Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza ofisini kwake mjini Babati.
……………………….
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema sekta ya afya ni nyeti isiyopaswa kuingiliwa na wanasiasa ila madaktari na wauguzi wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo ikiwemo kuzuia vifo vya mama na mtoto.
Mnyeti aliyasema hayo mjini Babati, wakati akizungumza na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, madaktari na wauguzi kwenye uzinduzi wa kampeni ya jiongeze tuwavushe salama. 

Alisema kazi ya viongozi ni kusimamia utekelezaji na madaktari na wauguzi wafanye kazi zao kwa vitendo huku wakitumia lugha nzuri pindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa. Alisema wataalamu wa afya wanapaswa kutimiza wajibu wao katika uwajibikaji na kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga waweze kuwa watu wazima. 

“Kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatimiza jukumu lake ikiwemo kupatiwa huduma bora ili kudhibiti vifo vya kina mama na watoto pamoja na kutoa elimu kuanzia ngazi ya jamii,” alisema Mnyeti. Alisema kwa mujibu wa sera za afya nchini, huduma za uzazi hutolewa bure ila kuna baadhi ya maeneo malalamiko ya mama wajawazito kudaiwa fedha yamekuwa yakitolewa. 

“Halmashauri na wengineo kasimamieni hilo inawezekana suala la kuwatoza fedha wajawazito au wa mama waliojifungua halipo kwetu ila lichunguzwe na kufanyiwa kazi,” alisema Mnyeti. Mkazi wa mjini Babati, Aloyce Bura aliiomba serikali kuhakikisha wanaboresha huduma kwenye hospitali ya mji wa Babati (Mrara) ikiwemo upungufu wa watumishi na dawa. 

Bura alisema wakati huu ambapo serikali inaboresha huduma za afya ikiwemo kujenga vituo vya afya na hospitali za wilaya inapaswa kuongeza watumishi na dawa. Mkazi wa mtaa wa Miyomboni, Mariam Sulle aliwapongeza wauguzi wa hospitali ya Mrara kwa kuwa na lugha nzuri kwa wanawake wajawazito pindi wanapowahudumia tofauti na awali. 


“Mgonjwa anahitaji faraja na lugha nzuri, niwapongeze kwa kutoa huduma zao ipasavyo kwani ukitoa lugha mbaya mgonjwa anaona bora akafie nyumbani kwao kuliko kutukanwa hospitalini,” alisema Sulle.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...