Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Wadau wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini leo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es salaam.(Picha na Emmanuel Masska,MMG)
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi akieleza jambo kuhusu mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini baada ya kupewa fursa ya Kumkaribisha mgeni rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu katika ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini ulio fanyika leo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim (katikati) akiwa na baadhi ya wadau wa masuala ya Kifua Kikuu wakijadi mambo mbalimbali katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa Wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa huo nchini leo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Wadau wa masuala ya Kifua Kikuu wakifuatilia neno kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha) katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa Wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa huo nchini leo kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es salaam.
Moja ya kikundi ambacho kimekuwa kikishiriki katika kampeni ya kupiga vita ugonjwa wa kifua kikuu kikitumbuiza katika mkutano huo.


Na WAMJW – DSM 

Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa viongozi wa madhehebu ya dini na Waganga wa tiba asili ni nguzo muhimu sana katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu(TB) nchini. 

Ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam 

Waziri Ummy amesema kuwa Waganga wa Jadi na Viongozi wa Dini ni Wadau muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB, huku akidai kutokana na utafiti uliofanywa 2018 na Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma unaonesha kuwa waganga wa jadi wamekuwa wahanga wakubwa wa ugonjwa wa kifua kikuu. 

Aliendelea kusema kuwa, viongozi wa dini ni kundi lingine muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini, hii ni kutokana na idadi kubwa ya waumini wanaowaamini katika kufikisha ujumbe. 

“Waganga wa jadi, ni wadau muhimu sana katika mapambano ya kifua kikuu, utafiti wa 2018 uliofanywa na mpango wa taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma unaonesha kuwa Waganga wa jadi na wenyewe wamekuwa wahanga wa ugonjwa wa kifua kikuu, na viongozi wa dini tunawahitaji wanaposimama katika makanisa na katika misikiti yetu ili wawe wanawakumbusha waumini juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu” alisema Waziri Ummy 

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa 2017, Tanzania iligundua na kuwapatia matibabu takribani wagonjwa 75,000 ikiwa ni sawa na 44% tu ya wagonjwa wanaokadiriwa kuugua TB, hii ina maana ya kuwa wagojwa 85,000 (56%) hawagunduliwi na hivyo kukosa matibabu kila mwaka nchini. 

Pia, Waziri Ummy amesema kuwa TB huathiri takriban watu milioni 10.4 duniani kila mwaka na 25% ya wagonjwa wanatoka barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 barani Afrika zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa TB na inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa TB 154,000 kila mwaka. 

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi, hali iliyoleta mafanikio ikiwamo kuvuka malengo ya mwaka 2018 ambapo tuliwafikia wagonjwa 75,845 ikiwa ni sawa ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015. 

Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammad Bakari Kambi amesema kuwa Tanzania ina wastani wa jumla ya Wagonjwa 154,000 ambao wanatakiwa kuibuliwa na kuanzishiwa matibabu, licha ya changamoto ya kutowafikia wote ametoa wito juu ya umuhimu wa ushirikishwaji wa watu na taasisi mbali mbali ili kurahisisha mapambano haya dhidi ya ugonjwa wa TB. 

Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt.Beatrice Mutayoba amesema kuwa kila mwaka watoto 1,000,000 wanaugua kifua kikuu Duniani, huku watoto 250,000 wanafariki. 

“Kwa bahati mbaya Kifua kikuu hakijaacha watoto, kila mwaka watoto 1,000,000 wanaugua kifua kikuu Duniani, huku watoto 250,000 wanafariki, huku nchini Tanzania 10% ya watu 68,000 wanaogundukila kuwa na Kifua kikuu huwa ni watoto” alisema Beatrice Mutayoba 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...