Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani Songwe. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan ametoa rai kwa Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 kumkumbuka Baba wa Taifa
kwa kupinga vitendo vya dhulma, ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau
na kuwataka kuenzi umoja na mshikamano wetu kuchapakazi kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa.
Makamu
wa Rais ameyasema hayo leo kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge
Kitaifa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
“Nimependezwa
na kaulimbiu hii ambayo inauwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la
kila siku la kusimamia na kutunza mazingira ya nchini. Sote tunafahamu
kuwa bila utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji hupotea”alisema Makamu wa Rais
Hali
ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini inaendelea
kuimarika ambapo huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka wastani wa
asilimia 58.7 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari
2019 na miji mikuu ya mikoa kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka
asilimia februari 2019.
“Niwahakikishie wananchi
tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi
inayotutaka kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 85 na
mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais
Aidha,
Makamu wa Rais kupitia hadhara ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
Kitaifa mwaka 2019 ametoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo,
ufugaji, ujenzi, ukataji na uchomaji miti kwenye vyanzo vya maji.
Makamu
wa Rais pia amewakumbusha wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa
utakaofanyika mwezi oktoba 2019 kuhakikisha wanachagua Viongozi
wachapakazi na wenye dhamira ya maendeleo kwa jamii.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...