Na Frank Mvungi- MAELEZO 

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imetajwa kutoa huduma katika viwango vya kimataifa na hivyo kupokea wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo ya Afrika Mashariki na Kati. 

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa kwa sasa taasisi hiyo ina vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ikiwemo mtambo wa kufanyia upasuaji kwa njia ya tundu dogo bila kufungua kifua cha mgonjwa kama ilivyo katika nchi zilizoendelea. 

“Kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali katika taasisi yetu kwa mwaka 2018 tuliweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 1400 ambao pengine wangetakiwa kupelekwa nje ya nchi hivyo tumeasaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi wenye magonjwa ya moyo” alisisitiza Prof. Janabi. 

Akifafanua amesema kuwa jukumu lao kama taasisi ni kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa wananchi na kwa sasa wagonjwa takribani 300 wanahudumiwa katika taasisi hiyo kila siku. 

Aliongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inafanya upasuaji kwa wagonjwa zaidi ya asilimia 85 wanaofika kupata matibabu, lengo likiwa kufikia asilimia 90 kutokana na uwekezaji unaofanywa na serikali ya awamu ya tano. 

“Bilioni 5 zimetumika kununua na kusimika mtambo wa kusaidia kufanya upusuajia kwa njia ya tundu dogo” alisisitiza Prof. Janabi .Pia wameanzisha kitengo maalum cha kuhudumia watoto wenye matatizo ya moyo na kufanya uchunguzi kwa watoto wakiwa bado hawajazaliwa ili kuona kama wana tatizo lolote katika moyo. 

Katika kuimarisha huduma zake JKCI imekuwa na utaratibu wa kualika madaktari bingwa wa moyo kutoka hospitali rafiki kwa ajili ya kushirikiana kufanya upasuaji na kukuza ujuzi kwa madaktari bingwa wazalendo. 

Baadhi ya huduma mpya zilizoanzishwa ni pamoja na huduma ya kuweka betri kwenye moyo, kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo ambapo wagonjwa 7 hadi 10 wanafanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo na wagonjwa 2 hadi 4 upasuaji kwa njia ya kufungua kifua kila siku. 

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kitwete imejengwa kwa gharama ya Bilioni 26 na imekuwa ikiboresha huduma zake mwaka hadi mwaka ili kukidhi mnahitaji na kupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kupata matibabu ya moyo ambapo tayari inahudumia asilimia 85 ya wagonjwa wote wanaofikishwa katika taasisi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...