Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Profesa. Elisante Ole Gabriel amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo hususan uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Wanyama.

Hospitali hiyo ni taasisi pekee nchini inayosaidia kutoa ushauri, tiba na chanjo kwa wanyama wa kufugwa na waporini ambao wamepewa rufaa kutoka katika Hospitali ndogo ndogo za wanyama, taasisi za serikali na binafsi ambazo huhifadhi na kuwatunza wanyama hao ambao hupatikana kisheria.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku moja chuoni hapo leo Aprili 23, 2019, Prof. Gabriel amesema alipata fursa ya kuzunguka nchi za Afrika Mashariki lakini hakuwahi kusikia uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Wanyama na hivyo kuwataka waandishi wa habari kwa kushirkiana na kitengo cha Mawasiliano na Masoko kuhakikisha Umma unafahamu kuhusu Hospitali hiyo kuwepo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

“Nimefurahishwa na Hospitali ya Rufaa ya Wanyama hapa SUA ambayo ni kwa Tanzania nzima, ni vyema tukauhabarisha Umma kuhusu hili na ikibidi Waziri aweze kutembelea Hoapitali hii, kiukweli nimefurahishwa sana na mambo niliyoyaona hapa SUA na nashukuru ziara yangu hii sikukosea kuifanya hapa”. Alisema Prof. Gabriel.

Pia aliongeza kuwa SUA inaweza kuwa zaidi ya eneo la mafunzo kwani kuna utalii ndani yake ambapo aliwashauri watumishi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya kuanzisha programu ya Utalii ambapo watu wakija kufanya mafunzo ya tiba ya wanyama wapate kujionea mambo ya Utalii yaliyopo katika Ndaki hiyo na hata Ndaki nyingine. 

Aidha, Prof. Gabriel alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo na kujionea shughuli zinazofanywa ambapo alipata fursa ya kuona wanyama wakipatiwa tiba ikiwemo upasuaji wakiwa katika uangalizi wa madaktari maalum wa wanyama.

“Sikuwa najua kama paka anaweza akafanyiwa upasuaji na kukatwa mguu na bado akaendelea kuwa hai hivyo natoa wito kwa wananchi wote kutumia Hospitali hii kuleta wanyama wao ili waweze kupatiwa matibabu mbalimbali, mimi nimefanikiwa kuona paka aliyefanyiwa operesheni na kukatwa mguu pamoja na mbwa ambao wote wako katika hali nzuri”, alisema Prof. Gabriel.

Katibu Mkuu huyo pia alipata fursa ya kuzungumza na Menejimenti ya Chuo na kuwataka kuendelea kuzalisha wahitimu bora na kuwafanya kuwa ni wahitimu waliofundishwa kwa vitendo zaidi kuliko nadharia huku akishauri kuwa Chuo kitoe uelewa kwa wanafunzi kuwa sekta ya mifugo ni sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 50 ya wataalam wa mifugo na kutambua kuwa ni vyema wajijengee hari ya kutaka kujiari ili nao waweze kuja kuajili wengine pia.

“Ili tumuenzi Rais wetu John Pombe Joseph Magufuli ambaye ameonyesha msukumo wa pekee ni vyema tuhakikishe wahitimu wetu wanakuwa na uelewa kwa vitendo na si nadharia tu ili kutatua changamoto za wanafunzi”, alishauri Prof. Gabriel.

Aliongeza kuwa chuo kinatakiwa kuongeza nguvu katika kutoa mafunzo ya biashara (Business knowledge) hususan katika upande wa tiba ya wanyama na Sayansi ya wanyama ili kuwapa wataalam ujuzi wa masuala ya biashara.

“Nina hakika tukiongeza mafunzo ya biashara kwa wataalam wetu itasaidia kupata wanafunzi wa tofauti sana ambao mara baada ya kumaliza Chuo wakienda mtaani hawatapwaya katika utendaji kutokana na taaluma waliyopewa kwani biashara ndio kila kitu”, aliongeza Prof. Gabriel.

Prof. Gabriel amesisitiza Chuo hicho kihakikishe kinawagusa wafugaji wa chini kwa kushirikiana na Wizara kuwapeleka wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika sehemu halisia za kujifunzia.
“Chuo kishirikiane na Wizara pamoja na Tamisemi kuandika barua ili kuomba Wilaya mbalimbali zikubali kuwapokea wanafunzi wetu na kuwapatia maradhi badala ya kuwaacha wanafunzi hao kwenda mahali ambapo hawatapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo wakijaribu kukwepa gharama za kujihudumia wawapo katika mafunzo na hivyo kuangalia wapi wana jamaa ambao wanaweza kupata hifadhi”, alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chubunda alimshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na mchango wa mawazo ambapo alisema kwa kiasi Chuo kimeshaanza kushughulikia baadhi ya masuala hususani kuwa na mahali halisia pa kujifunzia na hivyo kuanzisha mashamba darasa ya mazao ya kimkakati kwa ajili ya wanafunzi na jamii kwa ujumla.

 “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Mgufuli kwa kuwekea mkazo uwezeshaji kwenye vyuo na hasa chuo chetu kwa miaka miwili iliyopita kuna mambo makubwa ambayo huko serikali ilikuwa kama imevisusa vyuo vyake na kubaki kama yatima na kusababisha kuchakaa kwa baadhi ya miundombinu ya kufundishia mfano chuo chetu tunategemea mashamba na karakana ambazo kwa sehemu kubwa zilichakaa. Kwa sasa serikali na menejimenti ya chuo imefanya juhudi ya kupata mashamba makubwa ya chuo yaani “Modal farms na tumepanda mazao yote ya kimkakati kama vile zabibu, korosho pamoja na chai” alisema Prof.Chibunda.

Aidha, katika kuimarisha utoaji wa elimu bora Chuo kimeboresha maeneo ya mifugo kama vile ngombe, samaki na maabara kwa lengo la wanafunzi kujifunzia kwa vitendo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...