KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa Yanga zimezinduliwa rasmi leo kwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Dkt. Mshindo Msolla amesema kuwa uzoefu wake katika sekta ya michezo utamsaidia kuibadilisha Yanga na kuleta mabadiliko.

Dkt. Msolla amezindua kampeni hizo katika makao makuu ya Klabu ya Yanga na kunadi sera zake mbele ya wanachama wa klabu hiyo na kueleza kuwa uzoefu wake katika sekta ya  michezo kwa muda wa miaka 40 utamsaidia kuweza kutekeleza mipango ya klabu kwa wakati na lengo kuu ni kuirudisha timu kwa Wananchi.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo, Msolla amesema kuwa amedhamiria kuleta mabadiliko ndani ya Yanga ili kutatua changamoto zilizopo kwenye taasisi hiyo ikiwemo ya uongozi ambalo lilikuwa linaathiri ufanisi wa klabu.

"Kwa kipindi kirefu kumekuwa na changamoto ya kiuongozi na matokeo yake changamoto hiyo imefanya kuwe na ombwe la uongozi, nimeamua kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa klabu kwa sababu nina uzoefu wa kutosha hasa baada ya kuwa kwenye tasnia ya mpira kwa muda wa miaka 40 katika nyanja mbalimbali,"

"Nitahakikisha ninajenga umoja ndani ya klabu kwa wanachama na wapenzi wa Yanga na kuirudisha timu kwa wananchi kwa kuimarisha matawi yaliyopo, kuanzisha matawi mapya, matawi kupelekewa katiba ili wawe na uelewa wa katiba ya klabu yao na kuendeleza mchakato wa maboresho ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.

"Nitahakikisha Yanga inatengeneza Historia yake kwa kuboresha eneo la klabu na kufanya iwe sehemu ya utalii kama ulaya bila kusahau maboresho ya uwanja wa Kaunda pamoja na ukarabati wa jengo la klabu pamoja na kuweka misingi bora ya uwajibikaji," amesema Msolla na kuomba wanachama wamchague.

Yanga inatarajia kufanya uchaguzi wake Mei 5 mwaka huu na leo kampeni zimezinduliwa rasmi kwa wagombea ili kupata viongozi wapya kwa ngazi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ndani ya Yanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...