Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mkurugenzi  Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, Hisham Hendi raia wa Misri, wafanyakazi wake wanne, raia wa Kenya, kampuni ya Vodacom na Tala Tanzania kurejesha kiasi cha sh. Bil. 5,892,513,000 walichoisababishia hasara serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuingiza, kusimika vifaa ya mawasiliano bila kibali cha TCRA.

Washtakiwa pia wanadaiwa kuruhusu line 813 za Vodacom ambazo hazijasajiliwa  kutumika. Washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, likiwemo  shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya bilioni 5.2.

Mbali na Hendi, washtakiwa wengine waliohukumiwa ni Joseph Nderitu, Mkuu wa Kitengo cha Mapato Vodacom, Olaf Mumburi, Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Vodacom, Joseph Muhere, Mkuu wa Mauzo wa Vodacom na Meneja Mhasibu Ibrahim Bonzo.

Wengine ni,  Ahmed Issa ambaye ni Meneja uwendeshaji wa biashara wa kampuni ya In venture Mob Tanzania Ltd,  raia wa Kenya na Brian Lusiola ambaye ni mtaalamu wa IT. Pia washtakiwa hao wamehukumiwa kulipa fine ya jumla ya sh. Mil.120 na iwapo wakishindwa basi watatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Washtakiwa wamesomewa adhabu hizo baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yanawakabili  kufuatia upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi dhidi ya washtakiwa hao umekamilika na washtakiwa kusomewa mashtaka upya.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi amesema, katika shtaka la kwanza hadi la sita washtakiwa, Ngassa, Lusiola na kampuni ya Inventure/ T/A Tala Tanzania anahukumiwa kulipa faini ya Sh. Milioni tano kila mmoja katika kila shtaka na iwapo watashindwa basi watatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Katika shtaka la saba, washtakiwa, Ngassa, Luisola na Tala wamehukukiwa kulipa 642,276,000  ambazo waliisababishia TCRA hasara kwa kutumia laini 813 za Vodacom ambazo hazijasajiliwa na wakishindwa watarudishwa mahakamani kupangiwa adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.
Aidha katika shtaka la nane, washtakiwa Hendi, Nderitu,Mumburi, Muhere, Bonzo na Kampuni ya Vodacom wamehukumiwa kulipa faini ya sh. Milioni tano kila mmoja au kwenda jela miezi 12.

Katika shtaka la tisa washtakiwa hao wamehukumiwa kurejesha sh. 5,250,237,000  kama hasara waliyoisababisha kwa TCRA wakishindwa watarudishwa mahakamani kupangiwa adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.

Mapema kabla ya kusomewa adhabu, hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Jackline Nyantori aliiiomba mahakama kutoa adhabu kali ambayo itakuwa  fundisho kwao na kwa wengine wanaotenda makosa kama haya au wanaotarajia kutenda makosa kama haya.

Nao washtakiwa wakijitetea kupitia wakili wao Seni Malimi waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu washtakiwa kwani ni wakosaji wa kwanza. Hata hivyo, washtakiwa wamelipa faini na kurejesha fedha hizo na kunusurika kwenda rumande.

Awali ilidaiwa, kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2018, huko katika jengo la Tanzanite Park, lililopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa Ngasa, Lusiola na kampuni ya Tala Tanzania  waliingiza kifaa cha mawasiliano kinachoitwa Proliant MLI GEN 9 Server (PABX Virtual Mashine yenye serial number 76520D88838129_425) bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Washtakiwa wanadaiwa pia kusimika kifaa hicho na kuendesha mtambo huo wa mawasiliano bila kuwa na leseni inayotolewa na TCRA. Aidha  washtakiwa wanadaiwa, kutoka Januari 2 hadi  Machi 11,2019 waliendesha kifaa hicho cha kieletroniki cha mawasiliano kwa kurusu simu za kimataifa zilizoingia nchini bila kibali cha TCRA.

Pia imedaiwa kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, washtakiwa waliendesha mitambo hiyo kwa kupokea na kusambaza upokeaji wa simu za kimataifa bila kuwa na leseni hiyo. Katika shtaka la tano inadaiwa kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu, washtakiwa walikwepa kodi ya kupokea na kusambaza huduma ya upokeaji wa simu za kimataifa kwa kusambaza mawasiliano kwa kutumia mfumo huo.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu kinyume na sheria, washtakiwa walitumia vifaa vya mawasiliano kuunganisha  huduma ya kieletroniki ya mawasiliano kwa lengo la kupokea na kusambaza mfumo wa mawasiliano bila kupata kibali cha TCRA.

Imeendelea kudaiwa kuwa, katika tarehe hizo, maeneo ya Tanzanite Park Building Kinondoni, Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Tala, walitumia namba 813 za Vodacom ambazo ni namba maalum bila kupewa na TCRA. Ngassa, Lusiola na Tala, pia wanadaiwa katika tarehe hizo, waliisababishia TCRA hasara ya Sh Milioni 642.2.

Katika shtaka la Tisa, Wakili Wankyo Simon amedai kuwa Hendi, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Kampuni ya Vodacom, kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu maeneo ya jengo la Vodacom, lililopo Ursino Estate barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam, waliwaruhusu  Ngassa, Lusiola na Tala kutumia namba 813 za Vodacom bila kuzipata kutoka TCRA.

Pia Simon alidai washitakiwa hao kutoka Vodaom katika tarehe hizo, kwa pamoja waliisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh 5,250,237,000.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...