*Yakutana na wadau kujadili namna ya kuimarisha soko, ubora wa ngozi

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imewahamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kupenda kununua bidhaa za ndani na hasa bidhaa zinazotokana na mazao ya ngozi huku ikiweka wazi mikakati yake katika kuhakikisha ngozi za Tanzania zinaendelea kuwa bora.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya wadau wa ngozi nchini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel amesema ipo haja ya Watanzania kuhakikisha wananunua bidhaa zitokanazo na mazao ya ngozi ambazo zinatengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi badala ya kununua bidhaa za ngozi zinazotoka nchi nyingine.

"Tunatoa rai kwa wananchi wote tujenge tabia ya kupenda bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi yetu na hasa bidhaa za ngozi kama viatu, mkanda, mikoba na aina nyingine ya bidhaa.Binafsi viatu vyangu ambavyo nimevaa vimetokana na ngozi ya mifugo ya kwetu na kiwanda ambacho kimetengeneza nacho ni cha hapa hapa Tanzania.

"Ni viatu vizuri sana na kwa bei nafuu.Hivyo hakuna sababu ya kununua bidhaa za ngozi ambazo zinatoka nje wakati kwetu uwezo wa kutengeneza tena katika kiwango bora upo,"amesema Profesa Gabriel.

Kuhusu ubora wa ngozi, Profesa Ole Gabriel amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati mbaimbali ya kuhakikisha ngozi ambayo inatokana na mifugo iliyopo nchini Tanzania inaendelea kuwa bora ambapo amefafanua umefika wakati wa kuhakikisha ng'ombe wanaandaliwa tangu wanapozaliwa ngozi yao inalindwa ili iwe bora zaidi na hiyo si tu itafanya kuwepo na ngozi bora bali kuongeza thamani ya ngozi na bidhaa zake.

"Tumekutana na wadau wa ngozi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu, tumejadili mafanikio na changamoto na kwa pamoja tumekubaliana kuendelea kushirikiana kuhakikisha bidhaa zetu za ngozi zinapata nafasi ya kununuliwa na Watanzania.Wote tuwe na utamaduni wa kupenda vya kwetu kwani kuna baadhi ya watu wana ugonjwa wa kuona vinavyotoka nje ndio bora kuliko vya kwetu wakati si kweli.Bidhaa zinazozalishwa nchi ni bora , hivyo nitoe rai tununue vya kwetu,"amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu soko la bidhaa zitokanazo na ngozi, amesema Wizara yao inawahakikisha wadau wa ngozi kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika ambapo ameahidi kuendelea kufanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na wadau wengine kwani dhamira ya Serikali ni kujenga viwanda na hivyo kuna kila sababu ya uwepo wa viwanda vya ngozi. "Tutahakikisha tunakuwa na soko la uhakika katika bidhaa za ngozi hasa katika kipindi hiki cha ujenzi wa viwanda ambapo tunataka kuwepo na viwanda vya bidha za ngozi."

Wakati huo huo, Profesa Ole Gabriel amesema wamepokea ombi la wadau wa ngozi la kutaka iwepo bodi ya ngozi ambayo itasimamia sekta ya ngozi nchini na kwamba ombi hilo wamelipokea na Wizara italifanyika kazi kwani lina tija na nia njema.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa Ngozi chini Joram Wakari amesema kwa sasa wanakwenda vizuri kutokana na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha sekta ya ngozi inapewa kipaumbele nchini na tayari kuna mafanikio.
"Tukiri kuna mafanikio makubwa katika eneo hili la sekta ya ngozi.Hivyo iwapo changamoto chache zilizopo zikiondolewa tutafanya vizuri zaidi ya tunavyofanya sasa.Nitoe ombi kwa Wizara ni vema ikaanzisha Bodi au Mamlaka ya kusimamia sekta ya ngozi kwani kukosekana kwa chombo maalumu kwa ajili ya ngozi kuna mambo yanashindwa kutatuliwa kwa wakati,"amesema Wakari.

Wakati huo huo Meneja wa Operesheni wa Woiso Original Products Co Teya Herman amesema ombi lao kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusaidia kuzuia uingizwaji wa bidhaa za ngozi kutoka nje ambazo ziko chini ya ubora na zinapoingia nchini zinauzwa kwa bei ya chini na hivyo kusababisha wao kukosa soko.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Profesa Elisante Ole Gabriel (katikati) akizungumza na wadau wa ngozi nchini kuhusu namna ya kuimarisha sekta ya ngozi nchini na bidhaa zake
Mkurugenzi Mtendaji wa Woiso Original Products Co Kenneth Woiso(kulia) na Meneja Opereshenj wa Woiso Original Products Co Teya Herman wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) baada ya wadau wa ngozi kukutana kujadili sekta ya ngozi nchini.
 Baadhi ya wadau wa sekta ya ngozi nchini walioshiriki kikao cha wadau wa ngozi kilichoitishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...