Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa akitembezwa na wahandisi na viongozi wa TBA kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam alipofanya ziara yake leo.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa (kulia) akipata maelezo kwenye chumba cha kuendeshea mtambo wa kuchakata zege katika mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam alipofanya ziara yake leo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Eng. Jasper Lugemarila (katikati) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) alipofanya ziara leo kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa wa Magomeni Kota.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Eng. Jasper Lugemarila (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa (wa pili kulia) alipofanya ziara leo kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa wa Magomeni Kota. Wengine ni wahandisi wa mradi huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) akitoka katika moja ya majengo ya mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam alipofanya ziara yake leo.

……………………

NAIBU Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa ameagiza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kuhakikisha wanamaliza Mradi wa Nyumba za Kisasa wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam unamalizika kufikia mwezi Desemba mwaka huu.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Kwandikwa ametoa msisitizo huo leo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema kuanzia sasa atakuwa akiutembelea mradi huo kila mwezi ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na hatimaye mradi ukamilike Desemba kama ilivyoagizwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli alipoutembelea mradi huo hivi karibuni.

“…Kuanzia leo nitahakikisha nawatembelea hapa kama sio kila wiki basi kila mwezi, lengo langu ni kuhakikisha mradi huu mkubwa unakamilika kwa wakati na wananchi hawa wapatao 656 waliokuwa wakiishi hapa wanaingia na kuanza kuzitumia nyumba hizi,” alisema Naibu Waziri.

Aidha aliongeza kuwa wizara yake itahakikisha inafika eneo hilo kila mara kutatua changamoto zote ambazo zitakuwa zikihitaji kutatuliwa na wizara hiyo, huku akionya itakuwa ni jambo la kushangaza endapo mradi huo utasimama tena na kumlazimu Rais Dk. Magufuli arudi tena eneo hilo.

“…Sisi kama wizara tunataka endapo Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli akija tena eneo la Magomeni Kota ni kufanya uzinduzi wa nyumba zikiwa zimekamilika na si vinginevyo,” alisisitiza Naibu Waziri Kwandikwa akizungumza na viongozi na waandisi wa TBA wanaosimamia mradi huo.

Aliipongeza TBA kwa kitendo cha kuanza kutumia mitambo ya kisasa ya kufyatua matofali, kuchanganya na kubeba zege hadi gorofani jambo ambalo litaongeza kasi ya ujenzi na ufanisi katika mradi huo.

Aliwataka kuangalia namna ya kuanza haraka kufanya kazi usiku na mchana kutokana na ujio wa mitambo hiyo. Alisema wazo la kuanza kufanya kazi usiku na mchana licha ya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi linatoa fursa kwa vijana wengi sasa kuja kufanya kazi na kujipatia kipato.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA, Eng. Jasper Lugemarila akizungumzia changamoto zilizokwamisha mradi huo awali, alisema ilikuwa ni kupanda kwa bei ya zege ambayo walikuwa wakinunua pamoja na bidhaa nyingine kama simenti, kokoto na nondo.

Alisema kwa sasa wamekwisha tatua changamoto hizo baadha ya kuanza kutengeneza zege wenyewe kwa kutumia mitambo ya kisasa inayoendeshwa na kompyuta.

“…Mwanzoni tulikuwa tunamimina zege kwa kununua kutoka kwa wafanyabiashara hiyo, lakini walipoona mradi huu umeanza na ni mkubwa wakatupandishia bei sana wakijua lazima twende kwao,” alisema Eng. Jasper Lugemarila

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...