Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

HAKAMATIKI kabisa na atabaki kuwa kileleni!Ndivyo unavyoweza kuelezea kuhusu Peter Mollel a.k.a Pierre Luquid baada ya leo Machi 3, 2019 kutinga Bungeni kwa mualiko maalum wa Spika wa Bunge Job Ndugai.

Pierre anapata mualiko huo katika kipindi ambacho jina lake limekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii .Kwa siku kadhaa Pierre amekuwa akijadliwa sana lakini leo hii ameibukia Bungeni.

Kabla ya kuingia bungeni leo mapema asubuhi Pierre alipata nafasi ya kukutana na mwenyeji wake Spika Ndugai ambapo walisalimiana na kisha kama kawaida  yake akatoa kibwagizo kwa kumwambia hivi "Ndugai ooooo...utabaki kuwa juu mawinguni" .Kibwagizo hicho kilimfanya Spika aliyekuwa ameambatana na Naibu Spika Dk.Tulia Akson na maofisa wengine wa Bunge kubaki wakicheka.

Katika kudhihirisha Pierre nyota yake imeng'aa na hakuna wa kuizima kwa sasa amepata nafasi ya kuzungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amemuhakikishia Pierre ambaye anajulikana kama Mhamasishaji wa Taifa Stars kuwa kutakuwa kuna tiketi yake ya ndege ya kwenda kushiriki na timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' iliyofuzu mashindano ya AFCON 2019.

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa anazungumza na Pierre katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma.Pierre amekwenda Dodoma kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania na akiwa kwenye ndege hiyo aliamua kupiga picha akionesha ile ishara yake ya kubaki kileleni.

Kwa kukumbusha tu Pierre ni moja ya watu mashuhuri kwa sasa ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuhakikisha anahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye mechi kati ya Taifa Stars na Uganda ambapo Taifa Stars iliubuka na ushindi.

Wakati Rais Dk.John Magufuli alipokuwa amewaalika Ikulu jijini Dar es Salaam wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa TFF, bondia  Hassan Mwakinyo, Kamati ya Saidia Taifa Stars na wadau wengine wa soka, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alionesha kutambua mchango wa Pierre katika uhamasishaji kuelekea mchezo huo uliofanyika siku kadhaa zilizopita.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (kulia) akisalimiana na Mhamasishaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Taifa Stars, Ndg. Peter Mollel alimaarufu kama Pierre Liquid walipokutana leo katika Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma, kabla ya kumualika Bungeni kwa ajili ya kusikiliza Vikao vya Bunge vilivyoanza jana Jijini Dodoma. Katikati ni Katibu wa Bunge, Ndg. Stephen Kagaigai

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...