Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
MAMLAKA ya Maji safi na Majitaka Dar es Salaam DAWASA imejipanga kuwapotia wamiliki wa visima vya maji kwa lengo la kupima ubora wa maji  na kuwapatia leseni ya usambazaji maji kwa wananchi.

Hayo yamezungumzwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya mamlaka hiyo na ile ya jamii. Luhemeja amesema wenye mamlaka ya kusambaza maji kwa mkoa wa Dar es Salaam ni Dawasa kwahiyo wamejipanga kuweza kupitia kwa wamiliki wote wa visima kwa ajili ya kuvipima na kuthibitisha ubora wa maji.

Amesema wameanza kuvitambua visima vyote vinavyotoa huduma ya maji na kupima maji yake bure ili wakazi wapate maji safi na salama. “Kuna miradi ya jamii ambayo kuna visima vimechimbwa na Halmashauri, kuna vya Dawasa pia vipo vilivyochimbwa na wananchi wenyewe na kuwauzia maji watu wengine kwa hawa lazima tuwapitie na kupima ubora wa maji kama yanafaa kwa matumizi,”amesema Luhemeja.

Amesema, “wamiliki hao wasione kama tunataka kuwakataza kuuza maji kwa wananchi, kila mmiliki atapatiwa leseni kutoka Mamlaka husika ya kusambaza maji safi na salama,” Luhemeja ameeleza kuwa wameshavikagua visima 47 na takribani 10,770 wanatumia maji hayo  na lengo ni kuona wananchi wanatumia kitu kizuri na kuondokana na kero ya magonjwa ya mlipuko.

Katika ziara hiyo, Luhemeja aliweza pia kutembelea miradi mingine mbalimbali ambapo alitembelea ujenzi wa mradi wa Kiwalani Phase 3 ambapo ameeleza changamoto kubwa iliyokuwepo kwenye maeneo hayo kwa kukosekana kwa mtandao wa maji na wananchi kupelekea kutumia maji yasiyokuwa safi na salama.

“Ukiangalia kila inapotokea magonjwa ya mlipuko utasikia Kiwalani ndipo inapoanzia, ila kwa sasa tunaleta mradi wa maji na utakamilika kufikia Mwezi June mwaka huu, utawasaidia wananchi wa Buza na Kiwalani na kuondokana na kero ya kutumia maji yasiyo salama,”amesema Luhemeja.

Ujenzi wa mradi wa maji wa Kiwalani Phase 3 unatumia fedha za ndani na mabomba yatasambazwa kwa Kilomita 60 kwenda mpaka Yombo, Buza, Mwanagati Na Kitunda ukijengwa na wakandarasi wa ndani na kupunguza gharama.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja (katikati) akipata maelezo toka kwa Kaimu Meneja wa Miradi ya Maji Mhandisi Ramadhani Mtindasi mara baada ya kufika kukagua Tenki la maji la Mabwepande litakalohudumia wananchi wa Bunju, Kitunda na Mabwepande. Pembeni kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Miradi Mhandisi Lydia Ndibalema.
 Mafundi wakiendelea na ulazaji wa mabomba katika Ujenzi wa mradi wa Kiwalani Phase 3 wenye urefu wa Kilomita 60 unaojengwa kwa fedha za ndani za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA na utakaoweza kuhudumia  wananchi wa Buza, Kiwalani, Mwanagati, Yombo na Kitunda na kuondokana na kero ya magonjwa ya milipuko na kupata maji yaliyo safi na salama.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na wataalamu wengine wa Mamlaka hiyo wakikagua muendelezo wa ujenzi wa tenki la Kibamba litakalohudumia mpaka Kisarawe likiwa katika hatua za mwisho.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na wanahabari baada ya kukagua ulazaji wa mabomba ya inchi 8 yenye urefu wa Km 2.5 kwenye ujenzi wa mradi wa maji wa Mwabepande unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...