Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Roche ya nchini Kenya imeandaa mkutano wa kisayansi wa kuwajengea uwezo wataalam wa Radiolojia, Pathiolojia, Upasuaji, tiba ya mionzi na dawa kufanya upasuaji wa saratani ya matiti kwa kutoa uvimbe bila kuondoa titi lote kwa wagonjwa wenye dalili za mwanzoni.

Mkutano huo wa kisayansi ambao ni wa kwanza kufanyika katika Hospitali ya Mloganzila umefunguliwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Prof. Lawrence, umelenga kukumbushana namna bora ya kuwapatia matibabu kwa njia ya kisasa wagonjwa ambao wamethibitika kuwa na saratani ya matiti. Mafunzo hayo yanashirikisha wataalam 30 kutoka Muhimbili pamoja na Hospitali za rufaa nchini ambazo ni Bugando, KCMC, Mbeya na Hospitali binafsi ya Besta.

Kupitia mtaalam mbobezi kutoka Nairobi, Kenya Dkt. Peter Bird, wataalam hao watapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa muda wa siku nne ambapo pia mada mbalimbali zinazohusu utoaji wa matibabu ya saratani ya matiti zitawasilishwa.

“Nichukue fursa hii kuwashukuru kampuni ya dawa ya Roche kwa kushirikiana na hospitali yetu ili kuwajengea uwezo wataalam hapa nchini kwani wataalam watakaofaidika na mafunzo haya wataenda kuwajengea uwezo wataalam wengine”. Amesema Prof. Museru Akifafanua amesema saratani ya matiti inachangia vifo kwa wanawake duniani kwa asilimia 25 hadi 35, pia saratani ya matiti ipo kwa kiwango cha juu katika nchi zilizoendelea kuliko nchi zinazoendelea japokuwa vifo vingi vinavyotokana na saratani hiyo hutokea katika nchi zinazoendelea kutokana na wagonjwa kuchelewa kufika hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Kwa Tanzania saratani ya matiti ni ya pili kwa kusababisha vifo kwa wanawake wenye saratani ikiongozwa na saratani ya shingo ya kizazi, pia katika wanawake 20, mmoja wao yupo kwenye hatari ya kupata saratani hii ya matiti. Vilevile inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wanaothibitika kuwa na saratani ya matiti nchini Tanzania wanafika hospitalini wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne ya ugonjwa ambapo matibabu yake yanakuwa hayatoi matokeo mazuri.

Wakati huohuo, Kampuni ya dawa ya Roche imeipatia Hospitali ya Mloganzila msaada wa vifaa tiba (Biopsy gun and needle) vitakavyotumika kuchukua sampuli ya uvimbe kwa mgonjwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili -MNH- Prof Lawrence Museru akifungua mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo wataalam wa Radiolojia, Pathiolojia, Upasuaji, tiba ya mionzi na dawa namna bora ya kufanya upasuaji wa saratani ya matiti kwa kutoa uvimbe bila kuondoa titi lote kwa wagonjwa wenye dalili za mwanzoni.
Washiriki wa mafunzo hayo pamoja na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mloganzila wakimsikiliza Prof. Museru wakati akizungumza katika mafunzo hayo ambayo yanafanyika katika Hospitali ya Mloganzila.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akiwasilisha mada kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti nchini katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na MNH kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Roche.
Dkt. Stephen Maina kutoka Roche (wa kwanza kulia) akimkabidhi msaada wa vifaa tiba Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Prof. Lawrence Museru (Biopsy gun and needle) vitakavyotumika kuchukua sampuli ya uvimbe kwa mgonjwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru (wa pili kutoka kushoto kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo, anayemfuatia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi, wa kwanza kulia ni Dkt Stephen Maina. (kushoto) ni Mkurugenzi wa Upasuaji Dkt. Deogratius Masatu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...