Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Godfrey Mbawala akizungumza na madaktari bingwa wa magonjwa ya
moyo kutoka Hospitali kuu ya jimbo la Shandong la nchini China walipotembelea taasisi
hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Na Zawadi Masinde - JKCI
24/04/2019 Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu ya
jimbo la Shandong nchini China wanatarajia kuja nchini mwezi wa nane mwaka
huu kwa ajili ya kufanya kambi maalum ya matibabu ya moyo katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao cha pamoja cha viongozi kutoka
Hospitali hiyo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kilichofanyika jijini Dar es
Salaam..
Akizungumza katika kikao hicho Kiongozi wa msafara huo Wang Zhifeng alisema
wataalamu hao ambao watakuja nchini watafanya upasuaji wa moyo wa kufungua
na bila kufungua kifua pia watabadilishana ujuzi wa kazi na wenzao wa JKCI
“Wataalamu wetu kutoka Hospitali ya Shandong wakija hapa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete watakuja na vifaa tiba ambavyo watavitumia katika upasuaji
watakaoufanya. Pia mtatuambia ni vifaa gani vingine ambavyo mnavihitaji ili
wataalamu wetu watakapokuja waje navyo”, alisema Zhifeng.
Aliendelea kusema kuwa kabla ya kuja kwa wataalamu hao hapa nchini kutaanza
na program ya madaktari, wauguzi, wataalamu wa usingizi, mafundi sanifu wa
moyo na Wahandisi wa vifaa tiba kwenda katika Hospitali hiyo kwa ajili ya
mafunzo ya muda mfupi ya magonjwa ya moyo na mashine za moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi
aliwashukuru viongozi hao kwa kutembelea Taasisi hiyo na kusema kuwa kuja
kwa wataalamu hao ni matokeo ya mkataba wa mahusiano uliosainiwa mwezi wa
nane mwaka jana.
Makubaliano yaliyosainiwa katika mkataba huo ni kutolewa kwa mafunzo ya
muda mfupi kwa madaktari, wauguzi, mafundi sanifu wa moyo na wahandisi wa
vifaa tiba, kujenga jengo jipya la Taasisi hiyo, kutoa msaada wa vifaa tiba na
kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo ambazo zitasaidia kuwajengea
uwezo wataalam wa hapa nchini.
Naye Mratibu wa ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta ya Afya Dkt.
Ligile Vumilia alisema makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho ni lazima
yafanyike kwa wakati na kwa manufaa ya nchi kwani hakuna Taasisi itakayotoa
matibabu ya moyo zaidi ya wataalamu waliopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete.
Hospitali kuu ya jimbo la Shandong inautaalamu wa hali ya juu wa kutibu
magonjwa ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa kufungua na bila
kufungua kifua ambapo kwa mwaka 2018 ilifanya upasuaji wa moyo kwa
wagonjwa 85,000.
Daktari wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Hospitali kuu ya jimbo la
Shandong la nchini China anayejitolea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zhao
Lijian akiwaelezea madaktari wenzake kutoka China namna ambavyo anatoa huduma ya
matibabu ya moyo kwa watoto walipotembelea taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi akizungumza na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu ya
jimbo la Shandong la nchini China walipotembelea taasisi hiyo na kuahidi kushirikiana na
taasisi hiyo kuboresha sekta ya afya ikiwemo afya ya moyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi (katikati) akipokea zawadi ya picha ya Shandong kutoka kwa kiongozi wa madaktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu ya jimbo la Shandong la nchini China
Wang Zhifeng walipotembelea taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam na kuahidi kuendelea
kushirikiana na taasisi hiyo katika kubadilishana ujuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi katika picha ya pamoja na menejimenti ya taasisi hiyo na madaktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu ya jimbo la Shandong la nchini China
walipotembelea taasisi hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya
ikiwemo magonjwa ya moyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi akifafanua jambo alipokua akizungumza na madaktari bingwa wa magonjwa ya
moyo kutoka Hospitali kuu ya jimbo la Shandong la nchini China walipotembelea taasisi
hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika kutoa huduma za matibabu ya moyo leo
Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Angela Muhozya akielezea namna idara ya upasuaji inavyofanya kazi alipokua
akizungumza na baadhi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu
ya jimbo la Shandong la nchini China walipotembelea taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...