Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameutaka uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuona namna bora ya kuhuwisha mitaala ya Chuo hicho ili kifikie viwango vya Elimu ya Juu.

Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amesema mpaka sasa Chuo hicho kimekidhi viwango vya kuwa na hadhi ya Chuo Kikuu na kwamba elimu inayotolewa katika chuo hicho ndio inasisitizwa nchini.

Ameutaka uongozi wa chuo hicho kutia mkazo katika mafunzo ya uongozi na maadili hususan yale yenye mwelekeo wa kujenga uzalendo na kuendelea kutumia fursa ya uwepo wa makongamano kukuza uelewa wa jamii ya watanzania kuhusu umuhimu wa kuenzi falsafa za mwalimu katika umoja, upendo, uzalendo, uadilifu na mshikamano wa kitaifa.

Aidha Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga misingi ya Amani, umoja na kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na kuwataka watanzania kuzingatia maadili, uzalendo na utaifa katika uwajibikaji wa kila siku, kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au kabila katika kulinda na kudumisha tunu hizo.

“Nimpongeze Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazochukua ili kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya awali ambayo ni kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda Amani na kudumisha umoja katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi na kuzilinda kwa nguvu zote,” alisema Mhe. Majaliwa.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ni vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.

Waziri Ndalichako ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wanafunzi katika kongamano hilo kwa kuwa linawapa fursa ya kupata uelewa mpana wa zaidi ya kile wanachofundishwa shuleni, na kwamba taifa linawategema kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya uendeshaji wa Chuo cha Kumbu Kumbu ya Mwalimu Nyerere Steven Wassira alimweleza Waziri Mkuu kuwa wanaomba katika kumenzi Baba wa Taifa Chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa Chuo Kikuu na kwamba mazingira yake yaboreshwe yawe na hadhi ya Hayati Baba wa Taifa.

Kwa upande wake mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila amesema, uongozi wa chuo hicho unaendelea na maboresho ya kutoa taaluma yenye kujenga uzalendo kwa vijana wa kitanzania.

Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa limechagizwa na mada isemayo Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Amani, umoja na Kuleta Maendeleo ya Jamii nchini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Wananchi waliohudhuria Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Kivukoni
Mwenyekiti wa Bodi ya uendeshaji wa Chuo cha Kumbu Kumbu ya Mwalimu Nyerere Steven Wassiraakizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kongamano hilo Jaji Joseph Warioba akizungumza wakati wa kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere.
Waziri wa Elimu , Profesa Joyce Ndalichako akizungumza kukubali kuwa atafanyia kazi Ombi la chuo cha Mwalimu Nyerere kuwa Chuo Kikuu
mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila, akizungumza juu ya maboresho yaliyofanyika chuoni hapo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sara Msafiri mara alipowasili katika ukumbi wa Mkutano
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano hilo wakifuatilia mada mbalimbali zinazojadiliwa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...