NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema Chama hicho kimejizatiti kutatua kero za wananchi pamoja na kusimamia Demokrasia kwa kukemea vitendo viovu vinavyohatarisha Amani na Utulivu wa Nchi.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua Uhai wa Chama na Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja, amesema vipaumbele vya CCM ni kutekeleza kwa kasi ahadi zilizotolewa na Taasisi hiyo kwa wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuaminiwa,kupendwa na kuthaminiwa na Mamilioni ya Watanzania kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Sera zake, kwa kutatua changamoto za kijamii kwa wakati mwafaka.

Aidha alisema katika kusimamia dhana ya Demokrasia CCM haitosita kukemea vitendo viovu vinavyoashiria kuvunja Sheria za Nchi, hasa vinavyotekelezwa na baadhi ya Vyama vya upinzani.

“Tumekubali kuingia katika mfumo wa Vyama vingi ili tushindane kwa Sera na sio kushindana kwa vituko na vurugu ni muhimu kila mwanasiasa kujitathimini juu ya mwenendo wake kwa jamii anayoiongoza.”, alisema Dk.Mabodi.

Alisema katika zama za CCM mpya imekuwa imekuwa ni kimbilio la wananchi wanaoamini katika siasa za maendeleo ambao wametelekezwa na Vyama vyao na kupokelewa  vizuri ndani ya CCM ili wanufaike na Demokrasia iliyotukuka.

Aliwataka Viongozi na Watendaji wa CCM kutowawekea vikwazo Wananchi wanaotaka  kujiunga na Chama na badala yake wapewe fursa hiyo bila masharti magumu sambamba na kuwasomesha miongozo na itikadi za kitaasisi.

Aliwaagiza Wabunge,Wawakilishi na Madiwani kufanya mikutano katika maeneo yao ya kuwaeleza Wananchi mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Ilani ili wananchi hao wawe Mabalozi wa kufikisha taarifa hizo kwa jamii.

Aliwambia wananchi kuwa CCM imesimamia kwa ufanisi miradi ya maendeleo ukiwemo wa TASAF ambao upo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, ambao umewaondosha wananchi katika wimbi la umasikini na kuwa na kipato cha kati.  

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa mbali mbali vikiwemo Runinga (Television) pamoja na Fedha kwa vikundi 11 vya Saccos ya Shehia ya Mzuri katika Maskani ya CCM ya Kisonge Makunduchi Dk.Mabodi amesisitiza kuwa uhai wa Taasisi hiyo ya kisiasa unaanza kuimarishwa kuanzia ngazi ya mashina.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Mhe.Haroun Ali Suleiman alisema tayari Ilani ya CCM ndani ya Jimbo hilo imetekelezwa kwa asilimia 90, na kwa sasa wanaendelea kutatua baadhi ya changamoto ili kuzimaliza kabla ya 2020.

Mhe.Haroun alisema kwa kushirikiana na Kamati ya Siasa ya Jimbo hilo amefanya ziara katika Shehia zote 13 za Jimbo kwa kuratibu changamoto zinazowakabili wananchi na nyingi zimetatuliwa sambamba na kueleza fursa na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Ameir Haji Timbe alisema maendeleo yaliyopatikana katika Jimbo hilo yametokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya viongozi na wananchi.

Akizungumza Mwenyekiti wa Maskani ya CCM ya Kisonge iliyopo Makunduchi Abdallah Hassan Haji alisema wanaendelea kuvuna wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani huku wakijipanga kufuta masalia ya upinzania ndani ya Jimbo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Maskani ya CCM ya Hapa Kazi Tu Yussuf Abeid Haji, akizungumza katika uzinduzi wa Maskani hiyo alisema eneo la maskani yao litatumika kuwa chachu ya kujenga umoja,mshikamano pamoja na kuwa kituo mbadala cha kubuni miradi mbali mbali ya maendeleo kwa maslahi ya Wana CCM.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akiwa amebeba mtoto mara baada ya kuzungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kibuteni alipoenda kukagua uwanja wa mpira wa kisasa unaojengwa katika Kijiji hicho.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akiwahutubia Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla katika ziara yake ya kukagua Utekelezaji wa Ilani katika Maskani ya CCM ya Kisonge, iliyopo Shehia ya Mzuri Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akiwa amebeba ndoo yenye udongo katika ujenzi wa Tawi la CCM Miwaleni Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
  MWAKILISHI wa Jimbo la Makunduchi Mhe.Haroun Ali Suleiman akisomba udongo wa kifusi wa kuweka katika Tawi la CCM la Miwaleni katika ziara ya kukukagua uhai wa Chama na Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo hilo Wilaya ya Kusini Unguja.
 MKUU wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Mustafa Kitwana (aliyebeba kifaa cha kubebea udongo wa kifusi wa pili kushoto) akishiriki katika ujenzi wa Taifa wa Tawi la CCM Miwaleni Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizindua Maskani ya CCM ya Hapa Kazi Tu iliyopo Mtende Mndo Makunduchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...