Na Ripota wa blog ya jamii,Tanga

VYOMBO vya habari nchini vimekumbushwa juu ya wajibu wa kuendelea kuzipa kipaumbele habari zinazohusu masuala ya watoto na kufichua vitendo vyote vya ukatili wanavyotendewa ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo hivyo.

Hayo jana Mkoani Tanga, na kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile  wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za uandishi wa habari za watoto zinazoandaliwa na TEF kwa ushirikiano na Shirika la watoto ulimwenguni (UNICEF) Tawi la Tanzania.

Balile alisema iwapo vyombo vya habari nchini vitajenga utamaduni wa kutoa kipaumbele kwa habari za watoto ni wazi serikali na wadau wengine wa watoto wataweza kuchukua hatua madhubuni za kuhakikisha mtoto wa Tanzania analindwa na kupata haki zake za msingi.

“Lengo letu tukiwa waandishi wa habari ni kuangalia ni jinsi gani habari za watoto zinazoandikwa zitawasaidia watoto hapa nchini kuwaondolea ugumu  wa maisha ya katika sehemu mbalimbali kwa kuwashirikisha kiuchumi, ili tuwasaidie kuondokana na ugumu walionao hivi sasa na waishi maisha bora zaidi,” alieleza Balile.

Pia Balile alilishukuru shirika la UNICEF kwa ushirikiano mkubwa ambao linautoa kwa Jukwaa la wahariri hapa nchini ikiwemo kusaidia mafunzo mbalimbali kwa waandishi wa habari ambayo yameweza kuwajengea uwezo wa kuandika habari za watoto ambazo zimeanza kuleta matokeo mazuri kwa hivi sasa.

 Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Manisha Mashira aliwapongeza washindi wote 10 walioshinda tuzo hiyo kwa mwaka huu wa 2019 ambapo alisema wao binafsi wamefurahishwa na kazi nzuri zilizofanywa na waandishi hao na kuwataka waongeze bidii zaidi.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza waandishi wote mlioshinda kwa mwaka huu na kupewa Tuzo ya uandishi wa habari za masuala ya uchumi kwa watoto, tuzo hizi zimeonesha jinsi gani mnavyoandika habari kwa ajili ya kuwasaidia watoto,”

“Niwapongeze pia viongozi wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) kwa juhudi wanazozifanya kwa lengo la kuwasaidia waandishi wa habari hapa nchini na niombe tuendelee kujitahidi katika kuijenga Tanzania, kwa upande wetu UNICEF tutaendelea kuwaunga mkono katika masuala yanayohusu watoto,” alieleza Manisha.

Awali mmoja wa wajumbe wa baraza la TEF, Absalom Kibanda alitoa historia fupi ya jinsi kundi la wahariri lilivyoanzishwa mnamo mwaka 2017  likiwa na wahariri 15 ambapo moja ya malengo yake ni kuangalia jinsi gani waandishi watatumia kalamu zao kutetea haki za watoto.

Kibanda pia aliwapongeza washindi wa tuzo hiyo kwa mwaka huu ambapo alisema TEF iliamua kubeba dhima ya kuielimisha jamii na kutetea haki za mtoto kama msingi wa kuweka msukumo kwa serikali na taasisi nyingine za umma na binafsi kuweza kutambua masuala ya haki za msingi za mtoto.

Akitangaza rasmi majina ya washindi, katibu wa TEF, Neville Meena aliwakumbusha waandishi wote umuhimu wa kuendelea kuandika habari zinazohusu watoto kwa kuangalia pia katika halmashauri zao ni kiasi gani cha fedha kinatengwa katika bajeti za kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa masuala ya watoto.

Washindi waliotangazwa na kupewa Tuzo kwa mwaka huu wa 2019 ni pamoja na mwandishi wa gazeti la Majira, Suleiman Abeid kutoka Shinyanga, Lilian Lugakingira (Nipashe), Rehema Matowo (Mwananchi) na Sifa Lubasi (Habari Leo).

Wengine ni Anne Robi (Daily News) ambaye pia alikuwa mshindi wa Tuzo ya jumla, Tumaini Msowoya (Mwananchi), John Kabambala (TKT Morogoro), Mwanzani Kiembe (ABM Dodoma), Arnold Jovin (Radio Kwizera) na Angelina Lukindo (Upendo Radio) huku Anne Rhobi(Daily News)akiibuka mshindi wa Jumla katika tuzo hizo.
 Mshindi wa jumla tunzo za kuandika habari za watoto Anne Rhobi kutoka gazeti la Daily News akipokea zawadi yake kutoka kwa mwakilishi wa UNICEF Tanzania Manisha Mashira.
 
 Baadhi ya waandishi washindi wa tuzo za habari za uandishi.wa watoto wakiwa na vyeti vyao vya ushindi.
 Picha ya pamoja

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...