*Abaini malipo hewa ya mabilioni ya fedha, mashirika mengine hoi kwa madeni

Na Ripota Wetu, Globu ya jamii

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Asaad ametoa ropoti ya ofisi yake kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ambapo imebaini uwepo wa ubadhirifu wa fedha katika maeno mbalimbali.

Ripoti hiyo ya CAG ni ile inayoishia kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2018 ambapo Profesa Assad anasoma ripoti hiyo leo kwa waandishi wa habari Mjini Dodoma ripoti hiyo inaonesha mashirika ya umma 14 yenye yana matatizo makubwa ya kifedha na kwamba baadhi ya mashirika yamepata hasara kiasi cha kusababisha  madeni zaidi ya mitaji yao kwa zaidi ya asilimia 100. 

"Ukiangalia ripoti hii inaonesha kati ya mashirika hayo 14,  mashirika 11 yanajiendesha kwa hasara kwa zaidi ya miaka miwili.Ni dhahiri mashirika hayo hayawezi kujiendesha bila kutegemea msaada kutoka Serikali Kuu. Kwa mazingira ya aina hiyo mashirika hayo hayaweza kujiendesha na kutoa huduma kwa jamii,"amesema.

Profesa Assad ameyataja baadhi ya mashirika hayo ni Kampuni ya Maendeleo ya Nishati ya Joto Tanzania (TGDC), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira  Dar es Salaam (DAWASA), Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Baraza la Taifa la Bishara, Baraza la Michezo la Taifa, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Mtwara, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Lindi na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Mwanza, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kampuni ya Usafirishaji na Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usambazaji wa Umeme, Bodi ya Utalii Tanzania, Kampuni ya Simu (TTCL – Pesa), Shirika la Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Dar es Salaam (DAWASCO) na Bodi ya Maziwa Tanzania.

Akizungumzia zaidi ripoti hiyo, Profesa Assad amesema kuwa ripoti imebaini katika ununuzi wa Mashine za Mfumo wa Kidigitali wa Usajili wa Wapiga kura (BVR) uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ilinunua mashine za BVR, 8,000 ili kusajili wapiga kura na kati ya mashine hizo 5,000 hazikukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.

Amesema kuwa hivyo imesababisha kutolandana kimatumizi na vile vilivyonunuliwa hapo awali na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Taifa wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini (RITA). "Hivyo kutolandana huko kumeisababishia hasara kwa Serikali Sh. milioni 862.08 zilizotumiwa na NIDA kununulia leseni mpya za “Windows” na “Biometric Algorithms” ili kubadilisha mashine 5,000 zilizopokelewa kutoka NEC ziweze kufanya kazi na mfumo wa BVR wa NIDA,"amesema.

Pia amesema ndani ya ripoti hiyo imebaini mzabuni alilipwa dola milioni 72.3 badala ya dola milioni 72.1 na kwamba kiasi hicho kilikuwa bei ya mkataba."Ukifuatilia eneo hilo utaona kuna ongezeko la dola 148,243.73. Wakati mafunzo kwa maofisa 15 wa TEHAMA wa NEC hayakufanyika licha ya mzabuni kulipwa dola 358,650 kwa ajili ya mafunzo hayo".

Wakati huo huo Profesa Assad amesema ripoti hiyo imebaini ndani ya
Jeshi la Polisi katika ununuzi wa sare za askari ambapo ukaguzi maalumu uliofanywa ndani ya jeshi hilo,umeonesha Polisi wamelipa Sh.bilioni 16.66 bila ya kuwepo ushahidi wa uagizaji na upokeaji wa sare za askari kwa Boharia Mkuu katika jeshi hilo.

Profesa Assad amesema ukaguzi huo umebaini kuna maoni ya kisheria ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanayohusu uwasilishaji wa kiapo cha nguvu ya kisheria na leseni halali ya biashara hayakuzingatiwa wakati wa kusaini Mkataba Namba. ME.014/PF/2015/2016/G/30 Lot 2, uliohusu ununuzi wa sare za askari polisi.

Amefafanua zaidi ripoti imebaini katika ukaguzi maalumu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS)kuna mambo yameonekana ambayo ni mahitaji ya kitaalamu kutoka idara inayotumia mfumo huo ambayo hayakuzingatiwa wakati wa kutathmini na kutoa zabuni.

Pia amesema kuna malipo ya Sh. bilioni 3.30 yalifanyika kwa mzabuni kwa ajili ya huduma ya matengenezo na msaada wa kitaalamu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole kwenye mikoa nane ya Kipolisi ya Temeke, Simiyu, Mwanza, Tabora, Rukwa, Kigoma, na Kinondoni Geita  lakini Polisi ilishindwa kuthibitisha kuwa matengenezo hayo na msaada wa kitaalamu ulifanyika. 


Profesa Assad amesema kwamba vifaa vya Utambuzi wa Alama za Vidole vyenye thamani ya Sh. bilioni 1.73 havikufungwa kwenye magereza 35 yaliyoainishwa badala yake vilihifadhiwa katika Ofisi ya Upelelezi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuongeza malipo ya Sh. milioni 604.3 kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika kwani Jeshi la Polisi lilishindwa kuwaonesha maofisi ya CAG monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya Sh. milioni 159.1 zilizopelekwa kwenye Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

"Ripoti inaonesha kuwa monita 213 za kompyuta aina ya Dell zililipiwa Sh.milioni 195.22 kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited lakini mzabuni hakuzileta,"amesema Profesa Assad.

Kuhusu malipo hewa ,Profesa Assad amesema ripoti imebaini katika uchunguzi wa vitabu vya fedha, taarifa za benki na hati za malipo za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kuna malipo ya Sh. bilioni 3, kati ya malipo hayo sh. bilioni 2.61 yalikuwa malipo hewa, sh. milioni 350.8 ni malipo ambayo walipwaji walishindwa kubainika na sh. milioni 42.6 hazikuweza kuthibitika kupokelewa na walipwaji. 


"Malipo hayo yalitakiwa kulipwa watoa huduma za afya kwa kutumia hundi zilizofungwa lakini yalifanywa kwa fedha taslimu kinyume na Kanuni za Fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.Makusanyo ya mwaka yanaendelea kuwa makubwa zaidi ya malipo ya huduma za bima ya afya, ambapo kwa sasa malipo ya huduma za afya yanakua kwa uwiano mkubwa mwaka hadi mwaka zaidi ya uwiano wa kukua kwa mapato,"amesema wakati anasoma ripoti hiyo.

Ameongeza kutokana na hali hiyo makisio ya madai ya huduma za bima ya afya pekee ifikapo mwaka wa fedha utakaoishia Juni 2024 yatakuwa ni asilimia 99.2 ya jumla ya makusanyo yote ambapo uwiano huu unakisiwa kuongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 104.8 katika mwaka unaofuata. Profesa Assad amesema uchunguzi wa vitabu vya fedha, taarifa za benki na hati za malipoza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umebaini uwepo wa Sh.bilioni tatu.

"Kati ya malipo hayo Sh.bilioni 2.61 yalikuwamalipo hewa, Sh. milioni 350.8 ni malipo ambayo walipwaji walishindwa kubainika na Sh. milioni 42.6 hazikuthibitika kupokelewa na walipwaji. 

Kwa upande wa udanganyifu katika halmashauri, Profesa Assad amesema kuna udanganyifu katika malipo ya Sh. milioni 267.89 kwenye akaunti ya matumizi mengine katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ambapo alikagua malipo mbalimbali katika akaunti ya matumizi mengine na kubaini kuwa kwa nyakati tofauti kuna watumishi walianzisha, kupitisha, na kufanya malipo ya ya Sh. milioni 267.89 ambayo hayakuwa na viambatisho husika.

"Na mengine yalikuwa na viambatisho vyenye shaka.Upotevu wa mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 3.4 katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’  ambapo mapitio ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umebaini upungufu ukiwemo wa halmashauri hiyo kushindwa kuwasilisha vitabu 425 vya kukusanyia mapato. 

"Mambo mengine yaliyobainika ni upotevu wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya sh. bilioni 1.04 yaliyokuwa yanakusanywa na mawakala, kutopatikana kwa nyaraka muhimu za makampuni ya mawakala wa ukusanyaji wa mapato kwa mikataba yenye thamani ya sh. bilioni 2.36 na malipo hewa ya sh. milioni 73.45 katika kandarasi za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.


"Pia ukaguzi maalumu umebaini kuwa fedha Sh. milioni 73.45 za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji zililipwa kwa wakandarasi kama dharura bila kuwepo kazi za dharura. Ukaguzi umebaini kutokuwepo kwa ushahidi wowote wa kufanyika kwa kazi hiyo na hivyo kudhihirika kuwa matumizi hayo ni hewa," amesema Profesa Assad.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...