Na Moshy Kiyungi

Katika orodha ya wachezaji waliowahi kuicheza klabu ya Dar Young Africans ya Tanzania, Fredy Mayaula Mayoni ni miongoni mwao. Historia inaeleza kuwa baba yake alikuwa mwanadiplomasia katika ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire) nchini Tanzania, Mayaula alimfuata baba yake na ndipo alipojiunga klabu hiyo.

 Mayoni alikuwa mwanamuziki mkongwe mwenye kipaji cha utunzi na kuimba muziki wa dansi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alikulia na kusomea katika jiji la Dar es Salaam, mnamo  miaka ya 1960. Alimaliza shule za awali bila matatizo na kumaliza elimu yake mwaka 1962, katika chuo cha Kisantu nchini humo.

Fredy alipenda sana kusakata mpira wa miguu. Kati ya mwaka 1968 na 1971,  akicheza nafasi ya winga wa kushoto katika klabu ya ‘AS Vita  ya Kinshasa. Aidha katika juhudi zake za kujituma katika uchezaji wa mpira huo wa miguu, aliweza kuchaguliwa hadi  timu ya taifa ya nchi yake.

Akiwa Tanzainia, Mayaula alianza kuonesha cheche za kusakata kabumbu mara alipojiunga na klabu Dar Young Africans ya jijini Dar es Salaam. Baadae aliondoka akaelekea jiji la Charleroi, nchini Ubelgiji alikokwenda kujiendeleza kimasomo katika maomo ya Data Processing. Akiwa huko alijiunga na timu ya mpira ya ‘Racing Club de Charleroi’ baadae akajiunga na ‘Racing Club de Jette’ ya Brussels.

Mayaula kwa muda mfupi alichezea timu ya FC Fribourg ya Switzerland, na katika kipindi hicho alipoanza kujifunza kupiga gitaa. Muda si mrefu akajiunga na bendi ya wanafunzi wa Kikongo, iliyokuwa ikiitwa Orchestra Africana, akiwa kama mpiga gitaa la rhythm.

Fred aliporudi Kinshasa, akabadili kazi kutoka kwenye mpira wa miguu na kuwa mwanamuziki mtunzi. Haikuchukua kipindi kirefu kugundulika kipaji chake na kiongozi wa bendi ya T.P.OK. Jazz, Franco Luambo Makiadi, aliyemtaka kujiunga katika bendi yake.

Mayoni ndiye aliyetunga wimbo wa Ndaya mwaka 1977, ukaimbwa na mwanamuziki Mpongo Love. Wimbo huo ulikuwa unaongelea kuhusu mwanamke aliye na furaha kutokana na kuwa na mume bora na kuweza kumbana mumewe kutoka kwa wanawake wengine.

Mayaula alitunga wimbo mwingine ‘matata’ uliokuja kuwa maarufu wa Cherie Bondowe’ au ‘Sherry Bondowe. Kibao cha Cherie Bondowe, kilipokewa vizuri sana na wapenzi wa muziki. Kwa bahati mbaya National Censorship Commission ya Zaire wakati huo, iliupiga marufuku wimbo huo kwa kuwa hadithi yake ilikuwa ikimuelezea ‘changudoa’ mmoja aliyekuwa akibainisha shughuli zake zilivyo.

Wasifu wa Fredy Mayaula Mayoni unaonesha kuwa alizaliwa Novemba 06, 1946,  katika jiji la LĂ©opoldville, ambalo sasa linaitwa Kinshasa. Yasemekana kuwa japo Franco alimkaribisha Mayaula kujiunga na bendi hiyo, hakuwahi kuwa mwanachama halisi wa kundi hilo kwani alipendelea kuwa huru kutunga nyimbo zake.

Tungo zake kadhaa zilifanyiwa kazi na T.P. OK. Jazz kama vile Nabali Misere na Moni. Mayaula aliondoka  Zaire mwaka 1981 akiwa na wanamuziki kutoka bendi ya Abeti Masikini na kuhamia Afrika Magharibi. Hadi kufikia mwaka 1984, tayari likuwa merekodi album kadhaa chini ya label ya Disc-orient ya mjini Lome nchini Togo.

Mwaka 1984 alirudi Zaire, ilipotimu  mwaka 1986 alitoka na album iliyoitwa ‘Fiona Fiona’. Mwaka huohuo Tshala Muana alipata umaarufu kutokana na wimbo Nasi Nabali’, uliotungwa na Mayaula Mayoni. Baada ya hapo akarekodi album yake Mizele akiwa na T.P. OK Jazz, wakisindikizwa na waimbaji Carlito Lassa na Malage de Lugendo.

Album ya ‘L’amour au Kilo, ilifyatuliwa mwaka 1993 na miaka saba baadae akatoa album nyingine ya Bikini. Baada ya album hiyo Mayaula alihamia Dar es Salaam na kuanza kufanya kazi ubalozi wa Kongo. Wakazi wengi wa Magomeni jijini Dar es Salaam watamkumbuka Mayaula, ambaye  katika kipindi hicho akifanya kazi ubalozini, alikuwa akiishi maeneo hayo.

Baadaye Mayaula Mayoni akaanza kuugua na kuamua kurudi kwao alikozaliwa katika kijiji cha Makadi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hali ya afya yake ilizidi kuwa mbaya mwaka 2005  alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda kwa Mayaula akafariki dunia katika jiji hilo la Brussels nchini Ubelgiji  Mei 26, 2010 akiwa na umri wa miaka 64. Katika maisha yake ya muziki, Mayaula aliwahi kuchaguliwa kama mtunzi bora nchini mwake Zaire 1978, kwa wimbo  Bondowe 2, mwaka 1979 kwa wimbo Nabali Misere na mwaka 1993 Ousmane Bakayoko’

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...