaifu na kuyafanyia kazi,” alisema Jaji Dkt. Feleshi.
Sambamba na ukaguzi wa Magereza Jaji Kiongozi aliwataka pia kuendelea na kaguzi za Mahakama mbalimbali katika Mkoa wao ikiwa ni pamoja na kukagua rejesta za mashauri kama kumbukumbu za Mashauri na nyinginezo zinawekwa sawa.
Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi aliwasisitiza Watumishi wa Mkoa huo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa maadili ili kuilinda sura ya Mahakama kwa wananchi.
“Majaji na Mahakimu wamekasimishwa madaraka ya kutoa haki duniani hivyo si vyema madaraka haya kuyatumia kwa kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, suala la ukiukwaji wa maadili halina mbadala,” alisisitiza Jaji Kiongozi.
 Jaji Kiongozi alizungumzia pia suala ya usikilizwaji wa Mashauri ambapo alisema kuwa mbali na muda Mahakama iliyojipangia katika umalizaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali haizuii Hakimu kumaliza kesi chini ya muda uliowekwa mfano kwa Mahakama za Mwanzo miezi sita badala yake kesi inaweza kumalizwa chini ya muda huo.
Awali, akiwasilisha taarifa ya hali ya Mahakama mkoani Njombe, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa huo, Magdalena Nason Ntandu alisema kuwa hadi kufikia Desemba, 2018 Mahakama kwa Mkoa mzima ulibakiwa na jumla ya mashauri 492 na kuanzia Mwezi Januari hadi Machi mwaka huu jumla ya mashauri 825 yamefunguliwa katika mkoa huo na mpaka kufikia mwezi Machi, 2019 jumla ya mashauri 891 yalisikizwa na kubaki mashauri 426 ambayo yanaendelea kusikilizwa.
 Ntandu alieleza kuwa Mahakama yake imefanikiwa katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutembelea Mahakama zote ndani ya mkoa huo, kuimarisha mfumo wa usajili wa mashauri (JSDS) kwa kusafisha taarifa zilizokuwa kwenye JSDS 1  kwenda JSDS II, kufanya ukarabati mdogo katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Bulongwa na kadhalika.
Mbali ya Mafanikio, Mahakama katika Mkoa huo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa Watumishi, uhaba wa vyombo vya usafiri pamoja na uhaba wa majengo kwa kuwa baadhi ya maeneo hayana Mahakama.
Aidha katika ziara yake mkoani Njombe iliyopo Kanda ya Iringa, Jaji Kiongozi amekagua mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe ambapo kwa sasa lipo katika hatua ya msingi na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mbunifu majengo kutoka TBA, Bw. Mustafa Ndambachia jengo hilo linatarajiwa kukamilika tarehe Juni 30, 2019.   
Vilevile Jaji Kiongozi alitembelea Mahakama ya Mwanzo Mdandu na kupata fursa ya kuzungumza na Wananchi wa Tarafa ya Mdandu waliofika kumlaki alipotembelea Mahakamani hapo akiwataka kusuluhisha masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na migogoro ya ndoa kwa ngazi ya uongozi wa kijiji na endapo ikishindikana kupata suluhu ndio yaletwe Mahakamani. 
Wananchi hao walieleza kuridhishwa na huduma inayotolewa Mahakamani ikiwa ni pamoja na mchakato mzima wa utoaji haki na umalizaji wa mashauri kwa wakati.  
 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (mwenye suti ya kijivu kulia) akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Ally Kasinge.
 Jaji Kiongozi akionyeshwa mchoro wa jengo la mradi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe.
 Jaji Dkt. Feleshi akizungumza na sehemu ya Wananchi wa Tarafa ya Mdandu waliofika kumlaki alipotembelea Mahakama ya Mwanzo Mdandu. Kushoto kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo.
 Wananchi wakimsikiliza Jaji Kiongozi 
 Jaji Kiongozi akizungumza na Watumishi wa Mahakama mkoani Njombe (hawapo pichani), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Jaji Panterine Kente.
 Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Magdalena Nason Ntandu akiwasilisha taarifa ya hali ya Mahakama mkoani Njombe.

 Watumishi wa Mahakama mkoani Njombe wakimsikiliza Jaji Kiongozi alipokuwa akizungumza nao.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mwanzo Makambako (mwenye tai nyekundu) akimuonesha Jaji Kiongozi eneo la Mahakama hiyo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...