Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia)
akiwa katika kikao cha mwaka cha Majaji wa Mahakama ya Rufani cha
kutathmini utendaji wa mwaka 2018 na kuweka malengo ya mwaka 2019. Kikao
hicho kilifanyika kwa siku mbili (2) Aprili 23 na 24, 2019 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimewashirikisha Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani, Manaibu
Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Wasaidizi wa Kisheria
wa Majaji, Makarani na Watunza kumbukumbu wa Mahakama ya Rufani.
Na Mary Gwera, Mahakama
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu nchini na wote wanaoshughulika na
uandaaji wa kumbukumbu za rufaa kuzingatia sheria na kanuni muhimu
katika uandaaji wa nyaraka hizo ili kuondoa mapungufu yanayoweza
kusababisha usikilizaji wa rufaa kukwama.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi kikao cha siku mbili (2) cha Majaji
wa Mahakama ya Rufani nchini kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) Aprili 24, 2019, Mhe. Jaji
Mkuu alisema kwa kufanya hivyo kutapunguza makosa yanayojitokeza
ambayo kwa wakati mwingine hupelekea ucheleweshaji wa usikilizwaji wa
rufaa hizo kwa kufanya marekebisho mara kadhaa.
“Ni vyema Manaibu Wasajili na Watumishi wanaohusika katika utayarishaji
wa nyaraka hizo, kuandaa vyema kumbukumbu za rufaa ‘records of
appeal’ kwa kuibua makosa mbalimbali yanayoonekana pindi
wanapoandaa kumbukumbu za rufaa ili kuzuia kesi kuchukua muda mrefu
Mahakamani,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Awali, akitoa taarifa ya Utendaji wa Mahakama ya Rufani kwa mwaka
2018, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe.
Elizabeth Mkwizu alisema kwa mwaka huo Mahakama ya Rufani iliweza
kushughulikia jumla ya mashauri 1230 katika jumla ya vikao 38
vilivyofanyika katika Kanda 11 kote nchini.
Mhe. Mkwizu alisema kuwa jumla ya Mashauri 1108 kati ya 1230
yaliyopangwa katika vikao hivyo yalimalizika ikiwa ni asilimia tisini (90%) ya
mashauri yote yaliyopangwa kusikilizwa.
“Hiki ni kiwango kizuri pamoja na kuwa lengo la kumaliza mashauri kwa
asilimia mia moja (100%) halikutimia, hata hivyo tunatoa pongezi kwa wote
waliochangia mafanikio hayo,” alieleza Mhe. Mkwizu.
Akizungumzia muda wa mashauri kukaa Mahakamani, Mhe. Mkwizu
alisema kuwa takwimu za mashauri zinaonyesha kushuka kwa wastani wa
muda wa rufaa za jinai kukaa Mahakamani kutoka siku 5240 mnamo
Februari, 2017 hadi siku 898 kufikia mwishoni mwa Desemba 2018 na
kusema hii ni hatua kubwa.
Kwa upande mwingine, kwa mwaka huu 2019 Mahakama ya Rufani
imejiwekea malengo ya kuendelea kusikiliza mashauri na kuimarisha
masjala.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mpango kazi wa Mahakama ya Rufani ya mwaka
2019 Mahakama ya Rufani tayari imepitia Rejista na kukusanya takwimu
za mashauri, kufanya ‘stock taking’ ya mashauri yaliyopo katika masjala,
kuainisha idadi ya mashauri yaliyopo kwa kanda na kwa umri lengo likiwa
ni kuweka mkakati wa uondoshaji wa mashauri ya zamani kulingana na
mzigo uliopo kwa kila kanda.
Mkutano wa mwaka huu wa Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani pia
uliwashirikisha Manaibu Wasajili, wasaidizi wa kisheria wa Majaji, Makarani
na watunza kumbukumbu ambao walitoa taarifa za utendaji kazi pamoja na
changamoto zinazowakabili ili waweze kusaidiana kwa pamoja kupanga
mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...