*Azindua mabweni ya wanafunzi wenye ulemavu wa macho Tuangoma
* Aiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi kwa tenda za miradi ya DMPD
Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameendelea na ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika halmashauri ya Temeke ambapo amekagua ujenzi barabara ya Usalama Chang'ombe, ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya Sekondari kijichi mradi unaofadhiliwa na TAMISEMI, ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho ambapo pia ameweka jiwe la msingi, ujenzi wa mradi wa kisima cha maji katika kata ya Charambe pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Yombo Vituka.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara hiyo Makonda ameipongeza halmashauri hiyo kwa kusimamia vyema miradi hiyo hasa ya barabara ambapo wameokoa gharama kubwa na kujenga barabara imara kwa milioni 900 kwa kilomita moja ukilinganisha na halmashauri ya Kinondoni inayojenga barabara ya kilomita moja kwa zaidi ya shilingi bilioni 2 ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa TAKUKURU wa Mkoa huo kufanya uchunguzi wa utaratibu wa upatikanaji wa tenda kwenye miradi inayofadhiliwa na benki ya dunia (DMDP) baada ya kubaini matumizi mabaya ya fedha za serikali katika miradi hiyo kwa baadhi ya maeneo ya miradi.
Makonda amesema haiwezekani Kilomita Moja ya barabara ya Wilaya ya Kinondoni ikajengwa kwa Shilingi Billion 2.7 wakati kwa Wilaya ya Temeke barabara kama hiyo inajengwa kwa shilingi Milioni 900 pekee na yote inafadhiliwa na benki ya dunia.
Aidha Makonda amesema kuwa wazawa wawe mstari wa mbele kuomba tenda za kusimamia miradi ya fedha nyingi ili kuweza kujitangaza na kuongeza ujuzi zaidi na sio kuyaachia makampuni makubwa pekee.
Vilevile Makonda ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuwatazama watu wenye mahitaji maalumu kwa kujenga mabweni ya wanafunzi wenye ulemavu na amewataka kuwatazama watoto kutoka sehemu nyingine ili waweze kunufaika na fursa hiyo.
Ameeleza kuwa nafasi zitakazosalia katika bweni hilo wachukuliwe wanafunzi kutoka maeneo mengine kwa kuwa mradi huo ni wa pekee na maalumu katika mkoa huo na amezitaka halmashauri nyingine kuiga kutoka kwa wana Temeke.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiweka jiwe la msingi la ujenzi
wa madarasa, vyoo na mabweni katika shule ya msingi Tuangoma jijini Dar
es Salaam.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akisaini kitabu cha wageni mara
baada ya kuwasili katika shule ya sekondari Kijichi ambapo alizungumza
na wanafunzi na kuwataka kuzingatia masomo na kuweka mbele nidhamu,
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi akizungumza na wanahabari mara
baada ya zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa,
mabweni na vyoo katika shule ya msingi Tuangoma jijini Dar es Salaam.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akitoa maelekezo mara baada ya
kukagua ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika
shule ya msingi Tuangoma, jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...