Benny Mwaipaja, WFM, Washington DC

TANZANIA imeunga mkono uamuzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB wa kutaka kuongezewa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa mikopo kwa nchi wanachama wa benki hiyo kwa lengo la kuchochea zaidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa 7 wa magavana wa ambao ni Mawaziri wa Fedha kutoka nchi 54 wanachama wa Benki hiyo, Mjini Washington DC, Marekani, Waziri wa Fedfha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameeleza kuwa AfDB imefanya mambo makubwa nchini Tanzania ndio sababu inaunga mkono kusudio hilo.

Amesema kuwa Benki hiyo imeipatia Tanzania mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, kilimo, nishati na maji.

Benki inataka kuongezewa mtaji kwa asilimia 200 kutoka wastani wa UA bilioni 67.69 hadi UA 191.89 (kutoka dola za Marekani 94.76 hadi dola bilioni 268.6 ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii ya nchi wanachama hususan katika ujenzi wa reli, barabara, usafiri wa anga, tehama, bandari, uzalishaji na usambazaji wa nishati.

"Wakati umefika ili twende haraka zaidi, mitaji sehemu nyingine imepungua, pendekezo la kuongeza mtaji wa benki hii ni jema na matokeo ya miradi inayofadhiliwa na Benki hii yanaonekana katika nchi zetu za kiafrika kwa sababu benki hii iko Afrika na inaijua Afrika tofauti na benki nyingine" alisisitiza Dkt. Mpango

Uamuzi wa nchi za Kiafrika zenye hisa katika Benki ya Maendeleo ya Afrika ya kutaka Benki hiyo iongezewe mtaji ulitolewa wakati wa mkutano wa Magavana wa Benki hiyo mjini Rome, Italia, baada ya mahitaji ya nchi wanachama ya kutafuta mikopo kwenye taasisi hiyo kuongezeka.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kushoto) akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina, Mjini Washington DC, Marekani, kabla ya mkutano wa magavana wa Benki hiyo ambao ni Mawaziri wa Fedha kutoka nchi 54 zenye hisa kwenye benki uliofanyika katika ukumbi wa Willard Continental kujadili namna ya benki hiyo kuongezewa mtaji ili iweze kutoa mikopo kwenye nchi hizo kwa ufanisi zaidi
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akifuatilia kwa makini mjadala wa namna Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB inavyoweza kuongezewa mtaji, Mjini Washington DC, Marekani, ambapo Tanzania imeridhia hatua hiyo.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kulia) akifuatilia kwa makini mjadala wa namna Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, inavyoweza kuongezewa mtaji, Mjini Washington DC, Marekani, ambapo Tanzania imeridhia hatua hiyo.Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...