Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akiongea na wafanyakazi wa Tume ya Madini kwenye ukumbi wa mikutano katika ofisi za Tume hiyo mkoani Morogoro. Kulia kwake ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki. Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akitolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyo wasilishwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi Morogoro wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa Tume ya Madini alipotembelea kwa ziara ya kikazi. Kulia kwake ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki na kushoto ni Mhandisi Emmanuel Shija Kaimu Afisa Madini Mkazi Morogoro.


Athanas Macheyeki Kamishna wa Tume ya Madini mwenye vitabu mkononi akimsikiliza jambo Mwenyekiti wa Tume Prof. Kikula wakati wakikagua maeneo mbalimbali yanayo zunguka ofisi za Tume ya Madini Mkoa wa Morogoro
…………….

Na Issa Mtuwa- Morogoro

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amekerwa na kukasirishwa na ukosefu wa uadilifu kwa wafanyakazi wa Tume ya Madini katika baadhi ya Ofisi na kueleza kuwa, suala hilo halitavumilika kwa wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi.

Akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Madini Mkoa wa Morogoro katika siku ya kwanza ya ziara yake aliyoianza Aprili 8, 2019, Prof. Kikula amewaeleza wafanyakazi wa ofisi hiyo kuwa, yeye na viongozi wenzake wa tume wamekerwa na kusononeshwa na vitendo vya ukosefu wa uadilifu vinavyofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Tume ya Madini.

Ametolea mfano wa kitendo kilichofanywa na wanafanyakazi wa Tume hiyo wilayani Chunya ambapo watumishi wote wa kituo hicho wamesimamishwa kazi na Waziri wa Madini Doto Biteko kutokana na kukosa uadilifu na kutoa taarifa isiyo sahihi kwenye takwimu za madini.

“Kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na wachenjuaji madini, na udanganyifu huo unachochewa na watumishi wa Tume. Angalia mfano pale Chunya, wale wachenjuaji wamedanganya lakini ukifuatilia utagundua wafanyakazi wa tume wanahusika na huo udanganyifu, na ndio maana hata Waziri wa Madini aliamua kuchukua hatua ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi wote wa kituo kile,” amesema Prof. Kikula.

Kufuatia hali hiyo, Prof. amekemea vitendo hivyo na kueleza kuwa, suala la uadilifu ni muhimu katika kazi za watumishi wa tume na kueleza kuwa, pamoja na kuwepo vishawishi vingi katika sekta ya madini, lakini wanapaswa kukumbuka kuwa kazi ni muhimu kwao na familia zao.

“Mimi na wenzangu tunaumizwa moyoni tunapoona wafanyakazi wa Tume wanakutwa na hatia ya ukosefu wa uadilifu inatusikitisha sana, sana”, amesisitiza Prof. Kikula.

Akitolea ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yaliyowasilishwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi, Prof. Kikula amewapongeza watumishi wote wa kituo cha madini Morogoro kwa kazi nzuri ya kusimamia ukusanyaji wa maduhuli na kuwaomba kuongeza bidii ili wafikie malengo waliyojiwekea.

Kuhusu masuala ya leseni, Prof. Kikula amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi kufuatilia leseni zote zilizopo na kubainisha leseni ambazo sio hai na kuzifuta kwa mujibu wa sheria. Aidha, amekumbusha kuhusu kufuata utaratibu halali uliowekwa kwa mujibu wa sheria katika hatua za ufutaji wa leseni hizo na kusema “asimuogope mtu lakini pia asimuonee mtu katika hatua hiyo ya ufutaji wa lesini zisizo hai”.

Aidha, Prof. Kikula amekiri kuwepo kwa changamoto na kuwataka watumishi hao kuwa na subira na kuongeza kuwa, Tume imepanga kununua magari 34 ambayo yatasambazwa katika mikoa yote ili kuongeza tija. Prof. Kikula amezungumza hayo baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya ofisi hiyo ambayo ilieleza kuwepo kwa changamoto kadhaa.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkazi Morogoro Mhandisi Emmanuel Shija akisoma taarifa ya ofisi hiyo, pamoja na mambo mengine, amemweleza Mwenyekiti wa Tume masuala kadhaa yanayosimamiwa na ofisi hiyo ikiwemo uanzishwaji wa soko la Madini, ufutaji wa lesseni za uchimbaji kwa wamiliki wanaoshindwa kutimiza vigezo vya leseni zao, ukusanyaji wa maduhuli na changa moto zinazo wakabili katika kutekeleza majukumu yao.

Mhandisi Shija amesema, pamoja na changamoto zilipo, ofisi hiyo inafanya jitihada za kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ambapo mpaka sasa imefikia asilimia 53 ya lengo na kwamba, inategemea kufikia malengo ya ukusanyaji waliyojiwekea.

Naye, Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Macheyeki ambaye amembatana na Mwenyekiti wa Tume, amewapongeza kwa ukusanyaji mzuri wa maduhuli na kuwataka kujiwekea muda wa utekelezaji wa malengo ili waweze kujipima vizuri.

“Unapojiwekea muda wa utekelezaji unakufanya uongeze bidii pindi unapoona uko nyuma ya muda ya utekelezaji wa lengo hivyo ni muhimu wa kulizingatia hilo,”amesema Dkt. Macheyeki.

Prof. Kikula na Dkt. Macheyeki wako mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa shuguli za Tume katika Wilaya mbalimbali zinazofanya shuguli za madini sambamba na kutatua kero za wachimbaji na wadau wa madini, mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...